ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya kila siku
Jumapili, Novemba 3, 2024,
Juma la 31 la Mwaka
Kumb 6:2-6
Zab 18:2-4,47,51
Ebr 7:23-28
Mk 12:23-28
UPENDO WA JIRANI
Somo la kwanza linafuata mtiririko ambapo tunamuona Musa anawakumbusha wana
wa Israeli juu ya Amri za Mungu ambazo walizipokea kama watu wa Agano na Mungu.
Kushika amri hizi kwa uaminifu kinakuwa ndicho kigezo cha kuingia katika nchi
ya ahadi. Kiini cha somo la leo ni “sikiliza Ee Israeli”. Na huu ulikuwa wito
wa kwanza kabisa kwa kila Muisraeli mwaminifu. Ikiwa ni sawa na kutii. Sala hii
alipaswa kusali Mwisraeli kila siku asubuhi. Israeli kama taifa teule linaitwa
daima kumtii Mungu na kumsikiliza. Sisi tunapaswa kuwa watii kwa Mungu na
kumsikiliza na kutii mahusia yake. Dhambi inayotumaliza ni kiburi cha
kulichulia kawaida neno la Mungu linapo hubiriwa kwetu. Tumekuwa tukiona kana
kwamba linawahusu wengine zaidi kuliko sisi. Wakati mwingine linatusema sisi,
lakini kwasababu tumesha jihakikishia utakatifu na kujiona tayari tumesha
yaelewa mambo ya Mungu, tunafunga masikio na tunaona fundisho hili sio langu
nilamtu mwingine.
Katika hili ni wito mkubwa kabisa wa kumsikiliza Mungu kwa uaminifu na kuwa
mkweli. Kumsikiliza kwa moyo wote. Kuacha kitu kingine chochote kile ambacho
kitachukua nafasi ya Mungu. Kuacha yote na kuweka ufahamu wote kwa Mungu-nguvu
yako, moyo wako, akili yako na hata yote ulionayo.
Dhana ya kumpenda jirani kama nafsi yako katika Agano la Kale ipo pia
katika kitabu cha (Walawi 19:18). Na hivyo kuunganisha amri zote mbili, kama
Yesu alivyofanya katika somo la Injili. Yesu anatukumbusha pia kwamba kumpenda
Mungu na kumsikiliza haitengani kabisa na kuacha kuwapenda wanadamu wenzako na
kuwasikiliza. Kwa njia nyingine tusimpende Mungu kwa kisingizio cha kumchukia
jirani. Upendo wetu kwa Mungu na jirani daima iwe ndio kanuni ya Mfuasi wa
Kristo. Tunaweza kusema ndio katiba ya mfuasi wa Kristo.
Ndugu zangu tuchunguze katika maisha yetu, tuanze na Upendo wetu kwa Mungu.
Pengine upendo wetu kwa Mungu umekuwa hafifu. Muda wa kumpatatia Mungu ili
tuweze kusali pengine umeonekana kubwa msalaba mkubwa. Tumependa mambo yetu
zaidi kuliko ule muda wa sala. Hata jumapili tumejiona ni bora tufanye biashara
zetu kuliko kwenda kanisani. Kwakweli hapa tunakosa mapendo kwa Mungu. Tumpende
Mungu na muda wa sala uvutie na usiwe mzigo kwetu.
Tunakumbushwa pia juu ya mapendo yetu kwa Mwanadamu. Tuchunguze upendo wa
Mwanadamu tangu akiwa tumboni mwa mama yake. Utoaji wa mimba ni dalili wazi
kwamba upendo wa mwanadamu huyu umepungua kweli. Kutoa mimba kisa unalinda
urembo wako, au unaogopa kunyonyesha, unaogopa kuitwa mama. Ni kukosa mapendo.
Pia malumbano kati yetu na kutokusameheana ni dalili za kukosa upendo. Vita na
vurugu na kuoneana wivu mbaya kwa kweli ni vitu vinavyo dhihirisha kwamba
tunakosa mapendo.
Katika somo la Pili tunakumbushwa kwamba sisi tunaye kuhani mkuu ambaye
hakuwa na doa lolote ambaye alionesha mapendo makuu kwetu sisi. Tena alikuwa na
mapendo makuu kwa mwanadamu hata akakubali yeye mwenyewe kufa ili atukomboe
wote bila kumbagua yeyote. Hivyo sisi tuige sifa za kuhani huyu mkuu. Tuwe
tayari kujisadaka kwa jili ya wengine, tuwe wakarimu kwa Mungu, tutoe zaka na
michango ya kusaidia kueneza injili yake na huu ndio upendo na shukrani kwake.
Tusaidie mayatima na wajane, tusiwadhulumu mali zao, tuwatetee kwa kuonesha
upendo. Na hii ndiyo ishara ya kwamba tutakuwa tumeelewa ule upendo wa kuhani
wetu mkuu ambaye ni Yesu Kristo.
Copyright ©2013-2024 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki:
see www.fur-kat.blogspot
No comments:
Post a Comment