Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MAISHA YETU YANATOKA KWA KRISTO

 

ASALI ITOKAYO MWAMBANI”

Tafakari ya Pasaka

Ijumaa, Aprili 23, 2021

Juma la 3 la Pasaka

Mdo 9:1-20;

Zab 117:1-2 (K. Mk 16:15);

Yn 6:52-59.

MAISHA YETU YANATOKA KWA KRISTO!

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Bado tunaendelea kufurahia furaha tulizoletewa na sikukuu ya Pasaka kwa ufufuko wa Kristo Bwana wetu.

Na leo neno la Bwana katika injili yetu ya leo linaendelea kutufundisha juu ya Yesu kama mkate ulioshuka kutoka mbinguni ambao kila mmoja wetu anapaswa kwenda kwake kuula ili uweze kumpatia uzima, uweze kumsaidia apate kusafiri moja kwa moja hadi kwenye ile nchi ya ahadi, yaani mbinguni. Yeyote atakayeukosa mkate huu-hakika hatakaa aweze kufikia ile nchi ya ahadi.

Ndugu zangu, ukweli ni kwamba Yesu aliamua kujishusha na kukubali kukaa katika mkate wa Ekaristi. Hii ni namna ya kiunyenyekevu sana na ni namna aliyoamua mwenyewe na lengo ni kutufikia sisi. Na huu ni ukweli: jinsi Ekaristi ilivyo, ipo kwa namna ambayo inaweza kumfikia kila mtu, mkate unaotumika unampatia kila mmoja nafasi ya kuushiriki bila ya ubaguzi au mtu yeyote kukosa.

Lakini tukumbuke kwamba kitendo hiki cha Yesu kujishusha hivi na kukubali kukaa katika mkate wa kawaida kama hostia tayari kimeshawafanya wengi wamdharau Yesu. Wengi wetu tunakosa imani kwa Ekaristi-wengi wetu tunajiuliza je, kweli huu mkate ni Yesu kweli? Unaweza kutupatia uzima wa milele? na huu uzima unatoka wapi? Sasa, kitendo cha Yesu kuwa katika hali ya kiunyenyekevu namna hii kinamfanya aonekane kana kwamba hana nguvu. Lakini ukweli ni kwamba unyenyekevu wa Yesu usitufanye tusimheshimu.

Ekaristi Takatifu ni Yesu kweli na ndugu yangu nakuomba sisi tuendelee kutoa heshima kwa Ekaristi, tuendelee tu, hii ndio itakayotuokoa.Tuisiidhau hata kidogo. Kishawishi cha kuidharau ni kikubwa kwani bila imani huwezi kuiona nguvu ya Ekaristi lakini kwa walioiamini, kweli Ekaristi hutenda makubwa. Hivyo, jamani tuiheshimu Ekaristi na kuiabudu.

Katika somo la kwanza tumesikia jinsi nguvu ya Kristo mfufuka inavyotenda kazi. Leo imeweza kumgeuza yule mtesaji wa kanisa na kuwa mfuasi hodari wa Yesu. Kwa kweli jambo hili halikuwa rahisi lakini Yesu ndiye aliyependa na kwa nguvu za Yesu, haya yamefanyika-kumgeuza mtesaji wa kanisa kuwa mfuasi wa kanisa. Paulo anageuzwa kwa nguvu za Yesu, huyu huyu ambaye tunampokea katika Ekaristi. Sisi tunaopokea Ekaristi, kabla ya kuipokea tumwambie Yesu ee Yesu naomba unigeuze, nibadili mwenendo wangu. Tuache kuwa angamiza watu wema wasio na hatia labda kwa kuwasingizia uongo, kuwaonea wivu na kuwachafua, au pengine kuacha kuuwa kwa utoaji wa mimba. Yesu atugeuze kabisa tusiwe na hatia juu ya maisha ya mtu mwingine. Yesu aweza. Hili liwe ombi letu leo. Tumsifu Yesu Kristo.

 

Copyright © 2020, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

 

No comments:

Post a Comment