MASOMO YA MISA, JULAI 18, 2022
JUMATATU, JUMA LA 16 LA MWAKA
SOMO 1
Mik. 6:1 – 4, 6 – 8
Sikieni asemavyo Bwana; Simama, ujitetee mbele ya milima, vilima navyo na visikie sauti yako. Sikieni, enyi milima, mateto ya Bwana, na ninyi, enyi misingi ya dunia iliyo imara; kwa maana Bwana ana mateto na watu wake, naye atahujiana na Israeli. Enyi watu wangu, nimewatenda nini? Nami nimewachosha kwa habari gani? Shuhudieni juu yangu. Kwa maana nalikupandisha kutoka nchi ya Misri, na kukukomboa utoke katika nyumba ya utumwa, nami naliwapeleka Musa, na Haruni, na Miriamu, watangulie mbele yako.
Nimkaribie Bwana na kitu gani, na kuinamana mbele za Mungu aliye juu? Je! Nimkaribie na sadaka za kuteketezwa, na ndama za umri wa mwaka mmoja? Je! Bwana atapendezwa na elfu za kondoo waume, au na elfu kumi za mito ya mafuta? Je! Nimtoe mzaliwa wangu wa kwanza kwa kosa langu, mzao wa mwili wangu kwa dhambi ya roho yangu? Ee mwanadamu, yeye amekuonyesha yaliyo mema; na Bwana anataka nini kwako, ila kutenda haki, na kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako!
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 50:5 – 6, 8 – 9, 16 – 17, 21, 23 (K) 23
Nikusanyieni wacha Mungu wangu,
Waliofanya agano nami kwa dhabihu.
Na mbingu zitatangaza haki yake,
Kwa maana Mungu ndiye aliye hakimu. (K)
Sitakukemea kwa ajili ya dhabihu zako,
Na kafara zako ziko mbele zangu daima.
Sitatwaa ng’ombe katika nyumba yako,
Wala beberu katika mazizi yako. (K)
Mtu asiye haki, Mungu amwambia,
Una nini wewe kuitangaza sheria yangu.
Maana wewe umechukia maonyo,
Na kuyatupa maneno yangu nyuma yako. (K)
Ndivyo ulivyofanya, nami nikanyamaza,
Ukadhani ya kuwa Mimi ni kama wewe.
Atoaye dhabihu za kushukuru ndiye anayenitukuza,
Nitamwonyesha wokovu wa Mungu. (K)
SHANGILIO
Yn. 17:17
Aleluya, aleluya,
Neno lako ndiyo kweli, ee Bwana, ututakase kwa ile kweli.
Aleluya.
INJILI
Mt. 12: 38 – 42
Baadhi ya waandishi wa Mafarisayo walimjibu Yesu wakasema, Mwalimu, twataka kuona ishara kwako. Akajibu, akawaambia, Kizazi kibaya na cha zinaa chatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya nabii Yona. Kwani kama vile Yona alivyokuwa siku tatu mchana na usiku katika tumbo la nyangumi, hivyo ndivyo Mwana wa Adamu atakavyokuwa siku tatu mchana na usiku moyo wa nchi. Watu wa Ninawi watasimama siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, nao watawahukumu kuwa wamekosa; kwa sababu wao walitubu kwa mahubiri ya Yona; na hapa yupo aliye mkuu kuliko Yona. Malkia wa kusini atasimama siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, naye atawahukumu kuwa wamekosa; kwa sababu yeye alikuja kutoka pande za mwisho za dunia ili asikie hekima ya Sulemani, na hapa yupo aliye mkuu kuliko Sulemani.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 2022, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com
No comments:
Post a Comment