Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

UFUASI MAANA YAKE UTUME



“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya kila siku
Alhamisi, Oktoba 3, 2024
Juma la 26 la Mwaka


Ayu 19: 21-27; 
Zab 27:7-9.13-14;
Lk 10: 1-12


UFUASI MAANA YAKE UTUME


Mpango wa Mungu ni kuokoa watu kwa kutumia watu kama wao wenyewe, na pia kuwaongoza watu kwa kutumia watu, kama wao. Mungu alimtuma Mwanae mpendwa, aliyezaliwa na mwanamke, Mwana wa mtu, ambaye yupo kama sisi isipokuwa dhambi. Yesu alizaliwa maskini, akafanya kazi kama mwana wa seremala, na alienda kwa Yohane mbatizaji kubatizwa kama vile ana dhambi. Lakini kwa kukiona kifo chake aliwachagua watu wengine waendeleze utume wake kwa ajili ya wokovu wa watu wengine. Petro alikuwa karibu na Yesu sana. “Simoni Mwana wa Yohane, je wanipenda mimi kuliko hawa? Alafu kulikuwa na Yakobo na Yohane ambao aliwachukua pamoja na Petro, kushuhudia kungara kwake sura na baadae mateso yake katika bustani ya Gestemane. Na pia kulikuwa na mitume wengine. Na mwisho kabisa leo tunasoma kuhusu wale sabini na wawili. Wanapewa melezo jinsi ya kuenenda katika utume wao waweze kuwa na mtazamo wa utume wao na yapi wasitende. Imani na tabia njema ndicho kiini cha utume wao. Kwanza wasali wamuombe Bwana wa mavuno, kusali ni kuweka matumaini yao kwa Mungu na tabia njema ni silaha ya kupigana na mbwa mwitu au dunia wanayo pita. 

Papa Greogori Mkuu, alisema kwamba amri kuu ya mapendo ilipaswa kutawala na kungara kwa wajumbe wote wa injili. Upendo wao kwa kila mmoja utakuwa ni ujumbe wenye nguvu. Sisi tukiwa ni wajumbe wa Kanisa tumechaguliwa na kutumwa kuwa watu wa kutangaza habari njema. Na hivyo, tukiwa ni wajumbe katika kanisa maana yake kumhubiri Kristo, kumfanya awe hai, na kumfanya yeye aheshimike katika sehemu zote ambapo Injili inatangazwa, kuaminiwa na kukiriwa.

Tusisahau wito wetu na kujitoa kwetu. Meli ipo salama inapokuwa pwani na kutulia lakini haikutengenezwa ili ikae pwani tu. Tuondoke sehemu tulipo kaa na kusonga mbele, tukimchukua Yesu pamoja nasi, hasa kwa wale ambao hawamfahamu bado na kwa wale wanao mhitaji. 

Sala: Bwana Yesu, tufanye sisi wajumbe wako wa kweli. Yesu, nakuamini wewe. Amina


Copyright ©2013-2024 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

No comments:

Post a Comment