“ASALI
ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari
ya kila siku
Alhamisi,
Agosti 15 2024
Juma
la 19 la Mwaka
SIKUKUU
YA KUPALIZWA BIKIRA MARIA MBINGUNI
Ufu
11:19, 12:1-6, 10;
Zab
45:9-11, 15 (K) 10;
1Kor
15:20-26;
Lk
1:39-56
MALENGO
YA JITIHADA ZETU!
Katika
sikukuu ya Kupalizwa Mbinguni kwa Mama wa Mungu, tunafanya sherehe ya Bikira
Maria kutoka katika hali ya ubinadamu mpaka kufika hali ya mwenye heri. Kwa
kumtafakari Bikira Maria katika utukufu wake, tunaelewa kuwa hapa duniani sio
kwetu bali tu wapitaji, pia tunaelewa kuwa tunatakiwa kuishi hapa duniani
tukiwa tumejawa na tamaa ya vitu vya mbinguni basi kwa kufanya hivyo tutarithi
vivyo vitu katika ufalme wa milele. Kwa kusema hivyo basi tujitahidi kutunza
amani na utulivu wa mioyo yetu, japokuwa tumesongwa na magumu ya maisha.
Mwangaza wa Bikira Maria akiwa amechukuliwa mbinguni huendelea kuonekana
japokuwa wingi zito la huzuni na mateso limetanda.
Katika
sikukuuu ya Kupalizwa Mbinguni Bikira Maria tunakumbuka kushiriki kwa Bikira
Maria katika Ufufuko wa mwanae, kwa kupalizwa mbinguni mwili na roho,
alipomaliza kile alichokijia hapa duniani. Kupalizwa Mbinguni kunatuonyesha
kile kitakachotutokea pale tutakapofufuliwa siku ya mwisho. Kupalizwa mbinguni
ndio lengo kuu la maisha yetu kama Wakristo.
Kama
vile Mt. Paulo atuambiapo kuwa, tutafufuliwa na miili yetu iliyo tukuka kama
ilivyokuwa kwa Kristo. Kwa ile nguvu ya Yesu mfufuka tutaweza kuungana na Baba
katika utukufu wa Kristo, kama vile Bikira Maria anavyoshiriki katika muungano
huo kwa sasa. Kupalizwa Mbinguni ni siku ambayo tunaitwa kutafakari kwa kina
malengo ya maisha yetu, na urithi wa uzima wa milele.
Kwa
kusema hivyo basi tujitahidi kuyawaza hayo kila siku. Inatulazimu kufikiria
kuwa tumesimama na Bikira Maria na mwezi nchini ya miguu yake, akiwa wamevaa
taji la jua na nyota kichwani mwake. Pia inatubidi kumwona yule joka
limefungwa, na kila mmoja wetu kwa neema aliyopewa na Mungu na kwa msaada wa
Bikira maria anatakiwa kumzaa Kristo katika maisha yake. kwa kufanya hivyo basi
tutakuwa na uhakika wa kufufuliwa mwili na roho.kwa kufanya hivyo basi tunakuwa
tumepata maana halisi ya maisha yetu, na kwamba ukweli unaoelezewa katika
mafundisho ya kanisa juu ya kupalizwa Bikira Maria ndio utimilifu wa matamanio
ya maisha yetu.
Sala:
Ewe mama uliyejaa msamaha, utukufu wako unisaidie kuyabeza na kuyachukia yale
yaliyo ya dunia na kutamani yale yaliyo ya mbinguni. Amina
No comments:
Post a Comment