“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Ijumaa, Julai, 12, 2024
Tafakari ya kila siku
Juma la 14 la Mwaka wa Kanisa
Hos 14: 2-10;
Zab 50: 3-4, 8-9, 12-14, 17;
Mt 10: 16-23
KONDOO NA MBWA MWITU!
“Mti unaozaa matunda mazuri hupigwa mawe mengi”; vile vile Mkristo anayeshika kiaminifu tunu za Injili anapata mateso mengi. Katika Injili ya leo Yesu anatupa maelekezo nini cha kufanya wakati wa mambo kama hayo yanapotokea kwetu. “Nina watuma kama kondoo kati ya mbwa mwitu”. Yesu anatuita kondoo kwasababu hatutumii fujo wala vita, bali tunatumia ujumbe wa upendo, msamaha, Amani na haki kama silaha ya kuwatibia maadui na watesi wetu. Tunu hizi za kiroho mara nyingi kwao zinakuwa sumu na wanakuwa na hasira zaidi nakutaka kutuangamiza, lakini Yesu anatuambia ndio njia sahihi kabisa yenye tabia za Kimungu.
Pili, “Muwe na busara kama nyoka wenye upole kama njiwa”. Tunapaswa kuwa wabunifu na wenye kuzaa matunda mema kawasababu tutakukumbana na mambo ya ulimwengu bila hivyo tunaweza kutekwa na kuanza kuwa kama wa ulimwengu pia.
Tatu, “msiwe na wasiwasi mtasema nini au mtasema namna ghani”. Roho Mtakatifu aliyewashukia Mitume siku ile ya Pentekoste na kuwajaza nguvu wakatao ushuhuda juu ya Kristo atawaimarisha na ninyi pia. Sisi pia tumempokea Roho Mtakatifu kwa ubatizo wetu, atatuongoza na ataongea ndani mwetu wakati tunavyo ulizwa maswali na mamlaka ya ulimwengu huu, kama tuta shirikiana naye. Kwa nguvu zetu wenyewe bila msaada wake tutashindwa.
Neno la Kristo linatutia nguvu na kututia moyo katika hali ya vitisho na misukosuko yahusuyo Imani yetu. Kama Wafuasi wa Yesu mmoja wetu anaweza kupatwa na changamoto katika maisha, labda kuhukumiwa bila hatia, kuvunjika kwa familia, au kuonewa na kutengwa na jamii na mengine mengi. Katika nyakati hizi mmoja hapaswi kuwa kama mbwa mwitu (hasira, kulaumu na kulaani) , bali anapaswa kuwa kama kondoo akiendelea kuzishika tunu za Injili na kutoa ushuhuda wa Yesu kwa ujasiri na hekima. Yote yakiwa yametimilika katika mapendo ya Kristo, lengo la maisha yetu litakuwa limetimilika na tutapata tuzo katika maisha ya umilele.
Sala: Bwana wangu, nifanye mimi nitambue njia yako na uniongoze katika njia hiyo ili niweze kufuata kiaminifu neno lako na kuwa shuhuda wako. Amina.
Copyright ©2013-2024 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com
No comments:
Post a Comment