MASOMO YA IBAADA,
IJUMAA KUU APRILI 18, 2025
SOMO 1
Isa 52:13-53:12
Tazama, mtumishi wangu atatenda kwa busara,
atatukuzwa, na kuinuliwa juu, naye atakuwa juu sana. Kama vile wengi
walivyokustaajabia, (uso wake ulikuwa umeharibiwa sana zaidi ya mtu ye yote, na
umbo lake zaidi ya wanadamu), ndivyo atakavyowasitusha mataifa mengi; wafalme
watamfumbia vinywa vyao; maana mambo wasiyoambiwa watayaona; na mambo
wasiyoyasikia watayafahamu.Ni nani aliyesadiki habari tuliyoileta? Na mkono wa
Bwana amefunuliwa nani? Maana alikua mbele zake kama mche mwororo, Na kama
mzizi katika nchi kavu; Yeye hana umbo wala uzuri; Na tumwonapo hana uzuri hata
tumtamani. Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye
sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu
kuwa kitu. Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini
tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa. Bali alijeruhiwa
kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu
yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona. Sisi sote kama kondoo tumepotea; Kila
mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe; Na Bwana ameweka juu yake Maovu yetu
sisi sote. Alionewa, lakini alinyenyekea, Wala hakufunua kinywa chake; Kama
mwana-kondoo apelekwaye machinjoni, Na kama vile kondoo anyamazavyo Mbele yao
wakatao manyoya yake; Naam, hakufunua kinywa chake. Kwa kuonewa na kuhukumiwa
aliondolewa; Na maisha yake ni nani atakayeisimulia? Maana amekatiliwa mbali na
nchi ya walio hai; Alipigwa kwa sababu ya makosa ya watu wangu. Wakamfanyia
kaburi pamoja na wabaya; Na pamoja na matajiri katika kufa kwake; Ingawa
hakutenda jeuri, Wala hapakuwa na hila kinywani mwake. Lakini Bwana aliridhika
kumchubua; Amemhuzunisha; Utakapofanya nafsi yake kuwa dhabihu kwa dhambi, Ataona
uzao wake, ataishi siku nyingi, Na mapenzi ya Bwana yatafanikiwa mkononi mwake;
Ataona mazao ya taabu ya nafsi yake, na kuridhika. Kwa maarifa yake mtumishi
wangu mwenye haki Atawafanya wengi kuwa wenye haki; Naye atayachukua maovu yao.
Kwa hiyo nitamgawia sehemu pamoja na wakuu, Naye atagawanya nyara pamoja nao
walio hodari; Kwa sababu alimwaga nafsi yake hata kufa, Akahesabiwa pamoja na
hao wakosao. Walakini alichukua dhambi za watu wengi, Na kuwaombea wakosaji.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab 31:1, 5, 11-13, 14-16, 24
(K)Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu.
Nimekukimbilia Wewe, Bwana,
Nisiaibike milele.
Kwa haki yako uniponye,
Mikononi mwako naiweka roho yangu;
Umenikomboa, Ee Bwana, Mungu wa kweli. (K)
Kwa sababu ya watesi wangu nimekuwa laumu,
Naam, hasa kwa jirani zangu;
Na kitu cha kutisha kwa rafiki zangu;
Walioniona njiani walinikimbia. (K)
Nimesahauliwa kama mfu asiyekumbukwa;
Nimekuwa kama chombo kilichovunjika.
Maana nimesikia masingizio ya wengi;
Hofu ziko pande zote. (K)
Lakini mimi nakutumaini Wewe, Bwana,
Nimesema, Wewe ndiwe Mungu wangu.
Nyakati zangu zimo mikononi mwako;
Uniponye na adui zangu, nao wanaonifuatia. (K)
Umwangaze mtumishi wako
Kwa nuru ya uso wako;
Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako.
Iweni hodari, mpige moyo konde,
Ninyi nyote mnaomngoja Bwana. (K)
SOMO 2
Ebr 4: 14-16
Kwa kuwa tunaye Kuhani Mkuu kuliko wote ambaye ameingia mbinguni, Isa Mwana wa Mungu, basi na tushikamane sana kwa uthabiti na ule ukiri wa imani yetu. Kwa kuwa hatuna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuliana na sisi katika udhaifu wetu, lakini tunaye mmoja ambaye alijaribiwa kwa kila namna, kama vile sisi tujaribiwavyo: lakini yeye hakutenda dhambi. Basi na tukikaribie kiti cha rehema kwa ujasiri, ili tupewe rehema na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
INJILI
Yn 18:1 - 19:42
Alipokwisha kusema hayo, Yesu alitoka pamoja na
wanafunzi wake kwenda ng'ambo ya kijito Kedroni, palipokuwapo bustani; akaingia
yeye na wanafunzi wake. Naye Yuda, yule aliyetaka kumsaliti, alipajua mahali
pale; kwa sababu Yesu alikuwa akienda huko mara nyingi pamoja na wanafunzi
wake. Basi Yuda, akiisha kupokea kikosi cha askari na watumishi waliotoka kwa
wakuu wa makuhani na Mafarisayo, akaenda huko na taa na mienge na silaha. Basi
Yesu, hali akijua yote yatakayompata, akatokea, akawaambia, Ni nani
mnayemtafuta? Wao wakamjibu, Ni Yesu Mnazareti. Yesu akawaambia, Ni mimi. Yuda
naye aliyemsaliti alikuwa amesimama pamoja nao. Basi alipowaambia, Ni mimi,
walirudi nyuma, wakaanguka chini. Basi akawauliza tena, Mnamtafuta nani?
Wakasema, Yesu Mnazareti. Yesu akajibu, Nimekwisha kuwaambieni ya kwamba ni
mimi; basi ikiwa mnanitafuta mimi, waacheni hawa waende zao. Ili litimizwe lile
neno alilolisema, Wale ulionipa sikumpoteza hata mmoja wao. Basi Simoni Petro
alikuwa na upanga, akaufuta, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio la
kuume. Na yule mtumwa jina lake ni Malko. Basi Yesu akamwambia Petro, Rudisha
upanga alani mwake; je! Kikombe alichonipa Baba, mimi nisikinywee? Basi wale
askari na yule jemadari na wale watumishi wa Wayahudi walimkamata Yesu,
wakamfunga. Wakamchukua kwa Anasi kwanza; maana alikuwa mkwewe Kayafa, yule
aliyekuwa Kuhani Mkuu mwaka ule. Naye Kayafa ndiye yule aliyewapa Wayahudi lile
shauri ya kwamba yafaa mtu mmoja afe kwa ajili ya watu. Wakamfuata Yesu, Petro
na mwanafunzi mwingine. Na mwanafunzi huyo alikuwa amejulikana na Kuhani Mkuu,
akaingia pamoja na Yesu katika behewa ya Kuhani Mkuu. Lakini Petro akasimama
nje mlangoni. Basi yule mwanafunzi mwingine aliyejulikana na Kuhani Mkuu
akatoka, akasema na mngoja mlango, akamleta Petro ndani. Basi yule kijakazi,
aliyekuwa mngoja mlango, akamwambia Petro, Wewe nawe, je! Hu mwanafunzi
mmojawapo wa mtu huyu? Naye akasema, Si mimi. Na wale watumwa na watumishi
walikuwa wakisimama, wamefanya moto wa makaa; maana ilikuwa baridi; wakawa
wakikota moto. Petro naye alikuwapo pamoja nao, anakota moto. Basi Kuhani Mkuu
akamwuliza Yesu habari za wanafunzi wake, na habari za mafundisho yake. Yesu
akamjibu, Mimi nimesema na ulimwengu waziwazi; sikuzote nalifundisha katika
sinagogi na katika hekalu, wakusanyikapo Wayahudi wote; wala kwa siri mimi
sikusema neno lo lote. Ya nini kuniuliza mimi? Waulize wale waliosikia ni nini
niliyowaambia; wao wanajua niliyoyanena. Basi aliposema hayo, mtumishi
mmojawapo aliyesimama karibu alimpiga Yesu kofi akisema, Wamjibu hivi Kuhani
Mkuu? Yesu akamjibu, Kama nimesema vibaya, ushuhudie ule ubaya; bali kama
nimesema vema, wanipigia nini? Basi Anasi akampeleka hali amefungwa kwa Kayafa,
Kuhani Mkuu. Na Simoni Petro alikuwa akisimama huko, anakota moto. Basi
wakamwambia, Wewe nawe, je! Hu mwanafunzi wake mmojawapo? Naye akakana,
akasema, Si mimi. Mtumwa mmojawapo wa Kuhani Mkuu, naye ni jamaa yake yule
aliyekatwa sikio na Petro, akasema, Je! Mimi sikukuona wewe bustanini pamoja
naye? Basi Petro akakana tena, na mara akawika jimbi. Kisha wakamchukua Yesu
kutoka kwa Kayafa mpaka Praitorio, nayo ikawa alfajiri;lakini wao wenyewe
hawakuingia ndani ya ile praitorio,wasije wakanajisika,bali wapate kuila
Pasaka. Basi Pilato akawatokea nje, akasema, Ni mashitaka gani mnayoleta juu ya
mtu huyu? Wakajibu, wakamwambia, Kama huyu asingekuwa mtenda mabaya,
tusingemleta kwako. Basi Pilato akawaambia, Haya! Mtwaeni ninyi, mkamhukumu kwa
ile torati yenu! Wayahudi wakamwambia, Sisi hatuna ruhusa ya kuua mtu. Ili
litimie lile neno lake Yesu alilolisema, akionyesha ni mauti gani atakayokufa.
Basi Pilato akaingia tena ndani ya Praitorio, akamwita Yesu, akamwambia, Je!
Wewe ni Mfalme wa Wayahudi? Yesu akamjibu, Wewe wasema hivi kwa nafsi yako, au
watu wengine walikuambia habari zangu? Pilato akajibu, Ama! Ni Myahudi mimi!
Taifa lako na wakuu wa makuhani ndio waliokuleta kwangu. Umefanya nini? Yesu
akajibu, Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungekuwa wa
ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania, nisije nikatiwa mikononi mwa
Wayahudi. Lakini ufalme wangu sio wa hapa. Basi Pilato akamwambia, Wewe u
mfalme basi? Yesu akajibu, Wewe wasema, kwa kuwa mimi ni mfalme. Mimi
nimezaliwa kwa ajili ya haya, na kwa ajili ya haya mimi nalikuja ulimwenguni,
ili niishuhudie kweli. Kila aliye wa hiyo kweli hunisikia sauti yangu. Pilato
akamwambia, Kweli ni nini? Naye akiisha kusema neno hilo akawatokea Wayahudi
tena, akawaambia, Mimi sioni hatia yo yote kwake. Lakini kwenu kuna desturi ya
mimi kuwafungulia mtu mmoja wakati wa Pasaka; basi, mwapenda niwafungulie
Mfalme wa Wayahudi? Basi wakapiga kelele tena kusema, Si huyu, bali Baraba.
Naye yule Baraba alikuwa mnyang'anyi.Basi ndipo Pilato alipomtwaa Yesu,
akampiga mijeledi. Nao askari wakasokota taji ya miiba, wakamtia kichwani,
wakamvika vazi la zambarau. Wakawa wakimwendea, wakisema, Salamu! Mfalme wa
Wayahudi! Wakampiga makofi. Kisha Pilato akatokea tena nje, akawaambia, Mtu
huyu namleta nje kwenu, mpate kufahamu ya kuwa mimi sioni hatia yo yote kwake.
Ndipo Yesu alipotoka nje, naye amevaa ile taji ya miiba, na lile vazi la
zambarau. Pilato akawaambia, Tazama, mtu huyu! Basi wale wakuu wa makuhani na
watumishi wao walipomwona, walipiga kelele wakisema, Msulibishe! Msulibishe!
Pilato akawaambia, Mtwaeni ninyi basi, mkamsulibishe; kwa maana mimi sioni
hatia kwake. Wayahudi wakamjibu, Sisi tunayo sheria, na kwa sheria hiyo
amestahili kufa, kwa sababu alijifanya kuwa Mwana wa Mungu. Basi Pilato
aliposikia neno hilo, akazidi kuogopa. Akaingia tena ndani ya ile Praitorio,
akamwambia Yesu, Wewe umetokapi? Lakini Yesu hakumpa jibu lo lote. Basi Pilato
akamwambia, Husemi nami? Hujui ya kuwa mimi nina mamlaka ya kukufungua, nami
nina mamlaka ya kukusulibisha? Yesu akamjibu, Wewe hungekuwa na mamlaka yo yote
juu yangu, kama usingepewa kutoka juu; kwa hiyo yeye aliyenitia mikononi mwako
yuna dhambi iliyo kubwa zaidi. Na tangu hapo Pilato akatafuta kumfungua; lakini
Wayahudi wakapiga makelele wakisema, Ukimfungua huyu, wewe si rafiki yake
Kaisari; kila mtu ajifanyaye kuwa mfalme humfitini Kaisari. Basi Pilato,
aliposikia maneno hayo, akamleta Yesu nje, akaketi juu ya kiti cha hukumu,
mahali paitwapo Sakafu ya Mawe, au kwa Kiebrania, Gabatha. Nayo ilikuwa
Maandalio ya pasaka, yapata saa sita. Akawaambia Wayahudi, Tazama, Mfalme wenu!
Basi wale wakapiga kelele, Mwondoshe! Mwondoshe! Msulibishe! Pilato akawaambia,
Je! Nimsulibishe mfalme wenu! Wakuu wa makuhani wakamjibu, Sisi hatuna mfalme
ila Kaisari. Basi ndipo alipomtia mikononi mwao ili asulibiwe; nao wakampokea
Yesu. Akatoka, hali akijichukulia msalaba wake, mpaka mahali paitwapo Fuvu la
Kichwa, au kwa Kiebrania, Golgotha. Wakamsulibisha huko, na wengine wawili
pamoja naye, mmoja huku na mmoja huku, na Yesu katikati. Naye Pilato akaandika
anwani, akaiweka juu ya msalaba, imeandikwa, YESU MNAZARETI, MFALME WA
WAYAHUDI. Basi anwani hiyo waliisoma wengi katika Wayahudi; maana mahali pale
aliposulibiwa Yesu palikuwa karibu na mji; nayo iliandikwa kwa Kiebrania, na
Kirumi, na Kiyunani. Basi wakuu wa makuhani na Wayahudi wakamwambia Pilato,
Usiandike, Mfalme wa Wayahudi; bali ya kwamba yule alisema, Mimi ni mfalme wa Wayahudi.
Pilato akajibu, Niliyoandika nimeyaandika. Nao askari walipomsulibisha Yesu,
waliyatwaa mavazi yake, wakafanya mafungu manne, kwa kila askari fungu lake; na
kanzu nayo. Basi kanzu ile haikushonwa, ilikuwa imefumwa yote pia tangu juu.
Basi wakaambiana, Tusiipasue, lakini tuipigie kura, iwe ya nani. Ili litimie
andiko lile linenalo, Waligawanya nguo zangu, Na vazi langu wakalipigia kura.
Basi ndivyo walivyofanya wale askari. Na penye msalaba wake Yesu walikuwa
wamesimama mamaye, na umbu la mamaye, Mariamu wa Klopa, na Mariamu Magdalene.
Basi Yesu alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama
karibu, alimwambia mama yake, Mama, tazama, mwanao. Kisha akamwambia yule
mwanafunzi, Tazama, mama yako. Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua
nyumbani kwake. Baada ya hayo Yesu, hali akijua ya kuwa yote yamekwisha
kumalizika ili andiko litimizwe, akasema, Naona kiu. Kulikuwako huko chombo
kimejaa siki; basi wakatia sifongo iliyojaa siki juu ya ufito wa hisopo,
wakampelekea kinywani. Basi Yesu alipokwisha kuipokea ile siki, alisema,
Imekwisha. Akainama kichwa, akaisalimu roho yake. Basi Wayahudi, kwa sababu ni
Maandalio, miili isikae juu ya misalaba siku ya sabato, (maana sabato ile
ilikuwa siku kubwa), walimwomba Pilato miguu yao ivunjwe, wakaondolewe. Basi
askari wakaenda, wakamvunja miguu wa kwanza, na wa pili, aliyesulibiwa pamoja
naye. Lakini walipomjia Yesu na kuona ya kuwa amekwisha kufa, hawakumvunja
miguu; lakini askari mmojawapo alimchoma ubavu kwa mkuki; na mara ikatoka damu
na maji. Naye aliyeona ameshuhudia, na ushuhuda wake ni kweli; naye anajua ya
kuwa anasema kweli ili ninyi nanyi mpate kusadiki. Kwa maana hayo yalitukia ili
andiko litimie, Hapana mfupa wake utakaovunjwa. Na tena andiko lingine lanena,
Watamtazama yeye waliyemchoma. Hata baada ya hayo Yusufu wa Arimathaya, naye ni
mwanafunzi wa Yesu, (lakini kwa siri, kwa hofu ya Wayahudi), alimwomba Pilato
ruhusa ili auondoe mwili wake Yesu. Na Pilato akampa ruhusa. Basi akaenda,
akauondoa mwili wake. Akaenda Nikodemo naye, (yule aliyemwendea usiku hapo
kwanza), akaleta machanganyiko ya manemane na uudi, yapata ratli mia. Basi
wakautwaa mwili wake Yesu, wakaufunga sanda ya kitani pamoja na yale manukato,
kama ilivyo desturi ya Wayahudi katika kuzika. Na pale pale aliposulibiwa palikuwa
na bustani; na ndani ya bustani mna kaburi jipya, ambalo hajatiwa bado mtu ye
yote ndani yake. Humo basi, kwa sababu ya Maandalio ya Wayahudi, wakamweka
Yesu; maana lile kaburi lilikuwa karibu.
Copyright ©
2025, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com
No comments:
Post a Comment