
“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya kila siku
Jumamosi, Februari 22, 2025
Juma la 6 la Mwaka wa Kanisa
SIKUKUU YA UKULU WA MT. PETRO (MTUME)
1 Pt 5: 1-4;
Zab 23: 1-6;
Mt 16: 13-19.
MAMLAKA YA KUTUMIKIA.
Petro alimuungama Kristo na kumkiri tena baada ya
mateso na ufufuko wake. Sisi nasi tunapaswa kumkiri Kristo na kuishi daima,
tukianguka katika dhambi daima tujue kimbilio letu ni Kristo.
Leo tunasherekea sherehe ya pekee kidogo: Kiti cha
ukuu cha mtakatifu Petro (mtume). Hii sherehe sio kwaajili ya kumheshimu mtu
binafsi kama ilivyo kawaida, sio tukio kama yalivyo mengine, bali ni Kiti cha
ukuu. Si kwamba tunasherekea sherehe ya kiti kilichotengenezwa, bali ni kiti
kama ilivyo “mwenyekiti” nafasi, mamlaka au ofisi. Leo tunasherekea kuwekwa kwa
nafasi ya mamlaka ya Kanisa. Yesu Kristo ni kichwa cha Kanisa, ofisi hii
haiondoi mamlaka yake kama kuhani mkuu na mfalme. Mungu amependa kutuchagua wanadamu,
katika nafasi ya heshima ili atushirikishe neema yake.
Petro alimuungama Yesu, kwamba “wewe ndiwe Kristo
mwana wa Mungu aliye juu” baada ya ungamo hili Yesu anamuita kwajina la Kefa,
lenye maana kwa Kigiriki ya Petro. Yesu anampa Petro nafasi ya pekee kabisa
kati ya mitume. Alikuwa ni mmoja wapo kati ya wale watatu waliokuwa na bahati
ya kuona matukio ya pekee ya Yesu, kama vile kugeuka sura kwa Yesu na mateso ya
Yesu akiwa bustanini Gestemane. Alikuwa ni mtume pekee aliyetokewa na Yesu siku
ya kwanza tuu ya ufufuko wake. Petro pia aliongea kwaniaba ya mitume wengine,
alikuwa wa kwanza kutoa jibu, mara nyingi hakuona shida kuongea ndio maana Yesu
alimuonya wakati mwingine.
Kanisa kwa miaka yake 2000 ya historia kumekuwa na
matukio ya neema na furaha, kumekuwapo changamoto za migogoro, Kipindi cha giza
na mwanga. Lakini ukweli ambao haupingiki ni kwamba Kanisa limemudu na kuonesha
kwamba Baba mtakatifu (wakili wa Petro) alipata mamlaka yake kutoka kwa Kristo
na kwamba Roho wa Kristo yupo katika Kanisa hata leo na analiogoza.
Sala: Bwana, tunakushukuru kwa zawadi ya Baba
mtakatifu, tunakuomba umuongoze aendelee kutumia mamlaka yaliyotoka kwako
katika kuwahudumia watu wote. Tunamuombea Baba Mtakatifu Fransisko na Maaskofu
waliopewa mamlaka ya kufundisha ujumbe wa habari njema. Tunakuomba uwalinde na
uwe nao na kuwapatia nguvu daima , waendelee kutuongoza kama Wachungaji wako
katika kuelekea kwenye ufalme wako. Yesu tunakuamini wewe. Amina
Copyright ©2013-2025 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki:
see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment