
“KWARESIMA YA UKARIMU”
Tafakari ya Kwaresima
Alhamisi, Aprili 17, 2025.
Juma Kuu
ALHAMISI KUU
Kut 12: 1-8,11-14;
Zab116: 12-13,15-18;
1 Kor: 11:23-26;
Yn 13: 1-15
FANYENI HIVI KWA KUNIKUMBUKA MIMI!
Leo tunaanza siku tatu, muhimu katika
Pasaka-maadhimisho matatu makuu ya Imani yetu Katoliki. Leo tunaanza na zawadi
ya Bwana wetu ya Ekaristi Takatifu tuliopewa kwa ukuhani aliosimika. Kesho
tunaingia katika fumbo la Msalaba. Na Jumamosi jioni tunaingia katika utukufu
wa ufufuko wake.
Alhamisi kuu jioni, tuna adhimisha siku
ambayo Yesu aliweka Ekaristi Takatifu, kwa kusema “fanyeni hivi kwa kunikumbuka
mimi” Tangu siku hiyo Misa Takatifu imekuwa ikiadhimishwa mara nyingi sana
katika kila pembe ya dunia kwa kutii amri ya Yesu.
Kama tungeelewa thamani na zawadi hii
Takatifu, Ekaristi Takatifu! Ekaristi Takatifu ni Mungu mwenyewe katika
ulimwengu huu, tuliopewa sisi kutugeuza na kutufanya tuwe tunachopokea.
Ekaristi Takatifu katika ukweli halisi, inatubadilisha sisi tuwe kama Kristo
mwenyewe. Tukipokea Ekaristi Takatifu tunavutwa kwenye maisha ya Kimungu ya
Utatu Mtakatifu. Tunaungana na Mungu na tunapewa chakula cha uzima wa milele.
Yesu pia alioonesha mfano wa unyenyekevu wa
hali ya juu na huduma ambayo tunapaswa kuitoa na kuiiga tunapo amua kumfuata na
kuwa wamoja pamoja naye. Aliwaosha miguu mitume ili kuwafundisha wao na sisi
kwamba mwili na damu yake tumepewa ili tuweze kupenda kama yeye alivyo penda.
Ekaristi inatugeuza kuwa watumishi wa unyenyekevu wa kweli. Tunaitwa
tuwahudumie ndugu zetu. Huduma hii inachukua hali mbali mbali lakini ndicho
tulichoitiwa kufanya. Huduma katika unyenyekevu ni muonekano mzuri wa kueleza
muunganiko wetu na Mwana wa Mungu. Ukuu unaonekana katika hali ya dunia kama
kitu kizuri na cha kutamanika. Lakini leo Yesu anatupa aina nyingine ya ukuu.
Alhamisi kuu, anaonesha kwamba ukuu huu katika unyenyekevu unapatikana katika huduma
hii. Ili kumuiga yeye inatupasa kuacha majivuno yetu kwanza. Na hili
linawezekana tunapopokea Ekaristi Takatifu tukiwa safi na wenye Imani. Ekaristi
inatusaidia kuwapenda na kuwatumikia namna hii. Na kitendo hichi cha upendo na
huduma kitashinda katika mioyo yetu kwa ajili ya Ufalme wa Mungu. Tukiwa tuna
adhimisha Alhamisi kuu, tunapata changamoto ya kuangalia unyenyekevu wetu, na
kubadilika na kujikita katika kuwahudumia wengine.
Juu ya Msalaba, alitoa maisha yake kwasababu
ya dhambi zetu na kutupatanisha na Baba. Lakini kifo chake msalabani haina
maana kwamba tutakwenda Mbinguni moja kwa moja. Tunapaswa kushirikiana na neema
yake aliotoa pale msalabani. Na hii ndio Ekaristi iliotoka ndani yake. Yesu
aliyekufa juu ya Msalaba ndiye Yesu yule yule aliye aliye juu ya altare wakati
wa misa. Ambaye alilipia dhambi zetu pale msalabani ndiye yule yule anaye tupa
neema zake na ukombozi juu ya altare wakati wa misa. Juu ya Msalaba Yesu alitoa
sadaka kamili ambayo haina haja ya kurudiwa tena. Katika altare sadaka ile ile
ya Yesu alioitoa inawekwa wazi tena kwa ajili ya ukombozi wetu. Si kwamba
inarudiwa tena bali ni sadaka ile ile ya Yesu alioitoa msalabani. Inawezekana
je? Ni kwasababu Mungu hafungwi na sehemu wala wakati wala historia, ndio maana
sadaka inakuwa ileile. Yeye anayafanya yaliotokea wakati ule yawe tena wazi juu
ya altare. Kwahiyo juu ya altare anatupa tena nguvu ya kukabili madimbwi ya
dhambi na kuingia katika uwepo wake katika hali kamili. Kwa hiyo, kilicho tokea
pale msalabani ndicho kinacho tokea altareni.
Ndivyo Yesu alivyo jikita katika kuleta
ufalme wake kwetu. Hivyo, tutakavyo kwenda kanisani leo, tuangalie kwa makini
katika hostia Takatifu na kumuona Yesu akiwa mbele yetu. Na kumuona yeye
akitupa huruma yake. Tumuone yeye akitoa upendo wake.
Sala: Bwana, nisaidie niweze kuwaza jinsi ya
kuwa mtumishi. Nisaidie niweze kuishi unyenyekevu huu kwa matendo yangu.
Ninaomba zawadi ya mwili wako Mtakatifu na damu yako vinibadilishe niweze kuwa
mtu yule ambaye unapenda niwe. Yesu, nakuamini wewe. Amina.
No comments:
Post a Comment