MASOMO
YA MISA,
ALHAMISI, SEPTEMBA 18, 2025
JUMA
LA 24 LA MWAKA
________
SOMO
1
1Tim 4:12-16
Mtu awaye yote asiudharau ujana wako, bali uwe kielelezo kwao waaminio, katika usemi na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi. Hata nitakapokuja, ufanye bidii katika kusoma na kuonya na kufundisha. Usiache kuitumia karama ile iliyomo ndani yako, uliyopewa kwa unabii na kwa kuwekewa mikono ya wazee. Uyatafakari hayo; ukae katika hayo; ili kuendelea kwako kuwe dhahiri kwa watu wote. Jitunze nafsi yako, na mafundisho yako. Dumu katika mambo hayo; maana kwa kufanya hivyo utajiokoa nafsi yako na wale wakusikiao pia.
________
WIMBO
WA KATIKATI
Zab. 111:7-10
(K) Matendo ya Bwana ni makuu.
Matendo ya mikono yake ni kweli na hukumu,
Maagizo yake yote ni amini,
Yamethibitika milele na milele,
Yamefanywa katika kweli na adili. (K)
Amewapelekea watu wake ukombozi,
Ameamuru agano lake liwe la milele,
Jina lake ni takatifu la kuogopwa. (K)
Kumcha Bwana ndio mwanzo wa hekima,
Wote wafanyao hayo wana akili njema,
Sifa zake zakaa milele. (K)
________
SHAGILIO
1Pet.
1:25
Aleluya,
aleluya,
Neno
la Bwana hudumu hata milele, na neno hilo ni neno lile jema lililohubiriwa
kwenu.
Aleluya.
________
INJILI
Lk 7:36-50
Mtu mmoja katika Mafarisayo alimwalika ale chakula kwake; akaingia katika nyumba yake yule Farisayo, akaketi chakulani. Na tazama, mwanamke mmoja wa mji ule, aliyekuwa mwenye dhambi, alipopata habari ya kuwa ameketi chakulani katika nyumba ya yule Farisayo, alileta chupa ya marimari yenye marhamu. Akasimama nyuma karibu na miguu yake, akilia, akaanza kumdondoshea miguu machozi yake, na kuipangusa kwa nywele za kichwa chake, akiibusu-busu miguu yake na kuipaka yale marhamu.
Basi, yule Farisayo aliyemwalika alipoona vile, alisema moyoni mwake, Mtu huyu kama angekuwa nabii, angemtambua mwanamke huyu amgusaye, ni nani, naye ni wa namna gani, ya kwamba ni mwenye dhambi. Yesu akajibu akamwambia, Simoni, nina neno nitakalo kukuambia. Akasema, Mwalimu, nena. Akasema, Mtu mmoja mkopeshaji alikuwa na wadeni wawili; mmoja amwia dinari mia tano, na wa pili hamsini. Nao walipokuwa hawana cha kumlipa, aliwasamehe wote wawili. Katika hao wawili ni yupi atakayempenda zaidi? Simoni akajibu akasema, Nadhani ni yule ambaye alimsamehe nyingi. Akamwambia, Umeamua haki.
Akamgeukia yule mwanamke, akamwambia Simoni, Wamwona mwanamke huyu? Niliingia nyumbani kwako, hukunipa maji kwa miguu yangu; bali huyu amenidondoshea machozi miguu yangu, na kuipangusa kwa nywele za kichwa chake. Wewe hukunibusu; lakini huyu tangu nilipoingia hakuacha kunibusu sana miguu yangu. Hukunipaka kichwa changu mafuta; bali huyu amenipaka miguu yangu marhamu. Kwa ajili ya hayo nakuambia, Amesamehewa dhambi zake ambazo ni nyingi, kwa kuwa amependa sana; lakini asamehewaye kidogo, huyo hupenda kidogo. Kisha alimwambia mwanamke, Umesamehewa dhambi zako. Ndipo wale walioketi chakulani pamoja naye walianza kusema mioyoni mwao, Ni nani huyu hata asamehe dhambi? Akamwambia yule mwanamke, Imani yako imekuokoa, enenda zako kwa amani.
Neno
la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright
© 2025, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora
– Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com
No comments:
Post a Comment