“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Jumamosi, Julai 13, 2024
Tafakari ya kila siku
Juma la 14 la Mwaka wa Kanisa
Is 6: 1- 8;
Zab 92: 1-5;
Mt 10: 24 -33
USIOGOPE!
Tunaishi katika ulimwengu uliojawa wasiwasi tukiwa na hakika pia ya matukio ya kweli yanayotokea katika maisha. Tuna wasiwasi nini kitatokea kwetu tukumbanapo na ajali, au tukifilisika kifedha, au kama kutakuwa na vita, migomo au machafuko na mengine mengi. Kwa mawazo haya yaliopo mbele yetu huwa tunayaweka maisha yetu katika wasiwasi na pia kujijengea ulinzi mkubwa, pia wakati huo huo tuanasema tumeyaweka matumaini yetu kwa Yesu.
Woga na hofu tunayoiona katika maisha ya nabii Isaya, ndio hiyo hiyo inayotukumba sisi kutokana na matokeo ya maumivu ya dhambi tunazopalilia ndani mwetu. Kukabiliana na hali kama hiyo, Yesu anatutia moyo kwakusema “usiogope”. Na anatupa nguvu tunayohitaji ya kuachana na wasiwasi na hofu ya kujijengea ulinzi, na anatutaka tuweke matumaini yetu kwa Mungu ili tuweze kufurahia neema anazotujalia.
Ni Mungu mwenyewe anayetawala kiu ya roho zetu akiwasha ndani mwetu mwali wa matumani ili tumpende yeye na kumuamini yeye peke yake. Sisi tukiwa na matumaini yetu ya kweli yaliojikita kwa Mungu tunapokea fadhila na tunu za nguvu yakukabiliana na changamoto za ulimwengu na ndipo tutatangaza neno la Mungu ulimwenguni bila woga na wasiwasi. Tunu hii ya matumani inayotawala ndani mwetu inatufanya tuwe kama Kristo mwenyewe na kwa moyo wa furaha tutaitika na kujibu kwakusema “Nipo hapa Bwana, nitume mimi!”. Tukijua kwamba kazi ya kumtangaza Kristo ni kazi ya kila mbatizwa, sio kazi ya wachache. Tujitahidi sasa sisi wote kumfanya Kristo ajulikane Ulimwenguni bila kuwa na hofu na wasiwasi na tuendelee kumuomba ili tuweze kustahili kupokea kile alicho tuandalia Mbinguni.
Sala: Bwana, nisafishe dhambi yangu na ifanye safi dhamira yangu, ondoa hofu na woga moyoni mwangu, nijaze mapendo, ili niweze kuwa mfuasi wako mwaminifu. Amina.
Copyright ©2013-2024 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com
Amina🙏
ReplyDelete