Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

KUFUNGUA MIOYO YETU KWA YESU



“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya kila siku
Jumatano, Septemba 18, 2024, 
Juma la 24 la Mwaka 

1 Kor 12:31 – 13:13; 
Zab 32: 2-5, 12, 22; 
Lk 7: 31-35.


KUFUNGUA MIOYO YETU KWA YESU

“Nitakifananisha na nini kizazi hiki?” Kama Yesu angeuliza swali hili hili leo katika kizazi hiki. Angetuweka wapi? Je sisi tutakuwa kama wale watoto ambao wakiwekewa muziki hawachezi hata kukiwa na maombolezo hawaombolezi? Somo la leo linatualika tuweze kuwa katika mstari mmoja na wito wa Mungu, tujitafakari wenyewe na kazi zetu ili tuweze kuwa kweli watoto wa Ufalme wa Mungu. 

Paulo katika Barua yake anatuelekeza juu ya “ni kwa jinsi gani tunapaswa kuwa katika nyumba ya Mungu”. Anawakumbusha waumini kwamba wao ni watu katika nyumba ya Mungu aliye hai, iliyodhihirishwa na Yesu, na kutangazwa na ulimwengu. Anaonesha aina Fulani ya kanuni ya Imani ambayo ilikuwa ni ishara ya Wakristo wa Mwanzo.  Kanuni hii inaonesha aina Fulani ya sifa za Yesu na matendo yake na mpango wa Mungu kwa mwanadamu kwa njia ya Yesu. 

Katika somo la Injili, Mafarisayo wanajiona wenyewe kuwa wema wanafananishwa na wale watoto wasiopenda kufanya chochote. Kama ilivyo vigumu kwa mmoja kuingia nyumba ambayo mlango wake umefungwa na madirisha kufungwa. Yesu hakuweza kuingia katika mioyo ya Mafarisayo kwasababu wameifunga na wameamua kutokuamini. Yesu na Yohane Mbatizaji walikataliwa na Mafarisayo. Injili inamalizikia kwakusema maneno haya: “Aliye na masikio na asikie” yakitutaka tuwe wasikivu na kusikiliza sauti au wito wa Yesu.  

Watoto waliokaa sokoni inatoa picha ya watu ambao muda wote wapo na mambo yao, hawana muda wa kutafakari kuhusu nafsi yao.Wanajishughulisha na biashara zao, kuwa na simu muda wote, au kukesha kwenye komputa. Maisha yetu yamejazwa na uharibifu wa kila aina. Tunajishughulisha na mambo mengi na kusahau lile la muhimu. Hali hii inatufunga sisi na kushindwa kujitambua wenyewe. 
Tutafakari leo kama maisha yetu yamekuwa ya utulivu ya kutufanya tumtambue Yesu. Je, nimekuwa msikivu kwa nafsi yangu? Je, nipo tayari kumrushusu Mungu afanye kazi katika maisha yangu? Kama sio basi fanya jitihada ya kumfuata Yesu na kustahilishwa katika ufalme Mungu. 

Sala: Bwana, ninakuomba ufungue moyo wangu. Ninakuomba nisikie sauti yako ikiniita. Yesu, nakuamini wewe. Amina.

Copyright ©2013-2024 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

No comments:

Post a Comment