Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

ASALI MUBASHARA-TAFAKARI YA SHEREHE YA PENTEKOSTE-23/05/2021*

 *ASALI MUBASHARA-TAFAKARI YA SHEREHE YA PENTEKOSTE-23/05/2021*



Utangulizi: Sherehe ya Pentecoste inachimbuko lake kutoka kwa Wayahudi walioamriwa waiadhimishe katika kitabu cha Walawi 23:9-22. Iliadhimishwa siku ya hamsini baada ya pasaka ya Kiyahudi. Kwa Wayahudi, Pentecoste ni ukumbusho wa ile siku Mungu alipompatia Musa Torati mlimani Sinai, Torati iliyopaswa kuwatakasa na kuwaongoza kuwa taifa teule la Mungu. Roho Mtakatifu alilishukia kanisa siku ya Sikukuu ya Pentecoste ya Kiyahudi na kuliunda taifa jipya la Mungu lenye watu kutoka katika kila kabila, lugha na rangi likiunganishwa na Imani moja katika Kristo. Kwetu sisi Wakristo, katika sherehe hii, tunaadhimisha namna Roho Mtakatifu alivyolishukia kundi dogo la Wakristo ambalo lilikuja kuwa ndio chembe ya upandikizaji na ueneaji wa Kanisa; taifa takatifu la Mungu. Kwa njia ya Roho Mtakatifu, liliweza kuanza kama chembe ya haradali iliyoweza kutoa matawi na kuwavuta watu kutoka kila taifa, lugha na jamaa. Hii ndio maada kuu na ninaomba tusafiri katika kuitafakari kwa pamoja.


Tukianza kwa kuuangalia wimbo wa mwanzo unatoka katika kitabu cha Hekima ya Sulemani “roho wa Bwana ameujaza ulimwengu nayo ndiyo inayoviunganisha viumbe vyote, hujua maana ya kila sauti. Ni maneno ya hekima toka katika kitabu cha hekima ya Sulemani. Anaandika maneno haya baada ya kufanya tafakari nzima ya jinsi vitu vinavyokaa ndani ya huu ulimwengu na yeye anatambua kwamba ni Roho wa Bwana tu ndiye awezeshaye hivi kuishi. Roho huyu ndiye atoaye uhai kwa kila kitu, hata mimea, wadudu tunaowaona kumbe wanaishi kwa njia ya roho huyu na zaburi yetu ya wimbo wa katikati inatuambia kwamba roho akiondoa mkono wake juu ya hivi viumbe, basi vinacollapse na kurudia mavumbini walimotoka. Hivi huyu mwandishi wa kitabu hiki ingawa kwa kipindi hiki alikuwa hajaelewa maana ya Roho mtakatifu kama nafsi, lakini aliweza kuiona Roho wa Bwana kama nguvu iwezeshayo viumbe vyote kuishi, kusonga mbele, kuvipatia uhai. 


Halafu mwandishi pia anasema kwamba roho ndiye atoaye uwezo wote wa kutufanya tuelewane-kwa mfano kitendo cha kuja kwako na kuweza tu kuongea na kunielewa yeye anaona kwamba ni roho aliyeko kwako na ndani yangu pia aliyewezesha haya maelewanao. Sisi katika sherehe yetu ya pentecoste tunayatumia maneno haya kama sehemu ya kutambua kwamba Roho Mtakatifu kwa ile siku ya pentecoste amekuja ulimwenguni lengo likiwa ni kutuunganisha watu wa kabila zote ili tuweze kuongea lugha moja kama wafuasi wa kristo. Na kwa kufanya hivi basi ataweza kufanya jumuiya moja, taifa moja takatifu, lenye msikilizano-kwa kitendo hiki twaweza kusema kweli ya kwamba Roho wa Bwana ameujaza ulimwengu.


Katika wimbo wa katikati, zaburi yake inatoka katika zaburi ya 104. Maneno yanasema waipeleka roho yako na kuufanya upya uso wa nchi. Ni zaburi inayosifu ukuu wa Mungu na jinsi alivyouumba ulimwengu katika hekima kubwa. Mlawi aliyeimba zaburi hii anausifu ukuu wa Mungu, jinsi alivyouumba ulimwengu na jinsi kila kiumbe kinavyoweza kuishi kutokana na uwepo wa nguvu ya Mungu duniani. Hakika ukiiondoa Roho wa Bwana ulimwenguni, kila kitu kinaoza, hakuna tena uhai. Hivyo kumbe viumbe vinaishi kwa sababu Bwana yupo, kwa sababu ya pumzi ya Bwana. Sisi tunaitumia zaburi hii leo kuonyesha kwamba roho ndiye mwenye kuliletea kanisa na ulmwengu wote uhai. Hivyo asitokee mtu yoyote afikiri kanisa ni lake, ni mali ya roho, ebu lifanye liwe lako tuone kama utafika popote. Hizi ndizo nyimbo zetu.


Na tukiingia katika masomo yetu ya leo na tukianza kwa kuiangalia Injili yetu ya leo, tunamkuta Yesu akiongea na kundi dogo la watu kumi na moja jioni ya siku ile ya ufufuko wake. Kundi hili lipo katika hofu, utupu, na masikitiko na ukataji wa tamaa:Yesu anatokea mbele yao na kulipatia amani. Anawavuvia Roho Mtakatifu kama ishara ya kuwapa uhai mpya na analipatia madaraka ya kusamehe dhambi. Aliendelea kujitokeza kwa kundi hili na kabla ya kupaa kwake aliliamuru lisitoke Yerusalemu bali limsubiri Roho Mtakatifu. 


Katika somo la kwanza tunagundua kwamba idadi ya watu ndani ya hili kundi imeshaongezeka na idadi yao kufikia karibu watu 120 (Mdo 1:15). Hawa walikuwa wakidumu katika sala lakini bado walikuwa katika hofu ya wayahudi. Lakini ilipotimia siku ya Pentecoste, Roho Mtakatifu anawatokea, gafla wanapata nguvu, woga wote unakwisha, wanafungua milango, na kutoka nje kumhubiri Kristo bila hofu.


Wanapata pia kipaji cha kuongea lugha ngeni. Kwa kuwa siku hiyo ilikuwa pia Pentecoste ya Kiyahudi, wayahudi walitoka sehemu mbalimbali kuja Yerusalem kwa sherehe hii. Hawa walijua lugha mbalimbali za mataifa mengi na walivyowasikia wakiongea lugha hizo walishangaa-wakasema hawa watu wasiokuwa na elimu au kisomo wamepata wapi yote haya? Wamejifunza wapi lugha hizi? Wakabaki katika ushangao mkubwa. 


Katika Mdo 2:41, tunaelezwa kwamba mitume walipata nguvu za ajabu za kumtangaza Kristo na kwa mahubiri ya ile siku ya Pentecoste, hili kundi lilipata idadi ya wanachama wapya elfu tatu waliobatizwa. Kwa kuwa hawa ni Wayahudi waliokuwa wanaishi sehemu mbalimbali za ulimwengu, wao waligeuka kuwa chachu ya kuupeleka Ukristo kwenye mataifa waliyokuwa wanakaa; kama Roma, Alexandria na Afrika ya Kaskazini. Hawa walikuwa wa kwanza kuifikisha injili kwenye makanisa haya hata kabla ya mitume. Hivyo, katika siku hii moja tu, kanisa lilipatwa kutambulishwa kwa watu wa mataifa. 


Roho alileta mabadiliko kwa wale mitume. Mitume tuliowazoea sio wale baada ya Pentecoste. Waliondoa woga wote na kutiwa nguvu za ajabu. Mtazamo wao juu ya Yesu na mateso ulibadilika. Waliondoa maslahi yao mbele na kuyaweka ya kanisa; walikuwa tayari hata kuchapwa viboko kwa ajili ya Kristo na karibu wote waliishia kifo dini. Hapa ilikuwa ndio mwanzo tu wa Roho kuliongoza kanisa. 


Mdo 2:43-47 inatueleza kwamba kwa kuwa Roho alikuwa ndani ya kanisa, maisha ya kanisa yalikuwa na utamu wa ajabu. Kila mmoja aliiona ile jamii ya kikirsto kama rafiki: mfumo wao wa maisha ulivutia wengi. Tukumbuke kwamba kabla ya hapa kulikuwa na dini ya Kiyahudi iliyopokea watu wa taifa moja tu. Zaidi dunia ilikuwa ikiongozwa na mawazo na Philosophia mbalimbali kama za akina Plato, Aristotle, Wastoiki na Waepucurians. Hizi zilikuwa na wafuasi. Philosophia za Plato na Aristotle ziliwagawanya watu katika matabaka. Kulikuwa na tabaka la kutawala na la kutawaliwa; watoto toka katika matabaka haya mawili hawakuruhusiwa kuchangamana; na kazi ya kiongozi ilikuwa ni kuhakikisha kwamba kila mtu anabakia kwenye sehemu yake. Kutokana na hizi philosophia, baadhi ya watu waliteseka sana. Mfano, maskini na vilema walikataliwa kabisa. Mfano Waepukureans walionya kuanzisha uhusiano na watu maskini. Pia Philosophia hizi ziliamini kwamba wanadamu ni Wagiriki tu. 


Lakini jamii ya wale wakristo wa mwanzo ilimpokea kila mtu, watumwa, viwete na maskini wote. Hivyo jamii ya Wakristo ilivutia idadi kubwa ya watu. Wayahudi na watawala wa Kirumi walianza kuwaonea wivu, wakaleta madhulumu mengi, wakawaua mitume karibu wote. Kaisari Nero, Domitian na Diocletio waliwatesa na kuwauwa Wakristo wengi sana lakini hawakulishida kanisa. Miaka iliyofuata ukristo ukaja ukafanywa kuwa dini ya taifa lote. Ukristo ndivyo ulivyozidi kupata nguvu na baadaye chini ya uongozi wa Kaisari Constantino, Ukristo ulikuja kutawala katika Dola yote ya Kirumi. Roho alizidi kuliongoza kanisa na hata pale viongozi wa kanisa walipojiingiza katika mambo ya dunia Zaidi kuliko ya Mungu, Roho alizidi kuja na kuwaongoza katika mstari sahihi.


Katika kanisa, Roho Mtakatifu amekuwa mwalimu na kiongozi mkuu. Hili twaweza kulitafakari kwa namna mbili: kwanza: kila mara amekuwa akilijalia kanisa majibu ya kukabiliana na uzushi mbalimbali. Kwa mfano fundisho la kanuni ya Imani lilitolewa na kanisa kukabiliana na waliopinga umungu wa nafsi tatu za Utatu Mtakatifu. Fundisho hili ni kazi ya Roho Mtakatifu kwani limeweza kudumu karibu miaka elfu mbili bila kupoteza umuhimu wake au kuhitaji marekebisho. Kweli hii yote ni kazi ya Roho mtakatifu. Majibu yaliyotolewa katika mitaguso mbalimbali hushuhudia uwepo na uongozi wa Roho mtakatifu katika kanisa.


Pili: Roho Mtakatifu amekuwa akilisaidia kanisa na viongozi wake kupita katika changamoto mbalimbali. Kwa mfano, uzushi wa Arius uliokataa umungu wa Yesu, mapinduzi ya Martin Luther na mapinduzi ya Ufaransa ni miongoni mwa nyakati zilizolipatia kanisa changamoto kubwa sana. Mfano, mawazo ya mapinduzi ya Ufaransa yalipinga umuhimu wa Papa na kutaka kulifanya kanisa kuwa chini ya serekali. Watawa walifukuzwa kwenye nyumba zao. Baadhi hawakutaka kusikia juu ya kitu kinachoitwa kanisa. Kilikuwa ni kipindi cha changamoto kubwa. Lakini tukitafakari hekima waliyoitumia mapapa kuliongoza kanisa kwa kipindi hiki na majibu yaliyotolewa na kanisa kukabiliana na changamoto hizi hakika yanadhihirisha uwepo wa Roho anayeliongoza kanisa. 


Sisi tukizitafakari habari hizi, hakika zinatutia moyo na tunakuwa na kila sababu ya kumshukuru Roho Mtakatifu na kumuomba aendelee kuliongoza Kanisa letu na kutujalia neema zake kama alivyokwishafanya.

Leo basi tumwombe apambane na hali ya uregevu ndani ya kanisa letu. Watu jamani hawajagi kanisani, mtu anakuja siku tatu tu katika mwaka, ijumaa kuu, Christmas na pasaka. Tuache tabia hizi. Watu unakuta wapo wanauza chips hadi jumapili unafikiri hata wana ela basi? Shida tu. wanakazana wee lakini wapi!


Atufanye tuelewe kwamba sisi ni askari wa Kristo na kama askari tukubali kuwa mstari wa mbele. Tusiwe wategeaji na kushinda vita liwe lengo letu. Kama ni baba uwe mstari wa mbele, kama ni mama uwe mstari wa mbele, ukija kanisani uwe mstari wa mbele-unakuta mtu anakuja kanisani akiambiwa ati abebe hata vipaji anakataa, anajiona ni wa kiwango cha juu mnoo , kanisani sio sehemu ya kujionyesha, usifikiri hawa wanaobeba vipaji ni vimbelembele, au sio wastaarabu, au baadhi ya watu wanaokaa nyuma weee wanajiona kuwa wastaarabu wee, wee, jamani kuweni mstari wa mbele, acheni kujivuna tena ndani ya kanisa-au waliomakatekista wanaonekana kama wanaopoteza muda au wanaoimba wanaonekana kama wanakimbelembele. 


Lakini pia hata sisi tunaokuja  mbele jamani tuwe na tabia nzuri, tusiwe viruka njia jamani, au watu tusiokuwa serious, kama unakuja mbele na maisha yako yawe mazuri, uwatie watu moyo, sio tena uwe kikwazo hata watu wakikuona waogope kuja kufanya kazi za kanisa, hivyo lazima maisha yetu yawe mfano na tupende kuungama.


Tuepuke uchoyo wa kuvigawa vipaji na karama zetu kama Paulo anavyosisitiza katika somo la pili. Tukubali kutumika kwa ajili ya wengine, kila mmoja atoe mchango wake kulijenga kanisa na waamini wake. Kama ni kusaidia uwe mstari wa mbele, kama unatoa msaada toa wote sio unaficha mwingine mfukoni halafu mwingine unatoa kile kidogo kama yule "Tola" wa stori za darasa la kwanza aliyekuwa anafichaga chakula-anawadanganya watoto wake mchana kwamba hamna chakula halafu usiku anaanza kula. Unafikiri utaweza kufanikiwa? Utakula konokono kama Tola alivyokula wewe. Usiwe kama mama afichaye samaki aonapo mgeni anajidai ati anakula mboga za majani kumbe kaficha ili akale mwenyewe. 


Tuache unafiki kwenye kutoa vipaji vyetu.

Katika wimbo wa katikati tumeona kwamba roho ndiye aliyeujaza ulimwengu wote na akiondoa pumzi yake vyote vinakwenda. Hivyo jamani, tutambue hili, hata tutembeapo, tembea kama mtu anayetambua hili. Unakuta kuna watu wanatembea kwa maringo wee kana kwamba hawajui kwamba Bwana akiondoa pumzi yake unarudi mavumbini alimotoka. 

Hivyo jua ya kwamba uhai ni wake na heshimu uhai wa mwenzako pia. Hili ni la muhimu sana. 


Roho pia atuepushe pia na ile hali ya kuvichukia viumbe vya Mungu. Unakuta mtu anakuangalia jinsi ulivyoumbwa anakuchukia. Hii sio vizuri. Hapa unakosoa kiumbe cha Mungu.

Tupende kuishi wamoja, tusitengane tengane jamani. Roho amekuja kuleta umoja kwa watu wa rangi, kabila na mataifa yote. Lazima tuwe tayari kujisikia nyumabani na watu wa kabila zote. Roho mtakatifu amekwisha tuunganisha. Hivyo lazima tuwe wamoja na tuonyeshe hili kwa matendo. Kutengana kwa sababu ya maeneo tutokayo au makabila hakika tutakuwa tunaendana kinyume na muungano uletwao na pentecoste yetu. 


Atufundishe pia mwanga wa kuweza kusema ukweli bila kupindisha. Watu siku hizi watakuambia "you are a great man, you are so good," kumbe ni kupambapamba tu. Tuombe Mungu atupe ujasiri wa kuwaambia watu ukweli.


Atuepushe na kutafuta faraja katika vitu kama pombe, vyakula, wanawake, sigara, tujue namna ya kuthibiti vionjo vyetu.

 

Atupe pia ufundi wa kutatua mambo vyema. Tujue ni maneno yapi ya kuongea na ni wakati gani.


Hitimisho: Tumshukuru Mungu aliyeliletea kanisa Roho Mtakatifu. Tumwombe atufanye tuishi kwa amani na kila mmoja wetu. Tumsifu Yesu Kristo.



No comments:

Post a Comment