Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MAPENZI YA MUNGU!



“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya kila siku
Jumanne, Julai 23, 2024, 
Juma la 16 la Mwaka wa Kanisa


Mik 7: 14-15, 18-20; 
Zab 85: 2-8; 
Mt 12: 46-50


MAPENZI YA MUNGU!


Somo la Injili ya leo linatoa nafasi ya kuongea kuhusu Bikira Maria. Wengi wanaosoma sehemu hii ya injili hudhani kwamba Yesu alikuwa akijiweka mbali na Mama yake au kumtenga Mama yake. Lakini ukweli ni kwamba maneno ya Yesu yanatangaza ukweli zaidi kuliko maneno mengine. Kwasababu yanaeleza ni kwa jinsi gani mmoja anaweza kuwa mmoja katika familia yake. Na hili linatokea pale mmoja “anapofanya mapenzi ya Baba yake”. Ni nani aliyefanya mapenzi ya Mungu kama Bikira Maria? Ni nani aliyekuwa mtii kwa Mungu zaidi ya Bikira Maria? Hakuna hata mmoja. Alitenda kwa utii mkamilifu siku zote za maisha yake, na hivyo alitimiza vigezo vyakuwa mmoja katika familia ya Yesu. Maria ni Mwanadamu pekee aliyeshiriki moja kwa moja kwenye Mwili wa Kristo. Lakini Yesu anatutaka sisi wote tuweze kuwa katika familia yake. Tunaweza kuwa kaka zake, dada zake, baba zake na Mama zake kwa kufanya mapenzi ya Mungu. 

Tafakari leo juu ya kazi aliyonayo Mama Maria katika maisha yetu. Mungu anakutaka wewe umuheshimu, kumuiga na kumfanya mmoja wa familia yako. Anataka wewe umpokee kama mama yako wa kiroho kwasababu wewe ni mmoja katika familia yake. Kama unajitahidi kuwa mtii kwa Mungu na kutenda mapenzi yake utashiriki pia katika baraka za maisha yake. Moja wapo wa hizo baraka ni Bikira Maria kuwa Mama yako. Huwezi kuwa mmoja wa Familia ya Yesu alafu umkatae mama yake.

Sala: Bwana, ninatamani kuwa mtii kwako na kutenda mapenzi yako katika kila kitu. Ninatamani kukumbatia daima mapenzi kamili ya Mungu katika maisha yangu. Katika kutenda mapenzi haya Matakatifu, nisaidie niweze kushiriki kikamili na kuwa mmoja wa familia yako kikamilifu. Yesu, nakuamini wewe. Maria Mtakatifu Mama wa Mungu tunakuomba sisi tuweze kuwa karibu na Mwanao Yesu, kwa kutenda mapenzi yake muda wote. Amina.


Copyright ©2013-2024 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

No comments:

Post a Comment