“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya kila siku
Ijumaa, Novemba 15, 2024,
Juma la 32 la Mwaka wa Kanisa
2Yn 1:4-9
Zab 118:1-2, 10-11, 17-18
Lk 17:26-37
KUJIWEKA TAYARI KWA UPENDO!
Tunavyokaribia mwisho wa mwaka wa Lirtujia, masomo huwa yana elekeza akili zetu katika maisha ya wakati ujao, maisha baada ya maisha ya hapa duniani. Kwa kila mmoja wetu, anaelewa kwamba kifo chetu binafsi ni mwisho wa maisha yetu hapa duniani na kuingia katika maisha yajayo. Je, kuna mmoja wetu ambaye hana hofu hata kidogo juu ya kufunuliwa wakati wa hukumu kila eneo la mioyo yetu na matendo yetu yote kufunuliwa? Ni kweli kwamba tuna hofu kidogo kama tupo sawa.
Yesu leo anatuambia leo tujiweke tayari. Tuna leo tu. Jana imeshapita na haipo juu ya uwezo wetu tena, na kesho haijawapo bado. Lakini leo ipo hapa mbele yangu. Nina uwezo juu ya siku ya leo. Naweza kuchagua kupenda au kukataa. Naweza kusaidia au kuumiza. Naweza kuamini au kuwa na wasi wasi. Naweza kutumaini au kuwa na mashaka. Naweza kuishi kwa ajili ya wengine au kuishi kwa ajili ya mimi binafsi. Siku nzima imejazwa na hali zote zinazo niwezesha nipende na kumchagua Mungu. Kama kweli tunampenda Mungu na jirani hatuna haja ya kuogopa kifo na hukumu. Kinacholeta hofu na mashaka ni dhambi. Dhambi haileti raha inavyokaa moyoni au zinavyokaa moyoni. Tujipatanishe na Mungu daima ili tuishi kwa furaha tukiwa na matumaini ya wakati ujao. Tujiwekee mazoea ya kuijongea sakramenti ya kitubio ili tubaki tukiwa tumeunganika na Mungu daima.
Sala: Bwana nisaidie mimi niweze kujishughulisha kukupenda Wewe na jirani yangu. Amina
Copyright ©2013-2024 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com
No comments:
Post a Comment