ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya Pasaka
Jumamosi, Aprili
24, 2021
Juma la 3 la Pasaka
Mdo 9: 31-42;
Zab 116: 12-17;
Yn 6: 60-69.
UNA MANENO YA UZIMA WA MILELE!
Karibuni
ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Bado tunaendelea
kufurahia furaha tulizoletewa na sikukuu yetu ya Pasaka na neno la Bwana leo
katika injili Yesu anaendelea kufundisha juu ya yeye kama mwili ambao utabidi
uliwe na yeyote atakayeula hakika atapatiwa uzima wa milele. Fundisho hili
linakuwa gumu kupokelewa hata na baadhi ya wanafunzi wake na Yesu anapoona
kwamba hata wanafunzi wake wanapatwa na kigugumizi katika kulipokea hili, yeye
mwenyewe anashtuka. Alitegemea kwamba wale wanafunzi ndio wawe mstari wa mwanzo
katika kumsaidia lieleweke. Lakini cha ajabu ni kwamba wao wanajiunga tena na
lile kundi la wale Wayahudi, wale waliokataa kulipokea fundisho hili. Ndugu
zangu, wanafunzi wa Yesu hawakuwa na sababu ya kukataa kulielewa fundisho hili.
Wao wangalipaswa kulipokea, wao wangetakiwa mpaka sasa wawe wamekwisha mwelewa
Yesu kwamba huwa hadanganyi na kila asemacho ni ukweli. Kitendo cha kukataa
kulipokea fundisho ni dhahiri kwamba walikuwa bado hawajamwelewa vizuri na
hivyo walikuwa bado wanamtilia yYsu shaka. Hivyo, wao wangalipaswa kulipokea
neno hili ili watu wengine wapate moyo kulielewa. Yesu aliwategemea sana
wafanye hili.
Nasi
ndugu zangu inatupasa kutambua kwamba Yesu naye anatutegemea sana. Anategemea
sisi tumuamini na kuamini mafundisho yake ili yaweze kuwafikia wengine
kirahisi. Usipoamini wewe, ambaye ni Mkristo, wewe ambaye Yesu anakutegemea,
mimi padre ambaye Yesu ananitegemea, mimi mzazi ambaye watoto wananitazama, je,
wengine wataamini vipi? Yesu anatutegemea, tusimwangushe. Tutambue kwamba
kutokuamini kwetu, kukufuru mambo matakatifu na kulisema kanisa vibaya
kunawakwaza wengi wasimwamini Yesu. Hivyo jamani tumtetee huyu Yesu wetu,
anatutegemea, tusimwangushe. Kama wewe utamwangusha, je, wengine wataamini
vipi? Wewe ambaye umeishi na Yesu sasa na una miaka mingi sasa katika imani,
oneshe kwa matendo kwamba sasa unamuelewa Yesu, kwani Yesu anakutegemea
usijiunge nawasio lipenda kanisa na kuanza kulishambulia, linda imani yako.
Katika somo la kwanza, tunaikuta imani ya Kristo
mfufuka ikiendelea kupelekwa na kuhubiriwa mbali Zaidi na Zaidi. Jana Yesu
mfufuka alimgeuza mtesi wa kanisa kuwa mtume wake (Paulo). Leo nguvu ya Yesu
inatenda muujiza wa kumfufua mtu kutoka wafu. Lengo ni kutufanya tuiamini
habari njema ya Kristo mfufuka iliyofika kwetu na kwa kuamini kwetu tupate
uzima. Nasi kwa siku ya leo tumwombe Kristo asituache, apite kwetu, atutendee
na sisi muujiza na atuletee amani kama alivyoleta Amani kwa familia hii ya
Dorcas iliyokuwa katika maombolezo makali. Atufufue kutoka katika dhambi zetu
zinazo tufanya tuwe wafu wa kiroho. Fikiria juu ya dhambi inayokutesa kila
wakati na unairudiarudia daima, pengine ni majivuno, kukosa unyenyekevu,
kupenda sifa kupita kiasi na kuzitafuta huku ukiwaonea wadogo, kupamba watu kwa
maneno ya uongo badala ya kuwaambia Ukweli? n.k. Mwewe akitaka kumuua nyoka
humbeba juu kwani anajua lazima abadilishe uwanja Wa mapambano kwani akiwa
chini anajua hatamweza nyoka, hata sisi lazima tubadilishe mazingira ambayo
tunajua shetani anatukamata kirahisi- badilisha uwanja wa mapambano- kama wewe
unajijua una shida ya ulevi na unataka kuacha kwanini ukakae baa? Yapo
mazingira/watu wanautufanya tutende dhambi lazima tubadili uwanja wa mapambano
kwa nguvu ya Yesu mfufuka, tuwe viumbe vipya. Tumsifu Yesu Kristo
Copyright ©2013-2020 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki:
see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment