“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya kila siku
Jumapili, Februari 7, 2021,
Juma la 5 la Mwaka wa
Kanisa
Yob 7: 1-4,6-7
Zab 146: 1-6;
1 Cor: 9: 16-19,22-23
Mk 1: 29-39
Kutokana na mahangaiko
Mara
nyingi katika maisha ya kila siku, huwa tunashuhudia watu wengi wakipatwa na
shida mbalimbali. Kwa mfano; magonjwa, vita, njaa n.k. Matatizo hayo huwa yanawakumba
watu wote; wadogo kwa wakubwa, matajiri kwa fukara, wacha Mungu na wasiomcha
Mungu. Kutokana na mahangaiko, shida, mateso na taabu hizo, watu wengi huwa
wanajiuliza:“Hivi kwa nini dunia imejawa na mateso, mahangaiko na shida mbali
mbali?’’
Cha
kushangaza zaidi ni pale watu waonapo hata wacha Mungu, kwa mfano: Viongozi wa
dini na wafuasi wengine wa dini ambao kwa namna moja au nyingine hujitahidi
sana kushika maongozi ya Mungu, nao hupatwa na mateso zaidi ya wale ambao jamii
inawaona kuwa ni watenda dhambi zaidi. Kama vile wezi, majambazi, malaya n.k.
Jibu
la maswali kama haya, ni kwamba mateso, shida na mahangaiko kweli yapo. Haya
yote ni sehemu ya maisha ya mwanadamu. Jambo la msingi ni namna ya kuyapokea na
kuyakabili hayo mateso na taabu zote. Masomo yetu ya leo, yanatupa mwongozo
mzuri na bora wa namna ya kuyapokea na kukabiliana na mateso na taabu za hapa
duniani.
Katika
somo la Kwanza, tunamkuta Ayubu, mtu ambaye alikuwa mcha Mungu sana akiwa
katika mateso makali ya magonjwa na pia mateso ya kufiwa na wanawe wote pamoja
na upotevu wa mali yake yote. Matatizo haya yana mfanya Ayubu awe mtu wa mateso
na maumivu makali sana, ingawa hapo mwanzo alikuwa mtu mwenye furaha tele.
Ayubu anafananisha mateso yake na mateso ya watumwa ambao hufanyishwa kazi
nzito kila siku toka asubuhi hadi usiku. Kwake yeye, anaona mateso yake ni
magumu mno, kwani mateso yake hayana muda wa mapumziko.
Pamoja
na mateso na mahangaiko hayo yote, Ayubu anabaki katika msimamo wake wa kuwa na
imani kwa Mungu. Baadhi ya rafiki na jamaa zake walimshauri amwasi Mungu
(amtukane tu Mungu) ili aweze kuachana na mateso na magumu hayo. Lakini kwa
ushujaa wote Ayubu alikataa kufanya hivyo na akaendelea na msimamo wake wa
kubaki katika imani kwa Mungu. Hatimaye Mungu hakumwacha mtupu.
Katika
somo la Injili, tunamkuta Bwana wetu Yesu Kristo akijionesha bayana kuwa yeye
ana nguvu au uwezo wa kuponya au kuondoa mateso na shida ambazo mwanadamu
anakabiliwa nazo.Yeye anamponya mama mkwe wa Petro, ambaye alikuwa ameshikwa na
homa kali, kwa kumshika mkono na kumwinua.
Kadiri
ya desturi za Kiyahudi, ugonjwa wa namna hii ulitibiwa kwa kufunga nywele, toka
katika kichwa cha mgonjwa, na kisu cha chuma kwa pamoja, na kisha kifurushi
hicho kiliwekwa kichakani. Baadaye, mtaalamu/mganga alifanya matambillo fulani
ambayo yaliambatana na maneno ya pekee kwa ajili ya kumtibu mgonjwa huyo.
Baadhi ya wagonjwa, walibahatika kupona, lakini wengine ilishindikana. Kumbe,
Yesu anamponya mama Mkwe wa Petro, kwa namna isiyo ya kawaida kabisa kwa
Wayahudi. Kutokana natukio hilo, watu wengi walimwamini Yesu na hivi walianza
kutangaza habari zake katika kijiji chao cha Kapernaumu.
Ilipokuwa
jioni, watu wengi, toka katika kila kona ya kijiji, walifika kwa Yesu
wakimletea wagonjwa wao ili awaponye. Yesu alifanya kazi hiyo kubwa kwa muda
mrefu. Na ilipofika asubuhi alijitenga kidogo ili kusali. Watu wakawa wana
mtafuta, kwani walifahamu fika kwamba Yesu ana nguvu za kimungu na hivi ana
uwezo wa kuponya maradhi, shida na mateso yanayowakabili. Lakini Bwana wetu
Yesu Kristo aliwaambia wanafunzi wake waondoke na kwenda mahali pengine ili
kuhubiri habari za ufalme wa Mungu huko.
Mateso,
NDW, ni sehemu ya maisha ya mwanadamu. Ni vigumu kwa mwanadamu kuondokana na
matatizo au shida ambazo humpelekea katika kupata mateso au maumivu makali.
Matatizo katika maisha ya mwanadamu ni jambo la kawaida. Jambo la msingi kwetu
sisi, ambao ni wafuasi wa Kristo ni kuyapokea na kuyakabili katika jicho la
imani kwa Mungu na Yesu Kristo ambaye ni Mkombozi wetu. Katika matatizo na
shida zetu mbali mbali hatupaswi kukimbilia kwa waganga wa kienyeji ili kuagua
au kupata tiba zisizo za kweli. Bali yatupasa kumkimbilia Bwana wetu Yesu
Kristo.
------------------------
Copyright
©2013-2020 ©FurKat, FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment