Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, AGOSTI 19, 2024



MASOMO YA MISA, AGOSTI 19, 2024
JUMATATU, JUMA LA 20 LA MWAKA


SOMO 1
Eze. 24:15 – 24

Neno la Bwana linanijia tena, kusema, Mwanadamu, tazama, ninakuondolea kwa pigo moja tunu, mteule wa macho yako; walakini hutaomboleza wala kulia, wala yasichuruzike machozi yako. Ugua, lakini si kwa sauti ya kusikiwa; usifanye matanga kwa ajili yake yeye aliyekufa; jipige kilemba chako, ukavae viatu vyako, wala usiifunike midomo yako, wala usile chakula cha watu.

Basi nalisema na watu asubuhi; na jioni mke wangu akafa; nami nalifanya asubuhi kama nilivyoagizwa. Watu hao wakaniambia, Je! Hutaki kutuambia maana ya mambo haya kwetu, hata umefanya kama vile ufanyavyo.

Nikawaambia, Neno la Bwana, lilinijia, kusema, Uwaambie nyumba ya Israeli, Bwana Mungu asema hivi, Angalieni, nitapatia unajisi patakatifu pangu, fahari ya uwezo wenu, mahali pa kutamaniwa na macho yenu, ambapo roho zenu zinapahurumia; na wana wenu nab inti zenu, mliowaacha nyuma wataanguka kwa upanga. Nanyi mtafanya kama mimi nilivyofanya; hamtaifunika midomo yenu, wala kula chakula cha watu. Na vilemba vyenu vitakuwa juu ya vichwa vyenu, na viatu vyenu miguuni mwenu; hamtaomboleza wala kulia; lakini mtafifia katika maovu yenu, na kuugua kila mtu pamoja na mwenziwe. Basi ndivyo Ezekieli atakavyokuwa isahra kwenu; ninyi mtatenda sawasawa na yote aliyoyatenda yeye; litakapokuja jambo hili, ndipo mtakapojua ya kuwa mimi ndimi Bwana Mungu.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI
Kum. 32:18 – 21 (K) 18

(K) Umemsahau Mungu aliyekuzaa.

Humkumbuki Mwamba aliyekuzaa, 
Mungu aliyekuzaa umemsahau.
Bwana akaona, akawachukia,
Kwa sababu ya kukasirishwa na wanawe nab inti zake. (K)

Akasema, Nitawaficha uso wangu, 
Nitaona mwisho wao utakuwaje;
Maana, ni kizazi cha ukaidi mwingi,
Watoto wasio Imani ndani yao. (K)

Wamenitia wivu kwa kisicho Mungu;
Wamenikasirisha kwa ubatili wao;
Nami nitawatia wivu kwa wasio watu,
Nami nitawakasirisha kwa taifa lipumbaalo. (K)


SHANGILIO
1Sam. 3:9, Yn. 6:68

Aleluya, aleluya,
Nena, Bwana, kwa kuwa mtumishi wako anasikia: Wewe unayo maneno ya uzima wa milele.
Aleluya.


INJILI
Mt. 19:16 – 22

Mtu mmoja alimwendea Yesu akamwambia, Mwalimu, nitende jambo gani jema, ili nipate uzima wa milele? Akamwambia, Kwani kuniuliza habari ya wema? Aliye mwema ni mmoja. Lakini ukitaka kuingia katika uzima, zishike amri. Akamwambia, Zipi? Yesu akasema, Ni hivi, Usiue, Usizini, Usiibe, Usishuhudie uongo, Waheshimu baba yako na mama yako, na, Mpende jirani yako kama nafsi yako.

Yule kijana akamwambia, Haya yote nimeyashika; nimepungukiwa na nini tena? Yesu akamwambia, Ukitaka kuwa mkamilifu, enenda ukauze ulivyo navyo, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate. Yule kijana alipolisikia neno lile, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.


Copyright © 2024, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

No comments:

Post a Comment