MASOMO YA MISA, MEI 31, 2024
IJUMAA, JUMA LA 8 LA PASAKA
IJUMAA, JUMA LA 8 LA PASAKA
SIKUKUU YA BIKIRA MARIA KWENDA KUMWAMKIA ELIZABETI
SOMO 1
Sef. 3:14-18
Imba, Ee binti Sayuni; piga kelele, Ee Israeli; furahi na kushangilia kwa moyo wako wote, Ee binti Yerusalemu. Bwana ameziondoa hukumu zako, amemtupa nje adui yako; mfalme wa Israeli, naam, yeye Bwana, yu katikati yako; hutaogopa uovu tena. Katika siku ile Yerusalemu utaambiwa, usiogope, Ee Sayuni; mikono yako shujaa awezaye kuokoa; atakushangilia kwa furaha kuu, atatulia katika upendo wake. Atakufurahia kwa kuimba.
Au:
Rum. 12:9-16
Pendo na lisiwe na unafiki; lichukieni lililo ovu, mkiambatana na lililo jema. Kwa pendo la udugu, mpendane ninyi kwa ninyi; kwa heshima mkiwatanguliza wenzenu; kwa bidii, si walegevu; mkiwa na juhudi katika roho zenu; mkimtumikia Bwana; kwa tumaini, mkifurahi; katika dhiki, mkisubiri; katika kusali, mkidumu; kwa mahitaji ya watakatifu, mkifuata ukarimu; katika kukaribisha wageni, mkijitahidi.
Wabarikini wanaowaudhi; barikini, wala msilaani. Furahini pamoja nao wafurahio; lieni pamoja nao waliao. Mpatane nia zenu ninyi kwa ninyi. Msinie yaliyo makuu, lakini mkubali kushughulishwa na mambo manyonge.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Isa. 12:2-6 (K) 6
(K) Mtakatifu wa Israeli ni mkuu kati yako.
Tazama, Mungu ndiye wokovu wangu;
Nitatumaini wala sitaogopa;
Maana Bwana Yehova ni nguvu zangu na wimbo wangu;
Naye amekuwa wokovu wangu.
Basi, kwa furaha mtateka maji katika visima vya wokovu. (K)
Mshukuruni Bwana, liitieni jina lake;
Yatangazeni matendo yake kati ya mataifa,
Litajeni jina lake kuwa limetukuka. (K)
Mwimbieni Bwana; kwa kuwa ametenda makuu;
Na yajulikane haya katika dunia yote.
Paza sauti, piga kelele, mwenyeji wa Sayuni;
Maana Mtakatifu wa Israeli ni mkuu kati yako. (K)
SHANGILIO
Lk. 1:45
Aleluya, aleluya,
Heri Bikira Maria aliyesadiki ya kuwa aliyoambiwa na Bwana yatatimizwa.
Aleluya.
INJILI
Lk. 1:39-56
Mariamu aliondoka siku hizo, akaenda hata nchi ya milimani kwa haraka mpka mji mmoja wa Yuda, akaingia nyumbani kwa Zakaria akamwamkia Elisabeti. Ikawa Elisabeti aliposikia kule kuamkia kwake Mariamu, kitoto kichanga kikaruka ndani ya tumbo lake; Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu; akapaza sauti kwa nguvu akasema, Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu anijilie mimi? Maana sauti ya kuamkia kwako ilipoingia masikioni mwangu, kitoto kichanga kikaruka kwa shangwe ndani ya tumbo langu. Naye heri aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana.
Mariamu akasema, Moyo wangu wamwadhimisha Bwana, Na roho yangu imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu; Kwa kuwa ameutazama unyonge wa mjakazi wake. Kwa maana, tazama, tokea sasa vizazi vyote wataniita mbarikiwa. Kwa kuwa Mwenye nguvu amenitendea makuu, na jina lake ni takatifu. Na rehema zake hudumu vizazi hata vizazi, kwa hao wanaomcha. Wenye njaa amewashibisha mema, Na wenye mali amewaondoa mikono mitupu. Amemsaidia Israeli, mtumishi wake; Ili kukumbuka rehema zake. Kama alivyowaambia baba zetu Ibrahimu na uzao wake hata milele. Mariamu akakaa naye kadiri ya miezi mitatu, kisha akarudi kwenda nyumbani kwake.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 2024, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment