MASOMO YA MISA, APRILI 6, 2025
DOMINIKA YA 5 YA KWARESIMA MWAKA C
MWANZO:
Zab. 43:1-2
Ee Bwana, unihukumu, unitetee kwa taifa lisilo
haki, uniokoe na mtu asiye haki. Kwa kuwa wewe ndiwe Mungu uliye nguvu zangu.
SOMO 1
Isa. 43:16-21
Bwana asema hivi, yeye afanyaye njia katika
bahari, na mahali pa kupita katika maji yenye nguvu; atoaye gari na farasi,
jeshi la askari na uwezo; wamelala, hawataondoka; wametoweka, wamezimwa mfano
wa utambi. Msiyakumbuke mambo ya kwanza, wala msiyatafakari mambo ya zamani.
Tazama, nitatenda neno jipya; sasa litachipuka; je! Hamtalijua sasa? Nitafanya
njia hata jangwani, na mito ya maji nyikani. Wanyama wa kondeni wataniheshimu,
mbweha pia na mbuni; kwa sababu nimewapa maji jangwani, na mito nyikani, ili
kuwanywesha watu wangu, wateule wangu; watu wale niliojiumbia nafsi yangu, ili
wazitangaze sifa zangu.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 126, (K) 3
(K) Bwana alitutendea mambo makuu, tulikuwa
tukifurahi.
Bwana alipowarejeza mateka wa Sayuni,
Tulikuwa kama waotao ndoto.
Ndipo kinywa chetu kilipojaa kicheko.
Na ulimi wetu kelele za furaha. (K)
Ndipo waliposema katika mataifa,
Bwana amewatendea mambo makuu.
Bwana alitutendea mambo makuu,
Tulikuwa tukifurahi. (K)
Ee Bwana, uwarejeze watu wetu waliofungwa,
Kama vijito vya Kusini.
Wapandao kwa machozi,
Watavuna kwa kelele za furaha. (K)
Ingawa mtu anakwenda zake akilia,
Azichukuapo mbegu za kupanda.
Hakika atarudi kwa kelele za furaha,
Aichukuapo miganda yake. (K)
SOMO 2
Flp. 3:8-14
Nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya
uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake
nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo;
tena nionekane katika yeye, nisiwe na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa
sheria, bali ile ipatikanayo kwa Imani iliyo katika Kristo, haki ile itokayo
kwa Mungu, kwa Imani; ili nimjue yeye, na uweza wa kufufuka kwake, na ushirika
wa mateso yake, nikifananishwa na kufa kwake; ili nipate kwa njia yoyote
kuifikia kiyama ya wafu. Si kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu;
la! Bali nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo kwa ajili yake
nimeshikwa na Kristo Yesu. Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha
kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia
yaliyo mbele; nakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu
katika Kristo Yesu.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
SHANGILIO
Yoe. 2:12, 13
Lakini hata sasa, asema Bwana, nirudieni mimi
kwa mioyo yenu yote, kwa maana ni mwenye neema na huruma.
INJILI
Yn. 8:1-11
Yesu akaenda mpaka mlima wa Mizeituni. Hata
asubuhi kulipokucha akaingia tena hekaluni, na watu wote wakamwendea; naye
akaketi, akawa akiwafundisha.
Waandishi na Mafarisayo wakamletea mwanamke
aliyefumaniwa katika uzinzi, wakamweka katikati. Wakamwambia, Mwalimu, mwanamke
huyu amefumaniwa alipokuwa akizini. Basi katiak torati, Musa alituamuru
kuwapiga kwa mawe wanawake namna hii; nawe wasemaje? Nao wakasema neno hili
wakimjaribu, ili wapate sababu ya kumshitaki.
Lakini Yesu akainama, akaandika kwa kidole chake
katika nchi. Nao walipozidi kumhoji, alijiinua, akawaambia, Yeye asiye na
dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe. Akainama tena,
akaandika kwa kidole chake katika nchi. Nao waliposikia, wakashitakiwa na
dhamiri zao, wakatoka mmoja mmoja, wakianzia tangu wazee hata wa mwisho wao;
akabaki Yesu peke yake, na yule mwanamke amesimama katikati.
Yesu akajiinua asimwone mtu ila yule mwanamke,
akamwambia, Mwanamke, wako wapi wale washitaki wako? Hakuna aliyekuhukumu kuwa
na hatia? Akamwambia, Hakuna, Bwana. Yesu akamwambia, Wala mimi sikuhukumu.
Enenda zako; wala usitende dhambi tena.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright ©
2025, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com
No comments:
Post a Comment