Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, JULAI 26, 2018



MASOMO YA MISA, JULAI 26, 2024
IJUMAA, JUMA LA 16 LA MWAKA

KUMBUKUMBU YA WAT. YOAKIM NA ANNA, WAZAZI WA BIKIRA MARIA


SOMO 1
Yer. 2:1 – 3, 7 – 8, 12 – 13

Neno la Bwana likanijia, kusema, Enenda ukalie masikioni mwa Yerusalemu, ukisema, Bwana asema hivi, Nakumbuka hisani ya ujana wako, upendo wa wakati wa uposo wako; Jinsi ulivyonifuaata huko jangwani, katika nchi isiyopandwa mbegu. Israeli walikuwa utakatifu kwa Bwana; Malimbuko ya uzao wake; Wote watakaomla watakuwa na hatia; uovu utawajilia; asema Bwana. 

Nami nitawatia katika nchi ya shibe, mpate kula matunda yake na mema yake; lakini ninyi mlipoingia katika nchi ile, mliitia unajisi nchi yangu, na urithi wangu mliufanya kuwa chukizo. Makuhani hawakusema, Yuko wapi Bwana? Wala wanasheria hawakunijua; wachungaji nao waliniasi, nao manabii walitoa unabii kwa Baali, wakafuata mambo yasiyofaidia kitu.

Enyi mbingu, staajabuni kwa ajili ya jambo hili, mkaogope sana, na kuwa ukiwa sana, asema Bwana. Kwa maana watu wangu hawa wametenda maovu mawili; wameniacha mimi, niliye chemchemi ya maji ya uzima, wamejichimbia mabirika, mabirika yavunjayo, yasiyoweza kuweka maji.

Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 36:5 – 10 (K) 9

(K) Kwako Bwana iko chemchemi ya uzima.

Ee Bwana, fadhili zako zafika hata mbinguni,
Uaminifu wako hata mawinguni.
Haki yako ni kama milimo ya Mungu,
Hukumu zako ni vilindi vikuu. (K)

Ee Bwana, unawaokoa wanadamu na wanyama.
Ee Mungu, jinsi zilivyo na thamani fadhila zako! Wanadamu huukimbilia uvuli wa mbawa zako.
Watashibishwa kwa unono wa nyumba yako,
Nawe utawanywesha mto wa furaha zako. (K)

Maana kwako Wewe iko chemchemi ya uzima,
Katika nuru yako tutaona nuru.
Uwadumishie wakujuao fadhili zako,
Na wanyofu wa moyo uaminifu wako. (K)


SHANGILIO
Zab. 147:12, 15

Aleluya, aleluya, 
Msifu Bwana, ee Yerusalemu, huipeleka amri yake juu ya nchi.
Aleluya.


INJILI
Mt. 13:10 – 17

Wanafunzi walimwambia Yesu, Kwa nini wasema nao kwa mifano? Akajibu akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuzijua siri za ufalme wa mbinguni, bali wao hawakujaliwa. Kwa maana yeyote mwenye kitu atapewa, naye atazidishiwa tele; lakini yeyote asiye na kitu, hata kile alichonacho hata kile alicho nancho atanyang’anywa. Kwa sababu hii nasema nao kwa mifano kwa kuwa wakitazama hawaoni, na wakisikia hawasikii, wala kuelewa. Na neno la nabii Isaya linatimia kwao, likisema, Kusikia mtasikia, wala hamtaelewa; kutazama mtatazama, wala hamtaona. Maana mioyo ya watu hawa imekuwa mizito, na kwa masikio yao hawasikii vema, na macho yao wameyafumba; wasije wakaona  kwa macho yao, wakasikia kwa masikio yao, wakaelewa kwa mioyo yao, wakaongoka, nikawaponya.
Lakini, heri macho yenu, kwa kuwa yanaona; na masikio yenu, kwa kuwa yanasikia. Kwa maana, amin, nawaambia, Manabii wengi na wenye haki walitamani kuyaona mnayoyaona ninyi, wasiyaone na kuyasikia mnayoyasikia ninyi, wasiyasikie.

Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.


Copyright © 2024, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

No comments:

Post a Comment