Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, APRILI 17 2023




MASOMO YA MISA, APRILI 17, 2023
JUMA LA PILI LA PASAKA, JUMATATU


SOMO 1
Mdo. 4:23-31

Walipofunguliwa, Petro na Yohane wakaenda kwa watu wao, wakawapasha habari ya mambo yote waliyoambiwa na wakuu wa makuhani na wazee. Nao waliposikia, wakampazia Mungu sauti zao kwa moyo mmoja, wakisema, Mola, wewe ndiwe Mungu, ndiwe uliyefanya mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo; nawe ulinena kwa Roho Mtakatifu kwa kinywa cha babaetu Daudi, mtumishi wako.

Mbona mataifa wamefanya ghasia, na makabila wametafakari ubatili? Wafalme wa dunia wamejipanga, na wakuu wamefanya shauri pamoja juu ya Bwana na juu ya Kristo wake.

Maana ni kweli, Herode na Pontio Plato pamoja na Mataifa na watu wa Israeli, walikusanyika katika mji huu juu ya Mtumishi wako mtakatifu Yesu, uliyemtia mafuta, ili wafanye yote ambyo mkono wako na mashauri yako yamekusudia tangu zamani yatokee. Basi sasa, Bwana, yaangalie matisho yao; ukawajalie watumwa wako kunena neno lako kwa ujasiri wote, ukinyosha mkono wako kuponya; ishara na maajabu vifanyike kwa jina la Mtumishi wako mtakatifu Yesu. Hata walipokwisha kumwomba Mungu, mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.



WIMBO WA KATIKATI
Zab. 2:1-9 (K) 13

(K) Heri wale wanaomkimbilia Mungu. au Aleluya.

Mbona mataifa wanafanya ghasia,
Na makabila wanatafakari ubatili?
Wafalme wa dunia wanajipanga,
Na wakuu wanafanya shauri pamoja,
Juu ya Bwana, Na juu ya masihi wake,
Na tuvipasue vifungo vyao,
Na kuzitupia mbali nasi Kamba zao. (K)

Yeye aketiye mbinguni anacheka,
Bwana anawafanyia dhihaka.
Ndipo atakaposema nao kwa hasira yake,
Na kuwafadhaisha kwa ghadhabu yake.
Nami nimemweka mfalme wangu,
Juu ya Sayuni, mlima wangu mtakatifu. (K)

Nitaihubiri amri; Bwana aliniambia,
Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa.
Uniombe, nami nitakupa mataifa kuwa urithi wako,
Na miisho ya dunia kuwa milki yako.
Utawaponda kwa fimbo ya chuma,
Na kuwavunja kama chombo cha mfinyanzi. (K)



SHANGILIO
Lk 24:25-26

Aleluya, aleluya,
Ilimpasa Kristo kupata mateso haya na kuingia katika utukufu wake.
Aleluya.



INJILI
Yn. 3:1-8

Palikuwa na mtu mmoja wa Mafarisayo, jina lake Nikodemo, mkuu wa Wayahudi. Huyo alimjia usiku, akamwambia, Rabi, twajua ya kuwa u mwalimu, umetoka kwa Mungu; kwa maana hakuna mtu awezaye kuzifanya ishara hizi uzifanyazo wewe, isipokuwa Mungu yu pamoja naye.

Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu.

Nikodemo akamwambia, Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee? Aweza kuingia tumboni mwa mamaye mara ya pili akazaliwa?

Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu. Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa Roho ni roho. Usistaajabu kwa kuwa nilikuambia, Hamna budi kuzaliwa mara ya pili. Upepo huvuma upendako, na sauti yake waisikia, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda; kadhalika na hali yake kila mtu aliyezaliwa kwa Roho.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.


Copyright © 2023, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

No comments:

Post a Comment