Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA OKTOBA 20, 2024



MASOMO YA MISA OKTOBA 20, 2024
DOMINIKA YA 29 YA MWAKA B WA KANISA

SOMO 1
Isa. 53:10-11

Bwana aliridhika kumchubua; Amemhuzunisha; Utakapofanya nafsi yake kuwa dhabihu kwa dhambi, Ataona uzao wake, ataishi siku nyingi; Na mapenzi ya Bwana yatafanikiwa mkononi mwake; Ataona mazao ya taabu ya nafsi yake, na kuridhika. Kwa maarifa yake mtumishi wangu mwenye haki atawafanya wengi kuwa wenye haki; Naye atayachukua maovu yao.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 33:4-5, 18-20,22 (K) 22

(K) Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi, kama vile tulivyokungoja Wewe.

Neno la Bwana lina adili,
Na kazi yake yote huitenda kwa uaminifu.
Huzipenda haki na hukumu,
Nchi imejaa fadhili za Bwana. (K)

Tazama, jicho la Bwana li kwao wamchao,
Wazingojeao fadhili zake.
Yeye huwaponya nafsi zao na mauti,
Na kuwahuisha wakati wa njaa. (K)

Nafsi zetu ninamngoja Bwana,
Yeye ndiye msaada wetu na ngao yetu.
Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi,
Kama vile tunavyokungoja Wewe. (K)


SOMO 2
Ebra. 4:14-16

Iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na tuyashike sana maungano yetu. Kwa kuwa hatuna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi. Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu 


SHANGILIO
Efe. 1:17,18

Aleluya, aleluya!
Ewe Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Uyatie nuru macho ya mioyo yetu, ili tujue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo.
Aleluya.


INJILI
Mk. 10:35-45

Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo, walimwendea, wakamwambia, Mwalimu, twataka utufanyie lolote tutakalokuomba. Akawaambia, Mwataka niwafanyie nini? Wakamwambia, Utujalie sisi tuketi, mmoja mkono wako wa kushoto, katika utukufu wako. Yesu akawaambia, Hamjui mnaloliomba. Mwaweza kunywea kikombe ninyweacho mimi, au kubatizwa ubatizo nibatizwao mimi? Wakamwambia, Twaweza. Yesu akawaambia, Kikombe ninyweacho mimi mtakinywea, na ubatizo nibatizwao mimi mtabatizwa; lakini habari ya kuketi mkono wangu wa kuume au mkono wangu wa kushoto si langu kuwapa, ila wao watapewa waliowekewa tayari.

Hata wale kumi waliposikia wakaanza kuwakasirikia Yakobo na Yohane. Yesu akawaita, akawaambia, Mwajua ya kuwa wale wanaohesabiwa kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha. Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumishi wenu, na mtu anayetaka kuwa wa kwanza wenu, atakuwa mtumwa wa wote. Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

Copyright © 2024, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

2 comments: