Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA JUNI 28, 2024

 


MASOMO YA MISA JUNI 28, 2024

IJUMAA YA 12 YA MWAKA

 


SOMO1

2 Fal 25: 1-12

 

Ikawa katika mwaka wa kenda wa kutawala kwake, katika mwezi wa kumi, na siku ya kumi ya mwezi huo, Nebukadreza, mfalme wa Babeli, akaja yeye na jeshi lake lote, kupigana na Yerusalemu, akapanga hema zake kuukabili; bao wakajenga ngome juu yake pande zote. Basi mji huo ulihusuriwa hata mwaka wa kumi na moja wa mfatae Sedekia. Siku ya kenda ya mwezi wa nne njaa ilikuwa nzito ndani ya mji, hata hapakuwa na chakula kwa watu wa nchi. Ndipo mahali pakabomolewa katika ukuta wa maji, watu wote wa vita wakakimbia usiku kwa njia ya lango lililokuwa kati ya zile kuta mbili, karibu na bustani ya mfalme; (basi wale Wakaldayo walikuwa wakiuzuia mji pande zote;) mfalme akaenda kwa njia ya Araba. Lakini jeshi la Wakaldayo wakamfuatia mfalme, wakampata katika nchi tambarare ya Yeriko; na jeshi lake lote walikuwa wametawanyika na kumwacha. Ndipo wakamkamata mfalme, wakamchukua kwa mfalme wa Babeli  huko Ribla. wakatoa hukumu juu yake. Wakawaua wana wa Sedekia mbele ya macho yake, wakampofusha macho Sedekia, wakamfunga kwa pingu, wakamchukua mpaka Babeli.

 

Hata mwezi wa tano, siku ya saba ya mwezi, ndio mwaka wa kumi na kenda wa mfalme Nebukadreza, mfalme wa Babeli. Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, mtumishi wa mfalme wa Babeli, akaingi Yerusalemu. Akaiteketeza nyumba ya Bwana, na nyumba ya mfalme; na nyumba zote za Yerusalemu, naam, kila nyumba kubwa aliiteketeza kwa moto. Na jeshi lote la Wakaldayo, waliokuwa pamoja na huyo amiri wa askari walinzi, wakazibomoa kuta za Yerusalemu pande zote. Na mabaki ya watu waliosalia katika mji, nao wale walioasi, na kumkimbilia mfalme wa Babeli, na mabaki ya watu wote wengine, watu hao Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, akawachukua mateka. Lakini huyo amiri wa askari walinizi akawaacha watu walio maskini ili wawe watunza mizabibu na wakulima.

 

 

WIMBO WA KATIKATI

Zab. 137 : 1-6 (K). 6

 

(K) Ulimi wangu ugandamane nisipokukumbuka.

 

Kando ya mito ya Babeli ndiko tulikoketi,

Tukalia tulipoikumbuka Sayuni.

Katika miti iliyo katikati yake

Tulivitundika vinubi vyetu. (K)

 

Maana huko waliotuchukua mateka

Walitaka tuwaimbie;

Na waliotuonea walitaka furaha;

Tuimbieni baadhi ya nyimbo za Sayuni. (K)

 

Tuuimbeje wimbo wa Bwana

Katika nchi ya ugeni?

Ee Ycrusalemu, nikikusahau wewe,

Mkono wangu wa kuume na usahau. (K)

 

Ulimi wangu na ugandamane

Na kaakaa la kinywa changu, nisipokukumbuka.

Nisipoikuza Yerusalemu

Zaidi ya furaha yangu iliyo kuu. (K)

 

 

SHANGILIO

Yn. 10:27

 

Aleluya, aleluya, Kondoo wangu waisikia sauti yangu, nami nawajua, nao wanifuata. Aleluya.

 

 


INJILI

Mt. 8:1-4


Yesu aliposhuka mlimani, makutano mengi walimfuata. Na tazama, akaja mtu mwenye ukoma akamsujudia, akisema, Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa. Yesu akanyosha mkono, akamgusa, akisema, Nataka; takasika. Na mara ukoma wake ukatakasika. Yesu akamwambia, Angalia usimwambie mtu; ila enenda zako, ukajionyeshe kwa kuhani, ukaitoe sadaka kama alivyoamuru Musa, iwe ushuhuda kwao.


-------------------------


Copyright © 2024, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment