
KWARESIMA YA UKARIMU”
Tafakari ya Kwaresima
Ijumaa, Aprili 11, 2025
Juma la 5 la Kwaresima
Yer 20: 10-13;
Zab 17: 2-7;
Yn 10: 31-42.
IMANI ILIYO JARIBIWA
Lirtujia ya leo inampa changamoto kila mfuasi wa Kristo kuangalia
uwiano wa maneno yake na matendo yake kama yanaendana. Katika masomo ya leo
tunasikia nabii Yeremia akiwa katikati ya matatizo na Yesu akiwa katikati ya
Wayahudi wakijianda kutaka kumpiga mawe. Nabii Yeremia aliongea kwa jina la
Mungu na kwa niaba ya Mungu na sio kwa ajili yake mwenyewe. Maneno yake
hayakupokelewa na wasikilizaji wake. Hili lilileta matatizo kwa Yeremia. Na kwa
upande wa Yesu pia, maneno yake hawakuyapokea pia.
Tukiwa tunakaribia juma kuu, na hasa ijumaa kuu, tunaona kwamba
chuki inakuwa sana juu ya Yesu. Kumchukia Yesu na kufikia katika kitendo cha
kutaka kumuua kwa mawe ni kitendo cha kutokufikiri. Taratibu taratibu wale
waliokuwa wanamchukia Yesu chuki yao ilikuwa hata kufikia kilele cha siku
ambayo Yesu anayatoa maisha yake kwa ajili yetu na kwa mapenzi makubwa kukabili
kifo. Tukikutana na mabaya na uonevu tunapaswa kuwa kama Yesu alivyofanya.
Tunapaswa tuyakabili bila woga. Aliyakabili katika ukweli na hakukubali uongo.
Ukweli wa mambo ni kwamba, kadiri tunavyosogea karibu zaidi na
Mungu, ndivyo tunavyo shambuliwa zaidi na kuchukiwa zaidi. Kitu muhimu katika
kuelekea utakatifu ni kwamba katikati ya madhulimu, mateso, magumu, na uchungu,
tunapaswa kusimamia ukweli. Mara nyingi inashawishi kufikiria kwamba huenda
tumefanya kitu kibaya wakati mambo hayaendi. Kitu kimoja ambacho Mungu anataka
tutambue katika misalaba yetu, ni kuitakasa Imani yetu na kusimamia neno lake
na ukweli. Huu ndio muda ulio muhimu kuliko muda mwingine wowote, ambapo
tunatakiwa kusimama imara. Ni rahisi kusema tunamtumainia Mungu wakati maisha
yakiwa yanaenda vizuri na inakuwa vigumu kumwamini wakati misalaba yetu inakuwa
mizito. Kabili hofu yako na muombe Mungu akubadilishe katikati ya hayo
matatizo. Ukifanya hivyo, utagundua kwamba mahangaiko makubwa katika maisha
yanabadilika kuwa Baraka kubwa.
Sala: Bwana, tunapokaribia kumbukumbu ya mateso na kifo chako,
nisaidie niunganishe matatizo yangu na yako. Nisaidie kuona katika mahangaiko
yangu ya kila siku, uwepo wako na nguvu yako. Nisaidie niweze kuona mpango
ulionao kwa changamoto hizo. Yesu, nakuamini wewe. Amina.
No comments:
Post a Comment