
“KWARESIMA YA UKARIMU”
Tafakari ya Kwaresima
Alhamisi, Machi 20, 2025.
Juma la 2 la Kwaresima
Yer 17:5-10;
Zab 1:1-4, 6;
Lk 16:19-31
UPENDO WA MUNGU KWA MASKINI
Katika mfano wa Injili ya Leo tuna mtu mmoja
ambaye ametajwa kwa jina, Lazaro. Mfano wa tajiri na Lazaro ni mfano ambao
unabaki kuwa maarufu. Ni Lazaro tu anayetambulika katika hali hii? Kwanini
Lazaro? Inawezekana ni kwasababu ya nafasi walio nayo maskini machoni pa Mungu.
Mfano huu unatuonyesha ni kwa jinsi ghani Mungu anavyo chukizwa na ukosefu wa
haki wa kuwafanya wana wake kuwa waombaji na kuwafanya kula makombo yanayotoka
katika viti vya jirani zao walio na Mafanikio. Yesu anatuita kutoka moyoni
mwake kwa ajili ya maskini. Anatuita tumuone kila mmoja hata wale maskini
kabisa na walio katika hali ya mwisho kabisa, na kuwahudumia katika hali ya utu
na heshima wanayostahili kama wanadamu wenzetu na watoto wa Mungu.
Kama ilikuwa ni kuchagua ungechagua nini?
Kuwa tajiri na kuponda maisha kila siku, ukivaa mavazi ya kitani, kuwa na kila
kitu unachopenda ulimwenguni? Au kuwa maskini uliye mwombaji, uliyefunika
vidonda vyako, kuishi katika njia ya milango, ukihisi njaa?. Ni swali rahisi
sana kujibu katika hali ya kawaida. Maisha ya utajiri na mafanikio yanavutia
katika hali ya kwanza kabisa. Lakini swala ni kwamba hayapaswa kuchukuliwa
katika hali ya kawaida, tunapaswa kuzama ndani kabisa na kulinganisha watu hawa
wawili na matokeo ya maisha yao ya ndani ya roho yao ya milele.
Kwa maskini alivyokufa, “alichukuliwa na
malaika katika kifua cha Abraham”. Na kwa tajiri, maandiko yanasema kwamba
“alikufa na kuzikwa” na kwenda kwenye “ulimwengu mwingine ambapo alikuwa
akiteseka” Sasa ni yupi unayependa kuchagua? Lengo la mfano huu ni rahisi
kabisa, tukiwa hapa duniani tunapaswa kutubu, kuacha dhambi, kusikiliza
Maandiko Matakatifu, kuamini na kuweka mioyo yetu kuelekea lengo letu la
utajiri wa mbinguni.
Tajiri huyu angeweza kumuona Lazaro na kujali
utu wake na thamani yake, yeye aliyekuwa amelala katika mlango wake, na kumuona
kwa mapendo na huruma. Lakini hakufanya hivyo. Alikuwa amejikita sana juu ya
nafsi yake. Dhambi zilimfunika macho akashindwa kumuona Lazaro. Tutafakari leo,
kama unaona dhambi yeyote ndani yako inayo fanana na huyu tajiri katika maisha
yako, ungama dhambi leo na kuziacha. Na kama umezoea kujikita katika ubinafsi,
ukijiingiza katika anaasa za hali ya juu, kumbatia umaskini wa roho, na
kujitahidi kuunganika na Mungu tu na baraka nyingi zinazokuja kwetu kwa
kukumbatia yote yale aliyo yafunua kwetu.
Sala: Bwana, niweke huru kutoka katika hali
isio faa. Nisaidie mimi niweze kubaki katika heshima ya kuwaheshimu watu wote,
na kujitoa mwenyewe kuwahudumia. Yesu, nakuamini wewe. Amina.
No comments:
Post a Comment