Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

JE, MAHUSIANO NI KITU CHA ASILIMIA 50 KWA 50?




“MBEGU ZA UZIMA”
Tafakari ya Kila Jumapili
Jumapili, Oktoba 6, 2024.
Juma la 27 la Mwaka wa B Kanisa 

Mwa 2: 18-24;
Zab 128: 1-6 (R) 5;
Ebr 2: 9-11;
Mk 10: 2-16.


JE, MAHUSIANO NI KITU CHA ASILIMIA 50 KWA 50?

                       
Liturjia ya leo inaongelea maada nzuri sana katika maisha ya Kikristo. Ndoa kadiri ya mpango wa Mungu. Kwanini Mungu alitufanya sisi tuwe waume na wengine wawe wake? Siku hizi utamaduni wa leo ni tuonane leo na kesho hakuna kutafutana au ni tamaduni wa rafiki tu kama una kitu cha kunipatia. Siku hizi tunasikia talaka kila kukicha, ndoa za jinsia moja, udhalilishaji wa watoto nk. Mpango wa Mungu kwa ajili ya ndoa ni muhimu sana katika kulinda utu wa mwanadamu na ulimwengu wa sasa unapaswa kulitambua hili kwa undani. 

Katekisimu ya Kanisa Katoliki inasema : “Mtu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu ambaye yeye mwenyewe ni upendo. Ingawaje Mungu ameumba mume na mke,  mapendo yao ya kawaida huwa ni sura kamili na upendo usio na kipimo alionao Mungu kwa Wanadamu. Ni vyema tena vyema sana machoni mwa Mungu, na upendo huu ambao Mungu anatubariki unategemewa kuleta matunda….mke na mume waliumbwa kwa ajili ya kutegemezana…. Mwanamke ‘nyama katika nyama yangu’ ina maana kwamba yeye ni wa karibu kabisa kuliko wanyama wote na hivyo huyu amepewa na Mungu kama msaidizi, anawakilisha Mungu ambaye yeye ndiye msaada wetu.” “Na kwasababu hiyo mume atamuacha Babaye na mamaye atajiunga na mkewe nakuwa mwili mmoja” hili Mungu analidhihirisha na kwamba tangu mwanzo amelifanya hili liwe hivi, na hivyo sio wawili tena bali mwili mmoja.  (KKK 1604, 1605)

Somo la pili linaongelea mapendo ya Yesu na unyenyekevu wake. Upendo wake kwa wanadamu unakuwa mfano kamili wa mapendo ya ndoa. Kwa njaa ya Sakramenti wanandoa wamefungwa pamoja katika hali ya kutokutenganishwa, wanakuwa wamoja. Kwa kukaa kwao pamoja ni kiwakilishi na ishara ya Sakramenti, kama Yesu anavyolipenda kanisa na kuwa nalo daima. 

Somo la Injili linaeleza mambo mawili. Ndoa kutoruhusiwa kuvunjwa na uhusiano wetu na Mungu kuwa imara daima. Kila kitu ambacho Mungu amependa kiwe kutokana na mapendo yake kinapaswa kubaki daima na hakipaswi kuvunjwa. Upendo wa Mungu kwetu unakuwa ni mfano kamili wa upendo wa Ndoa. Na mfano wa watoto ni ishara ya kwamba tunapokubali Ubaba wa Mungu sisi tunakuwa watoto wake wakurithi ufalme wake. 

Kubaki katika muunganiko tunapswa kuwa tayari kuvumilia kupita katika magumu na hata kuvumia machungu. Tunapotawaliwa na mambo ya njee tuu tutashindwa kuwa na uvumilivu huu. Na hivyo kujitoa kwetu kuna kuwa kunavunjika. La muhimu linabaki kwamba :kila anayefanya mambo mazuri kwa ajili yangu basi ni mzuri kwa ajili yangu”. Kila kitu kinakuwa hakina maana wakati kinapokuwa ni kwa ajili ya matakwa ya mtu binafsi. 

Pia, kitu ambacho Mungu ametupatia sisi ni jinsia zetu. “Mungu aliumba mtu mke na mtu mume…”. Jambo hili ni jambo la hali ya hekima ya juu ya Mungu na linapaswa kurudisha utukufu kwake, jambo hili linapaswa kuheshimiwa. Kuwa mwanamke au mwamume ni kitu cha kawaida na kinapaswa kueleweka hivyo kama zawadi ya Mungu. Wakati mwingine siku hizi watu wamejaribu kubadilisha jinsia na kuanza kumpinga Mungu. Lakini ndani mwetu kabisa tunatambua kuwa mwanamke au mwanamume ni sehemu ya maumbile yetu. Inajenga hali yetu na kuleta Baraka nyingi kwa jinsi tulivyoumbwa. 

Tafakari leo na tambua kuwa wewe kuwa mume au mke ni Baraka kutoka kwa Mungu. Tafakari leo pia jinsi watu wanavyobadilisha mambo haya na kutaka kumkosoa Mungu. Jikubali kwa jinsi ulivyo, Mungu kakufanya wewe uwe wa pekee, na kubali Baraka hiyo ya Mungu itawale katika maisha yako.

Ndoa sio kitu cha asilimia 50 kwa 50, ni jambo la asilimia 100 kwa 100 muungano na agano. Na hivyohivyo katika mahusiano yetu na Mungu bado inabaki ni asilimia 100 kwa 100 hakuna wasi wasi kuhusu hili. Lakini leo tunaitwa tuangalie hata kama tumempa Mungu hata asilimia 50 tu. 

Sala: Bwana, ninakushukuru wewe kwa zawadi yako isiyo na mwisho. Nisaidie mimi niweze kukumbatia kitambulisho changu cha kujiunga na neema yako na katika muungano huo niweze kutambua zaidi utu wangu. Ninakushukuru kwa upendo wako usiokoma kwangu. Ninakuomba unisaidie na mimi niweze kurudisha upendo huo kwako na kwa watu ulionipa waliokaribu yangu. Yesu, nakuamini wewe. Amina

Copyright ©2013-2024 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

1 comment: