*ASALI MUBASHARA-DOMINIKA YA 17 YA MWAKA B*
*TAFAKARI DOMINKA 17 MWAMA B*
*--Utanguli--*
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la misa takatifu. Leo basi katika neno la Bwana, tunakutana na ujumbe kwamba Mungu ndiye mwenye kuwalisha watu wake. Na zaburi yetu ya wimbo wa katikati inasisitizia kwa ukali kabisa kwa kusema kwamba Mungu aifunguapo mikono yake, sisi wanadamu tunapata chakula kwa wakati uliokusudiwa na kushiba kabisa kabisa. Hivyo, macho ya viumbe vyote yanamwelekea Bwana, -kama ya vitoto vya ndege yamwelekeavyo mama yao ajapo na chakula. Katika somo la kwanza na la injili tunakutana na matukio rasmi ambapo wanaomwelekea Bwana wanapata kushiba. Nasi basi ndugu zangu tumwelekee Bwana siku zote na tuishi kwa matumaini ya neno litokalo kinywani mwake. Huu ndio ujumbe mkuu ninaomba ili tuutafakari kwa pamoja.
----------*****-----------
Tukianza kwa kuziangalia nyimbo zetu, wimbo wetu wa katikati unatoka kwenye zaburi ya 144. Ni zaburi inayokiri wema na ukuu wa Bwana hasa kwenye kuwalisha na kuwashibisha watu wake. inakiri kwamba Mungu ndiye mgawaji wa mapaji yote. Na hivyo macho yote ya viumbe vyote vya ulimwengu humwelekea Bwana kwa ajili ya kupata mahitaji yao. Na kila vimwelekeapo, Bwana havipi nyoka au nge au mawe bali huvipatia chakula chao tena kwa wakati ufaao navyo hufurahi.
Zaburi hii imetungwa na mlawi mmoja baada ya kutafakari namna jinsi Mungu alivyowalisha wana wa Israeli jangwani; wakitafakari wanaona kwamba kule jangwani kama si Mungu alifungua mikono yake; hakika wangalikufa njaa. Huu ni mwaliko kwetu kwamba sisi hatuwezi kujilisha wenyewe; tunalishwa kwa tendo la Mungu kufungua mikono yake-basi tumtumainie Bwana na kumwomba chakula chetu cha kila siku. Na wale wenzetu; wale wanaotegemea kwetu kitu, wapate toka kwetu kinachostahili na chenye hadhi na si kupata ati mawe au kitu kingine kibaya. Huu ndio ujumbe mkuu tuupatao kwenye nyimbo zetu ndugu zangu.
Tukiingia kwenye masomo yetu ya leo, somo la kwanza ni kutoka katika kitabu cha kwanza cha wafalme. Hapa tunakutana na Nabii Elisha. Yeye anaishi na jumuiya kubwa ya wana wa kinabii ya watu kama mia hivi inayomtegemea yeye kama baba. Sasa kunatokea kipindi kirefu sana cha njaa na ile njaa inaiathiri hii jumuiya ya nabii Elisha. Sasa, anatokea mtu mmoja mchamungu anamletea Elisha msaada wa chakula kwa sababu yeye ni mtu wa Mungu lakini chakula anachomletea, ni kidogo kulinganisha na idadi na kile chakula kimeletwa kwa ajili ya Elisha tu. Sasa, Elisha anapoona hili, anamwambia mtumishi wake akigawe chakula kile kwa watu wote na si kwa ajili yake yeye tu.
Mtumishi wake anamwambia hakitoshi lakini yeye anamwamuru akigawe na kweli watu wanakula na kushiba tofauti na mawazo ya huyu mtumishi.
Kwenye injili ya leo, tunakutana na mwendelezo wa tukio lililokama hili la nabii Elisha. Yesu yupo basi na umati si wa mamia bali wa maelfu ya watu na hawa wanaumwa njaa kweli kweli. Umati ulikuwa mkubwa sana na Yesu anawaambia baadhi ya wanafunzi wake wajaribu kuulisha ule umati lakini wanasema haiwezekani.
Lakini anatokea kijana mmoja mdogo anasema mimi nina mikate mitano na samaki wawili; huu ndio mchango wangu kwenye kuwalisha hawa watu. Lakini baadhi ya wanafunzi wanasema tena kwamba hivi havitoshi. Yesu anasema hivi hivi vinatosha; anavichukua hivi vimikate na visamaki na kushukuru na kuwagawia watu na cha ajabu wale wanakula na kushiba na wakasaza.
Katika masomo haya mawili naomba tujifunze yafuatyo ndugu zangu:-
Kwanza:wanadamu tunamwelekea Bwana kwa chakula. Ndiye mwenye kumlisha mwanadamu hivyo anapaswa ategemewe yeye tu. Lazima basi tukiamka asubuhi tumwambie ee Mungu tulishe leo, nitakula nini? Hata kama una magunia ya mchele ishirinI huko ndani au una akiba ya pesa kiasi gani lazima kweli uwe mnyenyekevu kila unapoamka na kumwambia Mungu kwamba fungua mikono yako ee Bwana na leo naomba unilishe kwani hifadhi yako ya chakula ghalani ni bure, Mungu akifunga mkono wake, huwezi kula. Na jioni basi ni siku ya kumshukuru Mungu kwa kutulisha na kumwambia ee Mungu usiniache na endelea kunilisha leo, niwe na afya njema siku zote.
Pili: ndugu zangu tumesikia kwamba yule kijana alikuwa na vimikate vyake vitano na visamaki lakini alikuwa tayari kuvitoa vyote na kusema huu ndio mchango wangu kwa ajili ya hawa watu ili washibe. Nakuambia wengine kwenye ule umati wangetoa hivyo hivyo, kila mmoja angekuwa kama yule kijana na kutoa alichonacho, kweli wangeweza kumaliza lile jambo. Lakni cha ajabu tumesikia hata wale mitume wakisema kwamba haiwezekani kuwalisha hawa watu, hakuna uwezo na kwenye injili nyingine wanasema watawanye hawa watu warudi makwao wakajitafutie chakula wenyewe bila kujali kwamba wengine wangeweza kuzimia njiani. Haya ndiyo yanayotokea kwetu ndugu zangu.
Wengi wetu wanakufa njaa kwa sababu tumekosa watu wenye moyo ulionyooka kama huyu kijana. Wengi wetu hatuko tayari kuonyesha yote tuliyonayo; lazima tunaficha baadhi kama ilivyokuwa kwa akina Safira na Anania katika kitabu cha matendo ya mitume sura ya tano. Na kutokana na kuficha ficha huku na kutokuwa wawazi, wengi wetu wanakufa njaa kati ya walio na mali za kutosha. Mfano, hata mimi nilipokuwa ninakusanya mchango kwa ajili ya misa yangu ya shukrani, watu hawakuwa wazi. Unampa mtu kadi akusambazie, anapata pesa anakuletea nusu. Mwisho wa siku unauliza hiyo bajeti haitimii jamani? Hizo milioni 15 zinaokotwa kwa mwaka mzima hazitimii-lakini pengine ni ukosefu wa uwazi na ubinafsi pengine. Na hii ndiyo inayotumaliza. Hii dunia isingefaa iwe na njaa. Ni ubinfasi tu umekidhiri.
Hata pale kwenye umati wa Yesu, kama watu wangekuwa wawazi kama huyu mtoto, naamini idadi kubwa ya watu wangelishwa kwani naamini si huyu mtoto mmoja aliyekuwa na chakula; kipindi hicho hadi leo, watu walipokuwa wanakwenda safari ndefu walichukua chakula. Lakni cha ajabu ni huyu aliyejitokeza.
Na kwa sababu basi Yesu aliweza kuongeza mikate ikawa mingi, usishangae kukuta kwamba hata wale waliokuwa na chakula chao wasikitoe ndani ya ule umati waliishia kukitupa; yawezekana kwamba kile chakula alichokiongeza Yesu kilikuwa kitamu zaidi. Na hiki ndicho kinachotokea kwa wengi wetu. Unakuta unaficha chakula chako huko ndani lakini mwisho wa siku unakuta kinaozea huko. Unakuta kinatupiwa kuku na kingine kinaharibika vibaya kiasi kwamba hata kuku hawezi kukila.
Na hili nililiona kule kijijini-kuna akina bibi waliokuwa wanaficha chakula hadi kinaozea ndani na mwishowe unaona anakitupa kwa kujificha tena usiku lakini habari zao za kutupa chakula zinafahamika mara moja. Tuache tabia hizi ndugu zangu. Tushirikishane chakula, tuache kuficha.
Ukiona kama kuna mtu anafanya sherehe yake na katindikiwa, toa sehemu ya chakula msaidie.
Kingine tutambue kwamba njaa inauma jamani hivyo akikuomba mtu chakula hasa huku mjini, jamani usimuache hivi hivi. Mnunulie chakula na umsaidie. Ukimuona mtu anakuomba chakula na wewe humpatii chochote, tambua kwamba unakuwa mnyama hapa. Toa kitu umsadie-acheni kuwa wachoyo kupita kiasi.
Kingine tutambue kwamba kuna wengine wana uhitaji mkubwa wa chakula. Wengine husikia njaa kwa haraka na wanamahitaji maalumu. Tusiwanyanyase. Kuna wagonjwa wa kisukari, ambao kuendana na aina ya kisukari, wengine hupata njaa kwa haraka sana. Hivyo atakuwa anakula kila saa. Hivyo, mkimpata mtu kama huyu ndani ya familia yenu, jamani onyesheni kumjali, msimuone kama mtu mwenye tumbo na kumtangaza.
Mwangalieni kwa huruma, mueleweni kama mtu mwenye shida. Na wengine watahitaji chakula maalum, labda watachagua vyakula, tuwe wavumilivu, watu hawa wapo jamani. Tuwe na huruma Zaidi. Tusiwanyanyase hawa watu.
Kingine ni kuwa na Imani. hawa wanafunzi walikosa imani kirahisi sana. Waliona kwamba Yesu sawa anaweza kuponya, na anaweza kufufua watu-lakini kwenye kulisha chakula watu wengi hivi waliona shaka. Ndivyo ilivyo kwa baadhi yetu. Kuna baadhi ya mambo tunaona kwamba hapa Yesu anaweza lakini mengine tunao kana kwamba hawezi. Hivyo hatumtegemei kwa kila kitu na ndio maana tumeishia kushindwa kwenye mambo mengi. Tunaishia kuona kwamba kwa sehemu nyinigne, ushirikina unaweza kuliko ilivyo kwa Mungu.
Unakuta mtu anasema ugonjwa huu unatibiwa na mganga fulani tu. Ndio maana hata kwa baadhi yetu tumeishia kushika zile mila za asili na kufanya matambiko licha ya kwamba sisi ni wakristo bado. Unakuta mkristo akiambiwa labda mizimu inahitaji mbuzi hii au kuna mzimu fulani anaogopa, anaona hata akimtegemea Mungu hawezi kumwokoa hapa, anaishia kutimiza ya huyu mganga. Jamani, Mungu ategemewe kwa kila kitu. Jamani, Yesu aweza yote na hivyo yabidi ategemewe kwa kila kitu jamani. Tufanye hivyo jamani. Tuache kukosa imani.
Ekarisit ndiyo chakula chetu cha kiroho ambacho basi kila mmoja wetu anaalikwa-tajiri, maskini, fukara, mgonjwa wote. Ni Yesu anayejitoa bila kujibakiza. Nasi tuwe hivyo hivyo ndugu zangu. Hatuweki matabaka na kusema ati ni wale waliotoa sadaka kubwa kanisani ndio wanapata zaidi. Unapokelewa jinsi ulivyo na kubarikiwa ndugu zangu kwa neema za Kimungu. Na hii inawezekana kwa sababu Yesu alijitoa bila kujibakiza, nasi tujitoe hivyo hivyo. Sherehe zetu nyingi zinakuwa na mambo kama ya kadi na kuponi za aina fulani-wanasema aliyechangia mchango huu atakunywa bia kuanzia tano, waliochangia mchango wa chini, wanakunywa bia mbilimbili. Hii sio sahihi. Mwisho wa siku kwenye sherehe moja, unakuta wengine wanakula nyama na wengine wanakula makande, huyu bia sita, huyu mbili. Wasiochangia wanatupwa nje kabisa. Hii sio sahihi. Ekaristi iwe ndio kielelezo cha sherehe zetu jamani. Hili sio rahisi najua lakini tujitahidi kwani hata parokiani kunakuwaga na ubaguzi lakini tujue kwamba hili sio sahihi na sisi kama kanisa lazima kurekebisha kuondoa ubaguzi. Ekaristi iwe ndio msingi wetu na model wetu. Kwamba "twaeni mle wote" sio wachache ni wote.
Na kingine ni kwenye shererhe jamani: watoto huwa wanaachwaga wanaangalia tu, wanabakia wakitoa macho tu, jamani, mkipanga sherehe, wekeni na kabajeti kwa ajii ya wale watoto wanaoangalia, msiache jamani kufanya hivi.
Na tunapoambiwa tutoe kitu kwa ajili ya watu kama msaada, tutoe vitu vya kufaaa, tuache kutoa makapi. Yesu alitoa mikate na samaki safi. Na wewe hata kama unatoa nguo kwa msaada, toa nguo safi na usitoe nguo chafu au makapi. Wengine wanafikiri ati kwa kuwa ni msaada, wanaweza kutoa kila kitu. Nakumbuka kuna nchi fulani iliwatumia nchi ya kiafrika chakula cha mbwa. Japokuwa ulikuwa ni unga mzuri wenye virutubisho na ungeokoa watoto wengi wa afrika, kikishakuwa chakula cha mbwa jua kwamba huu ni unyanyasaji na si tena msaada. Toa chema kwani Yesu naye anatoa chema kwa ajilii yako.
Kwenye somo la pili mtume Paulo anatuambia kwamba tushirikiane kwenye kubebeana mizigo yetu kama Kristo anavyopenda. Basi tusiache kubebeana mizigo. Wapo wengi wanashida zao nyingi tu ndugu zangu, tubebeana hii mizigo. Wengi kati yetu wamekufa kwa njaa, kwa magonjwa, kwa sababu hatubebeani mizigo jamani. Tubebeane mizigo.
©️Pd. PROSPER KESSY OFMCap.
No comments:
Post a Comment