“ASALI
ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari
ya Kwaresima
Alhamisi,
Machi 4, 2021.
Juma
la 2 la Kwaresima
Yer
17:5-10;
Zab
1:1-4, 6;
Lk
16:19-31
UPENDO
WA MUNGU KWA MASKINI
Karibuni ndugu zangu
wapendwa kwa adhimisho la Misa Takatifu Asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana
katika somo la kwanza tunakutana na Nabii Yeremia akitoa unabii-anasema kwamba
amelaaniwa yule amtegemeaye mwanadamu, amfanyaye Mwanadamu kuwa sababu yake
yeye kujiona salama, na kumtupia matumaini yote. Huyu hatadumu na kusonga
mbele, kwani ni kama mti uliooteshwa jangwani, pasipo na maji, au juu ya chumvi
pasipo na rutuba yoyote-na hakika hawataweza kuendelea, utanyauka tu, utatumia
nguvu nyingi bila mafanikio yoyote. Wataishi kwa kupoteza muda na rasilimali
zao.
Ujumbe huu ulielekezwa na
Yeremia kwa wana wa Yuda-wao waliacha kumtegemea Mungu awapatie ulinzi dhidi ya
mashambulizi toka taifa la Wababuloni-waliishia kulitegemea taifa la Misri liwaokoe.
Yeremia anawaeleza kwamba huku kuitegemea Misri kutawaletea laana-watapoteza
rasilimali zao na muda wao na mwishowe watapoteza hata miji na hekalu na maisha
ya wengi. Haya yaliyotabiriwa na Yeremia yaliwatokea wana wa Yuda kama
ilivyokwishatabiriwa.
Somo hili litupatie
fundisho. Litukumbushe jinsi tulivyokwishapoteza muda, rasilimali, afya na hata
uhai wa wenzetu kwa sababu ya kutokumtegemea Mungu na kutegemea nguvu zetu.
Wengi wetu ni maskini sasa na baadhi wamepoteza uhai kwa sababu ya kumtupa Mungu
pembeni. Tumwalike Mungu kati yetu kwa kila jambo. Tuanze kila kitu kwa sala,
pia tushukuru baada ya kupokea toka kwa Mungu. Hapa itatufanya tufaidi zaidi.
Tajiri tunayemsikia
katika injili aliishi kwa kutegemea nguvu zake, alijilimbikizia vyakula vingi mwenyewe
na kukataa kumshirikisha Mungu amwandalie maisha yake ya baadaye. Mwishowe
anakaribishwa kwenye Jehanamu na kila alichokifanya ulimwenguni kiliishia kuwa
bure, alipoteza muda wake na nguvu, na mali zake alipokuwa ulimwenguni.
Hazikumsaidia chochote kwa maisha ya baadaye. Alipaswa kumshirikisha Mungu.
Sisi tumshirikishe Mungu
kwa kila tufanyalo maishani. Hakika tutafaulu sana. Tusali kupata chakula
chetu, kuombea masomo yetu, magonjwa yetu na afya zetu. Hakika tutaepuka
kupoteza muda na rasilimali. Tumsifu Yesu Kristo.
Copyright
©2013-2020 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment