
“KWARESIMA YA UKARIMU”
Tafakari ya Kwaresima
Ijumaa, Machi 21, 2025,
Juma la 2 la Kwaresima
Mwa 37:3-4, 12-13, 17-28;
Zab 105:16-21;
Mt 21:33-43, 45-46
UPENDO UNAOTESEKA
Katika njia nyingi, Yusufu alikuwa mwaminifu,
alikuwa akilindwa katika upendo na kutendewa vyema na Baba yake. Lakini
kutokuwa na hatia kulimweka mashakani mara pale alipowaambia ndugu zake kuhusu
ndoto yake, na alipowaonyesha kanzu nzuri Baba yake aliyokuwa amempa. Baadaye,
ingawa ndugu zake walimpiga na kumuuza utumwani, Yusufu hakuacha kuziishi amri
za Mungu. Hata alipokuwa ameshtakiwa kwa uongo na kufungwa gerezani kwamba
alijaribu kumwingilia mke wa bwana wake kwa nguvu, yeye aliendelea kuwa imara
mbele ya Mungu. Wakati akiwa gerezani, uwezo wake wa kutafsiri ndoto ulimfikia
Farao ambaye hatimaye alimweka huru na kumweka awe mkuu baada yake. Kama Yusufu
alivyoamini kwamba, Mungu atamletea mema, Mungu alifanya hivyo kwa ajili yake
na kuutenga uovu. Nasi pia, tusikubali kamwe kumuacha Mungu tunapokabiliana na
magumu siku zote katika maisha yetu. Tumgeukia Mungu Baba yetu na kumwomba
atupiganie.
Katika hali zote za kuchukiwa na kukataliwa
kwa karne zote, kuna mmoja tu aliyesimama imara kuliko wengine wote. Kukataliwa
kwa Mwana wa Mungu. Yesu hakuwa na kitu kingine isipokuwa upendo kamili moyoni
mwake. Alipenda ubora wa kila aliyekutana naye. Na alikuwa tayari kumpa upendo
yeyote aliyekuwa tayari kuupokea. Ingawaje wengi waliupokea lakini pia wengi
waliukataa. Ni vizuri kutambua kuwa kukataliwa kwa Yesu kuliacha maumivu ya
ndani na mateso. Ni wazi kwamba mateso ya Msalabani ndio yaliokuwa ya hali ya
juu kabisa. Lakini kidonda alichohisi moyoni mwake kwa kukataliwa kilisababisha
mateso makubwa. Kuteseka namna hii ilikuwa ni kitendo cha upendo, sio kitendo
cha udhaifu. Yesu hakuteseka ndani kwasababu ya majivuno au kwasababu ya
ubinafsi wake. Bali moyo wake uliumia kwasababu alipenda kutoka ndani. Na pale
upendo huo ulipo kataliwa, ulimjaza yeye huzuni kuu (Mt 5:4).
Jaribu kufikiria kama Yesu ange amua kukata
tamaa. Jaribu kufikiria, kama kipindi cha kukamatwa kwake Yesu angeita malaika
kama jeshi kutoka mbinguni kumwokoa. Ingekuwaje kama angefanya kitendo hichi
cha kufikirika “watu hawa hawastahili!”. Matokeo yake yangekuwa tusinge pokea
zawadi ya ukombozi wa milele kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko. Mateso
yasinge badilika kwenda kwenye upendo.
Yesu alijibu kwa mapendo kamili pale alipolia
kwa sauti kuu “Baba, wasamehe, hawajui watendalo.” Kitendo hiki cha upendo
katikati ya mateso yake na kukataliwa kwake kilimfanya awe “jiwe kuu la msingi”
la Kanisa, na hivyo kuwa jiwe kuu la maisha mapya! Tunaitwa kuiga mapendo haya
na kushiriki sio tu kwakusamehe, bali pia kutoa mapendo matakatifu ya huruma.
Tukifanya hivyo, sisi pia tunakuwa jiwe la msingi la upendo na neema kwa wote
wanao hitaji zaidi.
Sala: Bwana, nisaidie mimi niweze kuwa jiwe
la pembeni. Nisaidie mimi sio nisamehe tu kila mara ninapokosewa bali pia nitoe
upendo na huruma kwao. Wewe ni Mungu na mfano kamili wa upendo huu. Ninaomba
nishiriki katika upendo huu, nikilia kwa sauti kuu pamoja nawe “Baba wasamehe,
hawajui watendalo”. Yesu, nakuamini wewe. Amina.
No comments:
Post a Comment