ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya Pasaka
Jumatano, Aprili 21, 2021
Juma la 3 la Pasaka
Mdo 8:1-8;
Zab 66:1-7 (K. 1);
Yn 6:35-40.
JE, MATESO YANA KUVUNJA MOYO?
Karibuni
ndugu zangu kwa adhimisho la Misa takatifu asubuhi ya leo. Bado tunaendelea
kufurahia baraka na neema ziletwazo na sikukuu ya pasaka na neno letu la Bwana
katika somo la letu la injili leo linatupatia matumaini makubwa sana.
Yesu
anatuambia kwamba yeye ni mkate wa uzima na anayekuja kwake hakika hataona njaa
kamwe. Anasema tena kwamba kila ajaye kwake na kumwamini hakika hatamtupa bali
atamfufua siku ya mwisho. Ndugu zangu, Yesu ni mkate wa uzima kwanza katika
Ekaristi takatifu tunayoila ambapo ni yeye mwenyewe tunayempokea na kuja ndani
yetu kutupatia uzima.
Halafu,
kwa neno lake tusikialo kila siku, neno hili huwa kwetu mkate wa uzima kwani
ndilo linalotuongoza na kutuonyesha sehemu ya kwenda kama mzaburi anavyotueleza
kwamba “Neno lako ni taa ya miguu yangu na mwanga katika njia yangu.” Yeyote
yule anayekuja kwa Yesu kwa ajili ya kumpokea katika Ekaristi na halafu tena
kwa ajili ya kuliruhusu neno lake liwe taa ya kumwongoza, hakika hatamtupa
kamwe bali atamfufua siku ya mwisho. Hili tayari tumekwisha liona hasa kwa
watakatifu kama akina Fransisko, Padre Pio na watakatifu wote: hawa walimpokea
Yesu katika Ekaristi na kulifanya neno lake liwe taa ya miguu yao na hakika
walifaulu kwa kiasi kikubwa sana. Nasi ndugu zangu tusiache hata mara moja
kuiheshimu Ekaristi takatifu na kulifanya neno la Bwana liwe taa ya kutuongoza.
Katika
somo la kwanza tumesikia habari za jinsi wale wakristo wa kwanza wanavyoendelea
kumtangaza Kristo mfufuka kwa watu. Jana tulimsikia jinsi shemasi Stefano
alivyoamua kumtangaza Kristo mfufuka kwa watu hadi kifo dini. Wayahudi
walifikiri kwamba wakristo wangeogopa na kukimbilia sehemu nyingine. Lakini cha
ajabu kumbe kile kitendo ndio kinachochea injili ihubiriwe zaidi. Leo injili
inapelekwa hadi Samaria na shemasi mwingine aitwaye Philipo. Na kilichochea
hili ni kile kifo cha Stefano. Wayahudi walifikiri kwamba kwa kumpiga chura
teke ndio wanamfanya aumie kumbe walikuwa wakimfanya aruke kwa kasi Zaidi.
Wayahudi
walifikiri kwamba kwa kuumwagia maji moto wa petrol ndio ungezima kumbe hali
ikageuka. Petrol ilipata nguvu na kutawanyika zaidi na ule moto kusambaa sehemu
nyingi zaidi. Ndivyo ilivyo ndugu zangu, pale tutakapoonesha ukatili na uonevu
kwa watu tukifikiria kwamba ndio watarudi nyuma wee-sio hivyo. Tambua kwamba
unapomnyanyasa mtu, ndio unamfanya aongeze bidii zaidi. Ni kama kumpiga chura
teke-unamsaidia aruke vizuri zaidi. Hivyo, tuache ukatili na unyanyasaji hasa
wa wadogo.
Akina
Nero walijaribu kuliangamiza kanisa na nguvu zao kwa kuamua kuwaua wale mitume
wakuu kama akina Petro na Paulo-lakini kwa kufanya hivyo, alijikuta anaufanya
ukristo ukue tena kwa kasi zaidi kwani vifo vya wale mitume wawili wakubwa
viliwahimiza wale wakristo wengine wafanye bidii zaidi kushuhudia ukristo wao.
Hivyo, kama kuna yeyote anayejidai kulipinga kanisa labda kwa kuliibia fedha,
kuliibia sadaka zake au kwa kulichafua, au kukataa kuhudhuria kanisani au
jumuiya au hata kwa kulihujumu nakwambia jua kwamba ndio unalifanya lisonge
mbele zaidi. Usiamke hata siku moja useme unapigana na kanisa, hutaweza
kushinda, kanisa lina ulinzi mkali.
Copyright ©2013-2020 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki:
see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment