MASOMO YA MISA, JULAI 21,
2021
JUMATANO, JUMA LA 16 LA
MWAKA
SOMO 1
Kut. 16:1-5, 9-15
Walisafiri kutoka Elimu,
na mkutano wote wa wana wa Israeli wakafikilia bara ya Sini, iliyoko kati ya
Elimu na Sinai, siku ya kumi na tano ya mwezi wa pili baada ya kutoka kwao nchi
ya Misri. Na mkutano mzima wa wana wa Israeli ukawanung’unikia Musa na Haruni,
huko barani; wana wa Israeli wakawaambia, Laiti tungalikufa kwa mkono wa Bwana
katika nchi ya Misri, hapo tulipoketi karibu na zile sufuria za nyama,
tulipokula vyakula hata kushiba; kwani mmetutoa huko na kututia katika bara
hii, ili kutuua kwa njaa kusanyiko hili lote.
Ndipo Bwana akamwambia
Musa, Tazama, mimi nitawanyeshea ninyi mvua ya mkate kutoka mbinguni; na hao
watu watatoka nje na kuokota kila siku sehemu ya siku; ili nipate kuwajaribu,
kwamba watakwenda katika sheria yangu, ama sivyo. Kisha itakuwa siku ya sita,
ya kwamba watayaandaa hayo watakayoleta ndani, nayo yatakuwa ni mara mbili
kuliko wayaokotayo kila siku.
Musa akamwambia Haruni,
Haya, sema na mkutano wote wa wana wa Israeli. Njoni karibu mbele ya Bwana; kwa
kuwa yeye ameyasikia manung’uniko yetu. Ilikuwa Haruni aliponena na huo mkutano
wote wa wana wa Israeli, wakaangalia upande wa bara, na tazama, utukufu wa Bwna
ukaonekana katika hilo wingu. Bwana akasema na Musa, akinena, Nimeyasikia
manung’uniko ya wana wa Israeli; haya! Sema nao, ukinena, Wakati wa jioni
mtakula nyama, na wakati wa asubuhi mtashiba mkate; nanyi mtajua ya kuwa mimi
ndimi Bwana, Mungu wenu. Ikawa wakati wa jioni; kware wakakaribia,
wakakifunikiza kituo; na wakati wa asubuhi umande ulikuwa juu ya nchi pande
zote za kituo. Na ulipoinuka ule umande uliokuwa juu ya nchi, kumbe! Juu ya uso
wa bara kitu kidogo kilichoviringana, kidogo kama sakitu juu ya nchi.
Wana wa Israeli
walipokiona, wakaambiana, Nini hiki? Maana hawakujua ni kitu gani. Musa
akawaambia, Ndio mkate ambao Bwana amewapa ninyi, mle.
Neno la Bwana...
Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 78:18-19, 23-28 (K)
24
(K) Bwana aliwapa nafaka
ya mbinguni.
Wakamjaribu Mungu mioyoni
mwao
Kwa kutaka chakula kwa
tamaa zao.
Naam, walimwambia Mungu,
wakasema,
Je! Mungu aweza kuandika
meza jangwani? (K)
Lakini aliyaamuru mawingu
juu;
Akaifungua milango ya
mbinguni;
Akawanyeshea mana ili
wale;
Akawapa nafaka ya
mbinguni. (K)
Mwanadamu akala chakula
cha mashujaa;
Aliwapelekea chakula cha
kuwashibisha.
Aliuelekeza upepo wa
mashariki mbinguni;
Akaiongoza kusi kwa uweza
wake. (K)
Akawanyeshea nyama kama
mavumbi,
Na ndege wenye mbawa,
Kama mchanga wa bahari.
Akawaangusha kati ya
matuo yao,
Pande zote za maskani
zao. (K)
SHANGILIO
Aleluya, aleluya,
Mbegu ni neno la Mungu,
anayepanda ni Kristu, atakayemkuta, ataishi milele.
Aleluya.
INJILI
Mt. 13:1 – 9
Yesu alitoka nyumbani,
akaketi kando ya bahari. Wakamkusanyikia makutano mengi, hata akapanda
chomboni, akaketi; na ule mkutano wote wakasimama pwani.
Akawaambia mambo mengi
kwa mifano, akisema, Tazama, mpanzi alitoka kwenda kupanda. Hata alipokuwa
akipanda, mbegu nyingine zilianguka karibu na njia, ndege wakaja wakazila;
nyingine zikaanguka penye miamba, pasipokuwa na udongo mwingi; mara zikaota,
kwa udongo kukosa kina; na jua lilipozuka ziliungua; na kwa kuwa hazina mizizi
zikanyauka. Nyingine zikaanguka penye miiba; ile miiba ikamea, ikazisonga;
nyingine zikaanguka penye udongo mzuri, zikazaa, moja mia, moja sitini, moja
thelathini. Mwenye masikio na asikie.
Neno la Bwana... Sifa
kwako Ee Kristo.
Copyright © 2020,
"MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania. Readings reproduced by FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment