MASOMO YA MISA, MEI 22,
2021
JUMAMOSI YA 7 YA PASAKA
SOMO 1
Mdo. 28 :16-20, 30-31
Tulipoingia Rumi Paulo
alipewa ruhusa kukaa kwake mwenyewe pamoja na askari aliyemlinda.
Ikawa baada ya siku tatu
akawaita wakuu wa Wayahudi wakutane; hata walipokutanika akawaambia, Ndugu
zangu, ingawa sikufanya neno kinyume cha watu wetu wala neno lililopingamana na
desturi za baba zetu, nalitiwa katika mikono ya Warumi, hali nimefungwa, tokea
Yerusalemu. Na hao walipokwisha kuniuliza-uliza walitaka kunifungua, kwa maana
hapakuwa na sababu yo yote kwangu ya kuuawa. Lakini Wayahudi walipotoa hoja juu
ya shauri hili nalishurutishwa kutaka rufani kwa Kaisari. Si kwamba nalikuwa na
neno la kuwashitaki watu wa taifa langu. Basi kwa ajili ya hayo, nimewaita mje
kunitazama na kusema nami; kwa maana nimefungwa kwa mnyororo huu kwa ajili ya
tumaini la Israeli.
Akakaa muda wa miaka
miwlli mizima katika nyumba yake aliyokuwa ameipanga, akawakaribi sha watu wote
waliokuwa wakimwendea, akihubiri habari za ufalme wa Mungu, na kuyafundisha
mambo ya Bwana Yesu Kristo, kwa ujasiri mwingi, asikatazwe na mtu.
Neno la Bwana...
Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 11 :4-5, 7 (K) 7
(K) Wanyofu wa moyo
wauona uso wake, Ee Bwana. au: Aleluya.
Bwana yu katika hekalu
lake takatifu.
Bwana ambaye kiti chake
kiko mbinguni,
Macho yake yanaangalia;
Kope zake zinawajaribu
wanadamu. (K)
Bwana humjaribu mwenye
haki;
Bali nafsi yake humchukia
asiye haki,
Na mwenye kupenda udhalimu.
(K)
Kwa kuwa Bwana ndiye
mwenye haki,
Apenda matendo ya haki,
Wanyofu wa moyo watamwona
uso wake. (K)
SHANGILIO
Mt. 28 :19-20
Aleluya, aleluya,
Enendeni, mkawafanye
mataifa yote kuwa wanafunzi. Mimi nipo pamoja nanyi sikuzote, Hata ukamilifu wa
dahari.
Aleluya.
INJILI
Yn. 21:20-25
Petro aligeuka akamwona
yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu anafuata; (ndiye huyo aliyeegama kifuani
pake wakati wa kula chakula cha jioni, akasema, Bwana, ni nani akusalitiye?).
Basi Petro akamwona huyo, akamwambia Yesu, Bwana, na huyu je? Yesu akamwambia,
Ikiwa nataka huyu akae hata nijapo, imekupasaje wewe? Wewe unifuate mimi.
Basi neno hilo lilienea
katikati ya ndugu ya kwamba mwanafunzi yule hafi. Walakini Yesu hakumwambia ya
kwamba hafi; bali, Ikiwa nataka huyu akae hata nijapo, imekupasaje wewe? Huyu
ndiye yule mwanafunzi ayashuhudiaye haya, na aliyeyaandika haya; nasi twajua ya
kuwa ushuhuda wake ni kweli. Kuna na mambo mengine mengi aliyoyafanya Yesu;
ambayo yakiandikwa moja moja, nadhani hata ulimwengu usingetosha kwa vile
vitabu vitakavyoandikwa.
Neno la Bwana... Sifa
kwako Ee Kristo.
-------------------------
Copyright © 2020,
"MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment