Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA DESEMBA 26, 2022


MASOMO YA MISA,
JUMATATU, 26 DESEMBA 2022
OKTAVA YA NOELI

SIKUKUU YA MT. STEFANO, MSHAHIDI WA KWANZA


SOMO 1
Mdo. 6:8-10, 7:54-60

Stefano, akijaa neema na uwezo, alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika watu. Lakini baadhi ya watu wa sinagogi lilioitwa sinagogi la Mahuru, na la Wakirene, na la Waiskanderia, na la wale wa Kilikia na Asia, wakaondoka na kujadiliana na Stefano; lakini hawakuweza kushindana na hiyo hekima na huyo Roho aliyesema naye. Basi waliposikia maneno yake wakachomwa mioyo, wakamsagia meno.

Lakini yeye akijaa Roho Mtakatifu, akakaza macho yake, akitazama mbinguni, akauona, utukufu wa Mungu, na Yesu akisimama upande wa mkono wa kuume wa Mungu. Akasema, Tazama, naona mbingu zimefunguka, na Mwana wa Adamu amesimama mkono wa kuume wa Mungu. Wakapiga kelele kwa sauti kuu, wakaziba masikio yao wakamrukia kwa nia moja, wakamtoa nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka nguo zao miguuni pa kijana mmoja aliyeitwa Sauli. Wakampiga kwa mawe Stefano, naye akiomba, akisema, Bwana Yesu, pokea roho yangu. Akapiga magoti, akalia kwa sauti kuu, Bwana, usiwahesabie dhambi hii. Akiisha kusema haya akalala. Na Sauli alikuwa akiona vema kwa kuuawa kwake.

Neno la Bwana… tumshukuru Mungu.

  
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 31:2-3, 5-7, 16, 20 (K)5

(K) Mikononi mwako, naiweka roho yangu, Ee Bwana.

Uwe kwangu mwamba wa nguvu,
Nyumba yenye maboma ya kuniokoa.
Ndiwe genge langu na ngome yangu;
Kwa ajili ya jina lako uniongoze, unichunge. (K)

Mikononi mwako naiweka roho yangu;
Umenikomboa, Ee Bwana, Mungu wa kweli.
Bali mimi namtumaini Bwana.
Na nishangilie, nizifurahie fadhili zako. (K)

Umwangaze mtumishi wako
Kwa nuru ya uso wako;
Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako. (K)


SHANGILIO

Aleluya, aleluya,
Abarikiwe yeye ajaye kwa jina la Bwana; 
Bwana ndiye aliyetupa nuru.
Aleluya.
 

INJILI
Mt. 10:17-22

Yesu aliwaambia mitume wake: Jihadharini na wanadamu; maana watawapeleka mabarazani, na katika masinagogi yao watawapiga; nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao na kwa mataifa. Lakini hapo watakapowapeleka, msifikiri-fikiri jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayosema. Kwa kuwa si ninyi msemao, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu.

Na ndugu atamsaliti nduguye ili auawe, na baba atamsaliti mwana, na wana watawainukia wazazi wao, na kuwasafisha. Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu; lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment