MASOMO YA MISA, MEI 25, 2025
DOMINIKA YA 6 YA PASAKA, MWAKA C
MWANZO:
Isa. 48:20
Hubirini kwa sauti ya kuimba, tangazeni haya
yatamkeni mpaka mwisho wa dunia, semeni, Bwana amelikomboa taifa lake, aleluya.
SOMO 1
Mdo. 15 :1-2, 22-29
Walishuka watu waliotoka Uyahudi wakawafundisha
wale ndugu ya kwamba, Msipotahiriwa kama desturi ya Musa hamwezi kuokoka. Basi
baada ya Paulo na Barnaba kushindana na watu hawa na kuhojiana nao sana, ndugu
wakaamuru kwamba Paulo na Barnaba na wengine miongoni mwao wapande kwenda
Yerusalemu kwa mitume na wazee kwa habari ya swali hilo.
Basi ikawapendeza mitume na wazee na kanisa lote
kuwachagua watu miongoni mwao na kuwapeleka Antiokia pamoja na Paulo na
Barnaba; nao ni hawa, Yuda aliyeitwa Barsaba, na Sila, waliokuwa watu wakuu
katika ndugu. Wakaandika hivi na kupeleka kwa mikono van Mitume na ndugu wazee,
kwa ndugu zetu walioko Antiokia na Shamu na Kilikia, walio wa Mataifa; Salamu.
Kwa kuwa tumesikia ya kwamba watu waliotoka kwetu wamewasumbua kwa maneno yao,
wakipotosha roho zenu, ambao sisi hatukuwaagiza; sisi tumeona vema, hali
tumepatana kwa moyo mmoja, kuwachagua watu na kuwapeleka kwenu pamoja na
wapendwa wetu Barnaba na Paulo, watu waliohatirisha maisha yao kwa ajili ya
jina la Bwana wetu Yesu Kristo. Basi tumewatuma Yuda na Sila, watakaowaambia
wenyewe maneno yayo hayo kwa vinywa vyao. Kwa maana ilimpendeza Roho Mtakatifu
na sisi, tusiwatwike mzigo ila hayo yaliyo lazima, yaani, mjiepushe na vitu
vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, na nyama zilizosongolewa, na
uasherati. Mkijizuia na hayo, mtafanya vema. Wasalamu.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 67:1-5, 7, (K) 3
(K) Watu na wakushukuru, Ee Mungu, Watu wote na
wakushukuru.
Au: Aleluya.
Mungu na atufadhili na kutubariki,
Na kutuangazia uso wake.
Njia yake ijulike duniani,
Wokovu wake katikati ya mataifa yote. (K)
Mataifa na washangilie,
Naam, waimbe kwa furaha,
Maana kwa haki utawahukumu watu,
Na kuwaongoza mataifa walioko duniani. (K)
Watu na wakushukuru, Ee Mungu,
Watu wote na wakushukuru.
Mungu atatubariki sisi;
Miisho yote ya dunia itamcha Yeye. (K)
SOMO 2
Ufu. 21 : 10-14, 22-23
Siku ile, mimi Yohana, Nilichukuliwa katika Roho
mpaka mlima mnkubwa, mrefu, akanionyesha ule mji mtakatifu, Yerusalemu,
ukishuka kutoka mbinguni kwa Mwenyezi Mungu; wenye utukufu wa Mungu, na
mwangaza wake ulikuwa mfano wa kito chenye thamani nyingi kama kito cha yaspi,
safi kama bilauri; ulikuwa na ukuta mkubwa, mrefu, wenye milango kumi na
miwili, na katika ile milango malaika kumi na wawili; na majina yameandikwa
ambayo ni majina ya kabila kumi na mbili za Waisraeli. Upande wa mashariki
milango rnitatu; na upande wa kaskazini milango mitatu; na upande wa kusini
milango mitatu; na upande wa magharibi milango mitatu. Na ukuta wa mji ulikuwa
na misingi kumi na miwili, na katika ile misingi majina kumi na mawili ya wale
mitume kumi na wawili wa Mwana-Kondoo.
Nami sikuona hekalu ndani yake, kwa maana Bwana
Mungu Mwenyezi na Mwana-Kondoo, ndio hekalu lake. Na mji ule hauhitaji jua wala
mwezi kuuangaza, kwa maana utukufu wa Mungu huutia nuru, na taa yake ni
Mwana-Kondoo.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
SHANGILIO
Yn. 14 : 23
Aleluya, aleluya,
Yesu alisema: Mtu akinipenda, atalishika neno
langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake.
Aleluya.
INJILI
Yn. 14:23-29
Yesu aliwaambia wafuasi wake: Mtu akinipenda,
atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya
makao kwake. Mtu asiyenipenda, yeye hayashiki maneno yangu; nalo neno
mnalolisikia silo langu, ila ni lake Baba aliyenipeleka.
Hayo ndiyo niliyowaambia wakati nilipokuwa
nikikaa kwenu. Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba
atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote
niliyowaambia.
Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo
mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga,
Mlisikia ya kwamba mimi naliwaambia, Naenda zangu, tena naja kwenu. Kama
mngalinipenda. mngalifurahi kwa sababu naenda kwa Baba; kwa maana Baba ni mkuu
kuliko mimi. Na sasa nimewaambia kabla halijatokea, kusudi litakapotokea mpate
kuamini.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo
Copyright © 2025, "MASOMO YA MISA"
published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by
Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com
No comments:
Post a Comment