MASOMO YA MISA, DESEMBA 20, 2020
DOMINIKA YA 4 YA MAJILIO
Somo la I
2Sam 7: 1-5, 8-11, 16
Ikawa, mfalme alipokuwa akikaa katika
nyumba yake, hapo BWANA alipomstarehesha, asiudhiwe na adui zake waliomzunguka
pande zote, mfalme akamwambia Nathani, nabii, Angalia sasa, mimi ninakaa katika
nyumba ya mierezi, bali sanduku la Mungu linakaa ndani ya mapazia. Nathani
akamwambia mfalme, Haya, fanya yote yaliyomo moyoni mwako; maana BWANA yu
pamoja nawe. Ikawa usiku uo huo, neno la BWANA likamfikia Nathani kusema,
Enenda, ukamwambie mtumishi wangu, Daudi, BWANA asema hivi, Je! Wewe
utanijengea nyumba, nikae ndani yake? Basi, sasa, mwambie mtumishi wangu,
Daudi, maneno haya, BWANA wa majeshi asema hivi, Nalikutwaa katika zizi la
kondoo, katika kuwaandama kondoo, ili uwe mkuu juu ya watu wangu, juu ya
Israeli; nami nimekuwa pamoja nawe kila ulikokwenda, na kuwakatilia mbali adui
zako wote mbele yako; nami nitakufanyia jina kuu, kama jina la wakuu walioko
duniani. Tena nitawaagizia mahali watu wangu Israeli, nami nitawapanda, wapate
kukaa mahali pao wenyewe, wasiondolewe tena; wala wana wa uovu hawatawatesa
tena, kama hapo kwanza; naam, kama vilivyokuwa tangu siku ile nilipowaamuru
waamuzi, wawe juu ya watu wangu Israeli; nami nitakustarehesha mbele ya adui
zako wote.Tena BWANA anakuambia ya kwamba BWANA atakujengea nyumba.
Na nyumba yako, na ufalme wako,
vitathibitishwa milele mbele yako. Nacho kiti chako kitafanywa imara milele.
Neno la Bwana.....tumshukuru Mungu.
Wimbo wa katikati
Zab 89: 1-4, 26, 28
Fadhili za BWANA nitaziimba milele;
Kwa kinywa changu nitavijulisha vizazi
vyote uaminifu wako.
Maana nimesema,
Fadhili zitajengwa milele;
Katika mbingu utauthibitisha uaminifu
wako.
(K) Fadhili za BWANA nitaziimba milele
Nimefanya agano na mteule wangu,
Nimemuapia Daudi, mtumishi wangu.
Wazao wako nitawafanya imara milele,
Nitakijenga kiti chako cha enzi hata
milele.
(K)
Yeye ataniita, Wewe baba yangu,
Mungu wangu na mwamba wa wokovu wangu.
Hata milele nitamwekea fadhili zangu,
Na agano langu litafanyika amini kwake.
(K)
Somo la 2
Rum 16: 25 - 27
Sasa na atukuzwe yeye awezaye kuwafanya
imara, sawasawa na injili yangu na kwa kuhubiriwa kwake Yesu Kristo, sawasawa
na ufunuo wa ile siri iliyositirika tangu zamani za milele, ikadhihirishwa
wakati huu kwa maandiko ya manabii, ikajulikana na mataifa yote kama
alivyoamuru Mungu wa milele, ili waitii Imani.Ndiye Mungu mwenye hekima peke
yake. Utukufu una yeye kwa Yesu Kristo, milele na milele, Amina.
Neno la Bwana......Tumshukuru Mungu.
Shangilio (Lk 1: 38)
Aleluya aleluya
Mariamu akasema, Tazama mimi ni mjakazi wa Bwana; Na iwe
kwangu kama ulivyosema.
Kisha malaika akaondoka akaenda zake
Aleluya
Injili
Lk 1:26 - 38
Malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda
mpaka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti, kwa mwanamwali bikira aliyekuwa
ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa mbari ya Daudi; na jina lake bikira huyo
ni Mariamu. Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa neema, Bwana yu
pamoja nawe. Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni,
Salamu hii ni ya namna gani? Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana
umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na
jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana
Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo
hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho. Mariamu akamwambia malaika,
Litakuwaje neno hili, maana sijui mume? Malaika akajibu akamwambia, Roho
Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama
kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa
Mungu. Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto
mwanamume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa;
kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu. Mariamu akasema, Tazama, mimi ni
mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika akaondoka
akaenda zake.
Neno la Bwana.......sifa kwako Ee Kristo.
-------------------------
Copyright © 2020, "MASOMO YA
MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings
reproduced by FurahayaKikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment