Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, JULAI 7, 2024



MASOMO YA MISA, JULAI 7, 2024
DOMINIKA YA 14 YA MWAKA B

SOMO 1
Eze. 2 :2-5

Bwana aliposema nami, roho ikaniingia, ikanisimamisha; nikamsikia yeye aliyesema nami. Akaniambia, Mwanadamu, nakutuma kwa wana wa Israeli, kwa mataifa wanaoasi, walioniasi mimi, wao na baba zao wamekosa juu yangu, naam, hata hivi leo. Na wana hao wana nyuso zisizo na haya, na mioyo yao ni migumu. Mimi nakutuma kwa hao; nawe utawaambia, Bwana Mungu asema hivi. Nao, kwamba watasikia, au kwamba hawataki kusikia, (maana ndio nyumba ya kuasi hao), hata hivyo watajua ya kuwa nabii amekuwako miongoni mwao. 

Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATI KATI 
Zab. 123 (K) 2

(K) Macho yetu humwelekea Bwana, Mungu wetu.

Nimekuinulia macho yangu,
Wewe uketiye mbinguni.
Kama vile macho ya watumishi
Kwa mkono wa bwana zao.

Kama macho ya mjakazi
Kwa mkono wa bibi yake;
Hivyo macho yetu humwelekea Bwana, Mungu wetu.
Hata atakapoturehemu. (K)

Uturehemu, Ee Bwana, uturehemu sisi,
Kwa maana tumeshiba dharau.
Nafsi zetu zimeshiba mzaha wa wenye raha,
Na dharau ya wenye kiburi. (K)


SOMO 2
2 Kor 12:7-10

Makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi, kwa wingi wa mafunuo hayo nalipewa mwiba katika mwili; mjumbe wa Shetani ili anipige, nisije nikajivuna kupita kiasi. Kwa ajili ya kitu hicho nalimsihi Bwana mara tatu kwamba kinitoke. Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu.

Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.


SHANG1LIO 
Yn. 14:23

Aleluya, aleluya, 
Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake. 
Aleluya.


INJILI 
Mk. 6:1-6

Yesu alitoka, akafika mpaka nchi ya kwao, wanafunzi wake wakamfuata. Na ilipowa sabato, alianza kufundisha katika sinagogi; wengi waliposikia wakashangaa, wakisema, Huyu ameyapata wapi haya? na, Ni hekima gani hii aliyopewa huyu? Na, Ni nini miujiza hii mikubwa inayotendeka kwa mikono yake? Huyu si yule seremala, mwana wa Mariamu, na ndugu yaoYakobo, na Yose, na Yuda, na Simoni? Na maumbu yake hawapo hapa petu? Wakajikwaa kwake. Yesu akawaambia, Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake mwenyewe, na kwa jamaa zake, na nyumbani mwake. Wala hakuweza kufanya mwujiza wo wote huko; isipokuwa aliweka mikono yake juu ya wagonjwa wachache akawaponya. Akastaajabu kwa sababu ya kutokuamini kwao.

Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.


Copyright © 2024, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

1 comment:

  1. Asanteni Kwa kutukumbusha masomo ya kesho. Mungu Abariki kazi ya mikono yenu.

    ReplyDelete