
“KWARESIMA YA UKARIMU”
Tafakari ya Kwaresima
Jumanne, Aprili 15, 2025,
Juma Kuu
Isa 49: 1-6;
Zab 71: 1-6, 15, 17;
Yn 13: 21-33, 36-38.
KUWA HURU KUMCHAGUA YESU!
Ni juma la mwisho Yesu yupo na wafuasi wake kabla ya kufa. Wote
kumi na tatu wanakula mlo wa Pasaka na ni muda muhimu. Yesu anaeleza kuhusu
yule atakaye msaliti “amin nawaambieni mmoja wenu atanisaliti”. Hakuna aliye
amini kwamba atakuwa yeye, “hakika sio mimi”. Majivuno ni kitu ambacho
kinatufanya tusikubali makosa yetu na hili ndilo linalo tokea wakati wa mlo
huu. “Mtanipa nini kama nikimtoa kwenu?” ndivyo Yuda anavyomsaliti kwasababu ya
tamaa. Petro anamkana kwasababu ya woga wa maisha yake mwenyewe, anasema uongo
ili aweze kukwepa hatari.
Yesu alikuwa na moyo wa Kibinadamu na alimpenda Yuda kwa mapendo
ya Kimungu kwa njia ya moyo wake wa kibinadamu. Kwa matokeo ya upendo huu
mkamilifu wa Yesu kwa Yuda, moyo wa Yesu unasumbuka. Si kwamba Yesu
mwenyewe aliumizwa au kuwa na hasira kwa usaliti wa Yuda. Bali, ni kwamba moyo
wa Yesu ulichomwa kwa uchungu kwamba Yuda anapotea, ambaye alikuwa anampenda
kwa mapendo kamili. Yuda alikuwa na uhuru kamili, lakini alichagua kumsaliti
Yesu. Hili ni kweli hata kwetu pia. Sisi tuna uhuru kamili na tumepewa uwezo
huo huo ambayo Yuda alikuwa nao kumpenda Yesu kwa mapendo kamili au kumsaliti.
Tunaweza kuruhusu zawadi yake ya ukombozi iingie katika maisha yetu au
kuikataa. Ni juu ya uwezo wetu kamili.
Juma kuu ni kipindi cha kuzama ndani kabisa na kujitazama upo
katika barabara ipi. Kila wakati na kila siku unaitwa na Mungu kumchagua yeye
kwa upendo wako wote. Lakini kama ilivyokuwa kwa Petro na Yuda, mara nyingi
tunamkana na kumsaliti. Tunashindwa kabisa kutoa maisha yetu katika hali ya
sadaka na kwa ukarimu kama alivyo fanya Bwana. Katika juma hili kuu, tujitafiti
kwa undani kabisa, kama nipo tayari kutafuta msamaha kwa Yesu wa Huruma?
Tumrudie Yesu na tumfuate na msalaba katika juma hili.
Sala: Bwana, ninakupenda wewe, lakini ninatambua kuwa nina
kuhuzunisha moyo wako kwa kukusaliti kwangu. Nisaidie niweze kuona dhambi yangu
katika kweli juma hili. Kwa kuiona ninaomba niachane na kile kinacho nifanya
daima niwe mbali nawe katika kukupenda, ili niweze kutembea nawe katika msalaba
na kushiriki utukufu wako. Yesu, ninakuamini wewe. Amina.
No comments:
Post a Comment