
“KUFUFUKA NA KRISTO”
Tafakari ya Pasaka
Jumanne, Aprili 22, 2025,
Oktava ya Pasaka
Mdo 2:36-41
Zab 33:4-5,18-20,22
Yn 20:11-18.
UFUFUKO: WITO WA KUKUWA KATIKA MAHUSIANO NA YESU!
Leo Maria Magdalena anarudi Kaburini baada ya Simoni Petro na
Yohane wameshaondoka. Akili ya ufufuko inaonekana haijaingia katika akili yake,
ingawaje yeye mwenyewe alikuwa amefufuka katika kaburi katika kufungwa na pepo
saba (Lk 8:2). Baada ya kuona kaburi li wazi anabubujika machozi. Uwepo wa
malaika haukumuogopesha, kwasababu alikuwa na huzuni kubwa kwasababu ya
kupotelewa na mkombozi wa roho yake. Yesu anamtokea ghafla katika huzuni yake
na kwa furaha, anasema “Rabi!” Mwalimu!. Yesu anamwambia asimshike.
Huu ulikuwa ni wakati ambao Maria alikuwa na hisia. Alikuwepo
alipokuwa akitazama msalaba. Alimfahamu Yesu vizuri na alimpenda sana.
Alimtazama akifa na ghafla sasa anamtamzama akiwa amefufuka amesimama mbele
yake. Ni wazi kwamba alipatwa na furaha kubwa. Yesu hakuwa mkali kwa Maria kwa
kumwambia kwamba asimshike. Alikuwa anampa ushauri mzuri na muelekeo wa safari
ya maisha yake ya kiroho na Yesu. Alikuwa anamwambia kwa hakika kwamba, hali
yetu sasa inabadilika, na kuwa katika hali ya ndani zaidi. Alimwambia
usinishike kwasababu ‘hajapaa kwenda kwa Baba bado’.
Kwa wakati huo uhusiano wa Maria ulikuwa katika ngazi ya
kibinadamu. Alipata muda wa kuwa na Yesu, kuwa karibu na Yesu na kumsikiliza,
na alimpenda kwa moyo wote wa kibinadamu. Lakini Yesu alipenda yeye na sisi
wote, tumpende sasa katika ngazi ya Kimungu. Akiwa katika kiti chake cha enzi
Mbinguni anaweza sasa kuingia katika mioyo yetu. Anaweza kuingia ndani ya moyo
wa Maria na sisi wote. Anaweza kuishi ndani yetu nasi ndani yake. Na yeye kuwa
mmoja pamoja nasi.
Kwa kuacha ngazi ya upendo wa kibinadamu tu na Yesu, Maria aliweza
sasa kumpenda katika ngazi ya juu ambayo asingeweza kama alikuwa katika ngazi
ya Kibinadamu. Huu ni muunganiko wa Kimungu, ambao kila mmoja wetu anaitwa.
Yesu sasa ameshafufuka na sasa tunaweza kushiriki matunda ya ufufuko wake.
Sisi, na Maria, tunaweza sasa kumuweka ndani ya mioyo yetu, kwasababu ndiye
anaye tutegemeza sisi.
Sala: Bwana, ninaomba niungane nawe kama wewe ulivyo ungana na
mimi. Ninaomba akili, moyo na utashi wangu wote uwe wako. Ninaomba uje uishi
ndani ya moyo wangu nami niishi ndani ya moyo wako. Nayatoa maisha yangu kwako,
Bwana mpendwa, ninakuomba nikupe yote niliyo nayo na jinsi nilivyo. Yesu,
nakuamini wewe. Amina
No comments:
Post a Comment