MASOMO YA MISA, JULAI 3, 2024
JUMATANO, JUMA LA 13 LA MWAKA
SIKUKUU YA MTAKATIFU TOMA, MTUME
SOMO 1
Efe. 2:19-22
Tangu sasa ninyi si wageni wala wapitaji, bali ninyi ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa nyumbani mwake Mungu. Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni. Katika yeye jengo lote linaungamanishwa vema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika Bwana. Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 117 (K) Mk. 16:15
(K) Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili.
Aleluya.
Enyi mataifa wote, mhimidini.
enyi watu wote, mhimidini. (K)
Maana fadhili zake kwetu sisi ni kuu,
na uaminifu wa Bwana ni wa milele. (K)
SHANGILIO
Yn. 20 : 29
Aleluya, aleluya,
Wewe, Tomaso, kwa kuwa umeniona, umesadiki, wa heri wale wasioona, wakasadiki.
Aleluya.
INJILI
Yn. 20 :24-29
Mmoja wa wale Thenashara, Tomaso, aitwaye Pacha, hakuwako pamoja nao alipokuja Yesu Basi wanafunzi wengine wakamwambia, Tumemwona Bwana. Akawaambia, Mimi nisipoziona mikononi mwake kovu za misumari, na kutia kidole changu katika mahali pa misumari, na kutia mkono wangu katika ubavu wake, mimi sisadiki hata kidogo. Basi, baada ya siku nane, wanafunzi wake walikuwamo ndani tena, na Tomaso pamoja nao. Akaja Yesu, na milango imefungwa, akasimama katikati, akasema, Amani iwe kwenu. Kisha akamwambia Tomaso, Lete hapa kidole chako, uitazame mikono yangu; ulete na mkono wako uutie ubavuni mwangu; wala usiwe asiyeamini, bali aaminiye. Tomaso akajibu, akamwambia, Bwana wangu na Mungu wangu! Yesu akamwambia, Wewe, kwa kuwa umeniona, umesadiki; wa heri wale wasioona, wakasadiki.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 2024, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment