Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

Hizi ndizo sababu za Petro kukataa unabii huu

 *ASALI MUBASHARA-Jumapili 12/09/2021*


*DOMINIKA YA 24 YA MWAKA B WA KANISA*


Karibuni ndugu zangu kwenye adhimisho la misa takatifu Jumapili ya leo. Leo basi ni Jumapili ya 24 ya mwaka B wa Kanisa na ujumbe wa neno la Mungu unaongozwa na zaburi yetu ya wimbo wa katikati” nitaenenda mbele za Bwana katika nchi ya walio hai” haya ni maneno ya zaburi ya 116 ikituambia tuenende katika njia ya Bwana na kutenda njia hizo. 


Zaburi inaendelea kusema kwamba anayeenenda katika njia hizi, alizungukwa na maadui lakini basi akawashinda wote. Zaburi hii ni ushuhuda wa Daudi mwenyewe ambaye katika historia ya maisha yake basi alipata kuenenda katika njia ya Bwana, hakuichagua njia ya muovu na kweli akashinda. Njia ya Bwana ni ulinzi tosha, hutoa ulinzi wa hali ya juu kabisa tofauti na njia ya shetani. Njia ya shetani ni wasiwasi na anayetenda uovu kila mara yupo kwenye wasiwasi. Bwana atakuokoa na hata ukipatwa na mateso basi atakupigania.


Zaburi hii inatumika kutilia mkazo juu ya ujumbe wa somo la kwanza. Tunaona kwamba aliyeenenda kwenye hii njia ya Bwana ni yule mtumishi mwaminfu wa nabii Isaya. Na kweli alikumbana na uadui mkubwa lakini njia ya Bwana ilimtetea sana. Huyu mtumishi alikuwa mkuu, mwenye uwezo, mtii na aliyependwa na Mungu sana. Lakini cha ajabu ni kwamba hakupokelewa vizuri na watu. Tunaambiwa kwamba walimdharau, wakampiga, na kumtaka kabisa hata asiwasogelee. Lakini sasa huyu tumaini lake lilikuwa Mungu. Mungu alimpatia moyo wa gumegume, akawa haogopi, akakaza moyo kwa Mungu na hakika hakushindwa na matukano au mapigo ya maadui. Kwa uvumilivu wake na maisha yake bora aliweza kuwafikia wengi. Kwa kupigwa kwake wengi waliokolewa.


Huyu mtumishi ni Yesu. Yeye ndiye alikataliwa na watu wake; lakini Mungu alimpatia moyo mgumu ambapo basi aliweza kushindana na yale matukano yao. Aliishi kiaminifu na hili liliwafanya watesi wake wakose cha kumkamata nacho. Walijaribu kutunga makosa ya uongo ili kumshtaki wakaishia kushindwa.  


Leo Yesu mbele ya wanafunzi wake anajitangaza kwamba yeye ni Masiha na utume wake ni kama huu wa huyu mtumishi wa Mungu; yaani atawaokoa kwa njia ya mateso ulimwengu. Huku kwa wanafunzi wake kumkubali Yesu kama Masiha kulikuwa ni kwa muhimu kwani hadi sasa, ni mapepo tu yalikuwa yamemtambua na kumkiri kuwa Masiha hadharani. Sasa siku ya leo mitume kupitia mkuu wao yaani Petro wanamtangaza Yesu kama Masiha.


Anawaeleza kwamba yeye ni huyu mtumishi mwaminfu wa Mungu atakayeteswa na aliyetabiriwa na Isaya. Wanafunzi wake wanakataa kwa sababu kwao Masiha ni mtu aliyeko hodari; mwenye nguvu kama kina Hitler, sasa walitegemea awapindue Waroma ili wao wawe huru na hivyo asingalitegemewa afe kirahisi hivyo au kifo cha aibu. Hizi ndizo sababu za Petro kukataa unabii huu. Hapa Petro anaitwa shetani kwani shetani ni kiumbe kinachovuruga mpango wa Mungu. Na hivyo basi Petro kwa hapa anavaa sura ya shetani na ndio maana Yesu anamkemea kwa ukali kwani lipepo ni lazima likemewe, usicheze nalo. 


Kwenye haya masomo mawili twajifunza yafuatayo: 


kwanza Yesu anatualika kila mmoja kuwa mtumishi wa Bwana. Daudi alikuwa mmoja wao, nasi tuwe watumishi; lazima tuishi kiaminifu, tujitoe kwa ajili ya wengine na kuleta faraja kama huyu alivyofanya. Tusiwe watu wa kulalamikiwa au  kwamba tunafanya vibaya kila mahali, tusiwe kero, watu wachoke hata kutuona tu. Tusiwe hivyo kabisa. Tuwe watumishi wa Bwana.

Watumishi wa Bwana wanalindwa na uadilifu. Ukiwa mwadilifu utawashinda wengi. Watakuletea visa lakini utashinda. Lakini ukiwa na makandokando, kweli watakushinda tu. 

Makandokando yanakufanya ushindwe kumfikia mtu yoyote, hata ukitaka kuhubiri wanakukataa au unaogopa. Ondoa makandokando. 


Mtumishi wa Bwana lazima uwe na ule utayari wa kuubeba msalaba.  Sio unakimbiakimbia tu. 


Angalia Daudi, alikumbana na adui mkubwa na mkali kweli; mfalme Sauli anapambana na mchunga kondoo. Ni kama vile Raisi wa Marekani aje  apambane na mwenyekiti wa mtaa au wa kijiji. Wapi na wapi? Daudi alibeba msalaba huu na kumtumainia Mungu na kushinda. Usiwe wa kuogopa shida. Ni kama Mkristo anayeogopa uchawi au mtu unaogopa kulala usiku? Wee! Unakuwa mfano ili walioko nyuma waige. Unakuta kazee ati ndio kanaogopa ushirikina au kanabadilisha dini ili ati mtoto wake aolewe au hata binti anabadili dini. Usikubali.


Mtumishi yupo ili wengine wafaidi. Na hii ndio imani hai isiyomfu-anayoisemea Yakobo kwenye somo la pili. Ukimtembelea mtu usiende mikono mitupu na kumwambia Yesu atakuponya ee, toa jibuu na faraja. Haya maneno yanakwaza. Waambie watu waende hospitali hii au wamwone Docta huyu na si maneno maneno tu. 


Hata unaposali, onyesha upendo; kanisani sio kwa ajili ya kujiombea wewe mwenyewe tu, bali na wengine. Angalia mwenzako pembeni kapigika. Mwombee. Na kwenye kusali omba ili ukipata ukawasaidie wengine. Na hata siku hizi hata kama unaomba msaada au scholarship, ukiomba ili ukafaidi wewe huwa hawakupi, wanakuuliza, je, kwa nini unaomba-ili wengine wafaidi. Na Mungu ni hivi hivi. Omba ili wengine wafaidi kwa ajili yako wewe. Na hata leo, kwa chochote unachomwomba Mungu, omba ili wengine wafaidi na hakika Mungu atakuangalia.


Yesu ni Masiha wetu, ndiye mtumishi mwema, kila mmoja akawe Masiha na aanze kwa kuwa mtumishi mwema-achukue msalaba wake na kujitoa kwa ajili ya wenzake. Katika Mathayo 24:42 tendo la kulisha wenye njaa na kuvisha wasio na nguo ni la muhimu kuliko yote; linampatia mmoja tiketi ya kukaribishwa mbinguni. Sisi kama watumishi wema tuyatende haya matendo ya namna hii. Tuwe na siku ya matendo ya huruma kama shule, parokia, familia, kampuni, na tuwafundsihe watoto wetu hivyo. Yatima anayekaa kwako msaidie jamani. Nchi imejaa fadhili za Bwana. Tuwe watumsihi wa blBwana. Tuzitumie kwa ajili ya wengine. 


©️Pd. Prosper Kessy OFMCap.

No comments:

Post a Comment