MASOMO YA MISA, APRILI 23, 2025
OCTAVA YA PASAKA, JUMATANO
SOMO 1
Mdo 3:1-10
Petro na Yohane walikuwa wakikwea pamoja kwenda
hekaluni, saa ya kusali, saa tisa.
Na mtu mmoja aliyekuwa kiwete toka tumboni mwa
mamaye alichukuliwa na watu, ambaye walimweka kila siku katika mlango wa hekalu
uitwao Mzuri, ili aombe sadaka kwa watu waingiao ndani ya hekalu. Mtu huyu
akiwaona Petro na Yohane wakiingia hekaluni aliomba apewe sadaka. Na Petro,
akimkazia macho, pamoja na Yohane, akasema, Tutazame sisi. Akawaangalia,
akitaraji kupata kitu kwao. Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala
dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa
Nazareti, simama uende. Akamshika mkono wa kuume, akamwinua, mara nyayo zake na
vifundo vya miguu yake vikatiwa nguvu. Akaondoka upesi akasimama, akaanza
kwenda; akaingia ndani ya hekalu pamoja nao, akienda, akiruka-ruka, na kumsifu
Mungu.
Watu wote wakamwona akienda, akimsifu Mungu.
Wakamtambua, ya kuwa yeye ndiye aliyekuwa akiketi na kuomba sadaka penye mlango
Mzuri wa hekalu; wakajaa ushangao wakastaajabia mambo yale yaliyompata.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab 105:1-4, 6-9
(K)Bwana anajaza nchi na fadhili zake.
Au Aleluya
Mshukuruni Bwana,liitieni jina,
Wajulisheni watu matendo yake.
Mwimbieni, mwimbieni kwa zaburi,
Zitafakarini ajabu zake zote. (K)
Jisifuni kwa jina lake takatifu,
Na ufurahi moyo wao wamtafutao Bwana.
Mtakeni Bwana na nguvu zake,
Utafuteni uso wake sikuzote. (K)
Enyi wazao wa Ibrahimu, mtumishi wake;
Enyi wana wa Yakobo, wateule wake.
Yeye, Bwana, ndiye Mungu wetu;
Duniani mwote mna hukumu zake. (K)
Analikumbuka agano lake milele;
Neno lile aliloviamuru vizazi elfu.
Agano alilofanya na Ibrahimu,
Na uapo wake kwa Isaka. (K)
INJILI
Lk 24:14-35
Siku ile ile watu wawili miongoni mwao walikuwa
wakienda kijiji kimoja, jina lake Emau, kilichokuwa mbali na Yerusalemu kama
mwendo wa saa mbili. Nao walikuwa wakizungumza wao kwa wao habari za mambo hayo
yote yaliyotukia. YesuIkawa katika kuzungumza na kuulizana kwao, Yesu mwenyewe
alikaribia, akaandamana nao. Macho yao yakafumbwa wasimtambue. Akawaambia, Ni
maneno gani haya mnayosemezana hivi mnapotembea? Wakasimama wamekunja nyuso
zao.
Akajibu mmoja wao, jina lake Kleopa, akamwambia,
Je! Wewe peke yako u mgeni katika Yerusalemu, hata huyajui yaliyotukia humo
siku hizi? Akawauliza, Mambo gani? Wakamwambia, Mambo ya Yesu wa Nazareti,
aliyekuwa mtu nabii, mwenye uwezo katika kutenda na kunena mbele za Mungu na
watu wote; tena jinsi wakuu wa makuhani na wakubwa wetu walivyomtia katika
hukumu ya kufa, wakamsulibisha. Nasi tulikuwa tukitumaini ya kuwa yeye ndiye
atakayewakomboa Israeli. Zaidi ya hayo yote, leo ni siku ya tatu tangu
yalipotendeka mambo hayo; tena, wanawake kadha wa kadha wa kwetu walitushitusha,
waliokwenda kaburini asubuhi na mapema, wasiuone mwili wake; wakaja wakasema ya
kwamba wametokewa na malaika waliosema kwamba yu hai. Na wengine waliokuwa
pamoja nasi walikwenda kaburini wakaona vivyo hivyo kama wale wanawake
walivyosema, ila yeye hawakumwona.
Akawaambia, Enyi msiofahamu, wenye mioyo mizito
ya kuamini yote waliyoyasema manabii! Je! Haikumpasa Kristo kupata mateso haya
na kuingia katika utukufu wake? Akaanza kutoka Musa na manabii wote, akawaeleza
katika maandiko yote mambo yaliyomhusu yeye mwenyewe.
Wakakikaribia kile kijiji walichokuwa wakienda,
naye alifanya kama anataka kuendelea mbele. Wakamshawishi wakisema, Kaa pamoja
nasi, kwa kuwa kumekuchwa, na mchana unakwisha. Akaingia ndani kukaa nao. Ikawa
alipokuwa ameketi nao chakulani, alitwaa mkate, akaubariki, akaumega, akawapa.
Yakafumbuliwa macho yao, wakamtambua; kisha akatoweka mbele yao. Wakaambiana,
Je! Mioyo yetu haikuwaka ndani yetu hapo alipokuwa akisema nasi njiani, na
kutufunulia maandiko? Wakaondoka saa ile ile, wakarejea Yerusalemu, wakawakuta
wale kumi na mmoja wamekutanika, wao na wale waliokuwa pamoja nao, wakisema,
Bwana amefufuka kweli kweli, naye amemtokea Simoni. Nao waliwapa habari ya
mambo yale ya njiani, na jinsi alivyotambulikana nao katika kuumega mkate.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright ©
2025, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com
No comments:
Post a Comment