MASOMO YA MISA, NOVEMBA 16, 2024
JUMAMOSI, JUMA LA 32 LA MWAKA
SOMO 1
3Yoh. 1:5 – 8
Mpenzi, kazi ile ni ya uaminifu uwatendeayo hao ndugu na hao wageni nao, waliokushuhudia upendo wako mbele ya kanisa; utafanya vizuri ukiwasafirisha kama ipasavyo kwa Mungu. Kwa maana, kwa ajili ya Jina hilo, walitoka, wasipokee kitu kwa Mataifa. Basi imetupasa sisi kuwakaribisha watu kama hao, ili tuwe watenda kazi pamoja na kweli.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 112:1 – 6 (K) 1
(K) Heri mtu yule amchaye Bwana.
Aleluya.
Heri mtu yule amchaye Bwana,
Apendezwaye sana na maagizo yake
Wazao wake watakuwa hodari duniani;
Kizazi cha wenye adili kitabarikiwa. (K)
Nyumbani mwake mna utajiri na mali,
Na haki yake yakaa milele.
Nuru huwazukia wenye adili gizani;
Ana fadhili na huruma na haki. (K)
Heri atendaye fadhili na kukopesha;
Atengenezaye mambo yake kwa haki.
Kwa maana hataondoshwa kamwe;
Mwenye haki atakumbukwa milele. (K)
SHANGILIO
Zab. 130:5
Aleluya, aleluya,
Roho yangu inamngoja Bwana, na neno lake nimelitumainia.
Aleluya.
INJILI
Lk. 18:1-8
Yesu aliwaambia wanafunzi wake mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa. Akasema, Palikuwa na kadhi katika mji Fulani, hamchi Mungu, wala hajali watu. Na katika mji huo palikuwa na mwanamke mjane, aliyekuwa akimwendea-endea, akisema, Nipatie haki na adui wangu. Naye kwa muda alikataa; halafu akasema moyoni mwake, Ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu, lakini, kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima.
Bwana akasema, Sikilizeni asemavyo yule kadhi dhalimu. Na Mungu, je! Hatawapatia haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao? Nawaambia, atawapatia haki upesi; walakini, atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona Imani duniani?
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 2024, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com
No comments:
Post a Comment