“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya kila siku
Alhamisi, Julai 1, 2021
Juma la 13 la Mwaka
Mwa 22: 1-19;
Zab 115: 1-9;
Mt 9: 1-8
UJASIRI WAKUTAFUTA
MSAMAHA
Ndugu zangu wapendwa,
karibuni kwa adhimisho la Misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika
somo la kwanza, tunakutana na simulizi kuhusu utayari wa Abrahamu kumtoa Mwanae
Isaka kama sadaka ya kuteketezwa. Hakika hili lilikuwa jaribu la ajabu kwani huyu
ni mtoto wa pekee, aliyesubiri miaka 25 kumpata, na ambaye alikuwa ameahidiwa
kwamba kwa njia yake uzao wake utaongezeka. Na pia Abrahamu alikuwa mzee
tayari. Lakini haoneshi ugumu katika kukubali kumtoa mwanae kama sadaka.
Tukio hili lilimbariki
kwa maisha yake yote. Likamfanya ndio uzao wake uongezeke na kuwa tukio la
kusimuliwa kwa vizazi vingi. Tunachojifunza hapa ni kwamba ukarimu, utayari wa
kutoa yote kwa ajili ya Mungu hakika ni ufunguo wa kupata yote. Mbele ya Mungu
hakuna cha kupoteza. Kila unachokitoa kwa ajili ya Bwana, utashangaa
hakitapotea-iwe ni muda wako, rasilimali zako. Tuondoe tabia yoyote ya kichoyo.
Abrahamu kadiri
alivyozidi kujitolea kwa ajili ya Bwana, ndivyo alivyozidi na yeye kubarikiwa.
Sisi tuwe tayari kuzifanya kazi ya Bwana. Tutoe rasilimali zetu kwa ajili ya
Bwana. Pia tutoe muda wetu kufanya kazi ya Bwana. Juu ya Mlima wa Bwana,
itapatikana neema, hivyo jitoe kwa ajili ya Bwana.
Mwenyezi Mungu alimzuia
Abrahamu kumtoa Mwanae kama sadaka lakini Mungu Mwenyewe alikuwa tayari kumtoa
Yesu Kristo Mwanae kama sadaka ya kuteketezwa. Tutambue kwamba Mungu
anapokuambia tutekeleze sadaka kubwa, hakika ni yeye anayekuja kuitimiza sadaka
ile. Yeye anakurudishia kama ilivyo –Yehova Yire. Juu ya mlima wa Bwana,
hupatikana. Usiogope kujitoa kwa ajili ya Bwana, juu ya mlima wake, hakika
atatoa.
Katika injili, tunakutana
na habari za kupona Mwenye kupooza. Huyu mwenye kupooza anasaidiwa na rafiki
zake, ndio wanaompeleka kwa Bwana. Imani ya walio karibu na mgonjwa inaleta
uponyaji kwa mgonjwa. Hapa twajifunza umuhimu wa kuuguzwa na watu wenye imani.
Watu wenye imani huleta uponyaji kwa wagonjwa. Lakini kuuguzwa na wasio na
imani, ni sababu za wagonjwa wengi kupotea.
Sisi tunaotunza wagonjwa
tujifunze kuwahudumia kiroho pia. Tuwapatie pia sakramenti za wagonjwa,
tuwapatie sakramenti ya upatanisho na Ekaristi. Hizi huwaponya kiroho na
kimwili. Tusiache kutumia sakramenti hizi.
------------------------
Copyright ©2013-2020
©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment