“ASALI
ITOKAYO MWMABANI”
Tafakari
ya Kwaresima
Ijumaa,
Machi 5, 2021,
Juma
la 2 la Kwaresima
Mwa
37:3-4, 12-13, 17-28;
Zab
105:16-21;
Mt
21:33-43, 45-46
UPENDO
UNAOTESEKA
Karibuni sana ndugu zangu
wapendwa kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana
katika somo la kwanza tunakutana na ujumbe wa Yusufu kuuzwa Misri na ndugu
zake. Ndugu zake walimuonea wivu kwa sababu ya vipaji alivyogawiwa na Mwenyezi
Mungu na kutokana na upendeleo aliokuwa nao toka kwa Baba yao. Badala ya ndugu
zake kushirikiana naye ili kwa pamoja wayafaidi mema ya nchi, wao waliona wivu,
wakamuona kama tishio na hivyo wakaamua kumuuza Misri. Cha ajabu ni kwamba kule
Misri alizidi kubarikiwa na Bwana na kufanywa Msimamizi wa mali za Pharao na
mwishowe wakaja kumpigia magoti.
Hili lilimtokea Yesu
pia-yeye alichukiwa na Wafarisayo kutokana na wivu tu-kwamba Yesu anapata
umaarufu na wafuasi kuliko wao. Lakini mwishowe, yule waliyempiga na kumuua,
walimkuta akitawala, akipigiwa kila goti na viumbe vyote mbinguni na duniani.
Sisi ndugu zangu tusitake
kumchukia yeyote. Wapo wenye uwezo zaidi yetu, wapo watakaokuwa maarufu zaidi
yetu. Wengine tutawaona wakizaliwa lakini watakuja kuwa maarufu zaidi yetu.
Tuwapokee, tushirikiane nao. Tukiwachukia hakika hatutaweza kuzuia riziki zao
au baraka zao. Ukiwachukia utawashangaa ndio wanabarikiwa zaidi-wapo watu wa
namna hii-ukiwapiga teke ndio wanasogea hatua nyingi mbele. Bahati ya mtu
haizibwi na mwanadamu. Tusitake kuja kuona sonu baadaye, tuachane na chuki za
zisizo za msingi.
Kwenye somo la injili,
Yesu anajitangaza kwamba yeye ni jiwe lililokataliwa na waashi na hakika
limekuwa jiwe kuu la msingi. Yesu anaeleza kwamba Wafarisayo watajitahidi
kumwandama wakifikiri kwamba ndio wamemteketeza lakini mwishowe watakuja
kushangaa akiwa katika utukufu wake-yaani lile jiwe lililokataliwa na
waashi-ndio litakalokuja kuwa jiwe kuu la msingi.
Hii imetokea kwa wengi,
wapo waliokataliwa kwamba hawafai lakini mwishowe ndio wamekuja kuwa tegemeo
kwa jamii, familia, taifa na kanisa. Tuepuke kumhukumu yeyote kutokana na
kabila, taifa, rangi, historia au familia. Mungu aweza kumkweza yeyote.
Tushirikiane na wenzetu ili kwa pamoja tuyafurahie mema ya nchi. Wengi
tumeshindwa kuyafurahia mema ya nchi kutokana na wivu, dharau na kuwachukia
wenzetu. Tupambane na vilema hivi ili tupate kufurahia mema ya nchi. Tumsifu
Yesu Kristo.
Copyright
©2013-2020 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment