Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

SAMEHE KUTOKA MOYONI!


“ASALI ITOKAYO MWAMBANI
Alhamisi, Juni 13, 2024,
Tafakari ya kila siku 
Juma la 10 la Mwaka wa Kanisa

Kumbukumbu ya Mtakatifu Antoni wa Padua, Mwalimu wa Kanisa


1Fal 18:41-46; 
Zab 64:10-13; 
Mt 5:20-26


SAMEHE KUTOKA MOYONI!


Dhambi haitokei tuu alimradi, inakuwa kwanza ndani ya moyo wa mtu kama mbegu. Isipo ondolewa na neema ya Mungu, inakuwa kama magugu nakuondoa uzima ndani yetu. Yesu anatuonesha moyo kama sehemu panapotoka tamaa mbaya, moyo unachagua na kutoa lengo. Tamaa zetu mbaya zisipo ondolewa ndani ya mioyo yetu na kungolewa, moyo unatiwa sumu na kuwa mtumwa wa tamaa hizo. Yesu anaelezea hili kwa mfano wa amri ya usiue. Kuua kwanza kunaanzia ndani ya moyo kama mbegu ya hasira mbaya na inakuwa na kutawanywa kwa maneno na baadae vitendo dhidi ya ndugu yako. Hii ni hasira mbaya inayoanza taratibu na mtu hukaa nayo kwa muda mrefu, anailea ndani yake na kutengeneza, vinyongo na kuipasha joto kwa laana na baadae inakataa kutoka ndani yake. 

Kwa hiyo Yesu anatuonya tuepuke hasira hii, tuingoe ndani ya mioyo yetu kwakupokea huruma yake. Je, tutumie nini ili tuweze kukwepa hasira hii na laana? Tunapaswa kuwa na huruma, tujitawale, na kuwa mtu wakujali uzuri wa wengine, haya yote yanatoka kwenye moyo uliojaa huruma na msamaha. Sisi wote tunapenda Mungu atusamehe makosa yetu ili tuishi bila hatia mbele zake, basi nasi tuwe wakwanza kuwasamehe ndugu zetu, wanapotukosea, tusiwaue kwakuwasema na kuwasengenya na kuwasingizia uongo. Kwakufanya hivyo tutajifungia neema za Mungu sisi wenyewe.

Sala: Bwana Yesu moyo wangu ni baridi. Naomba uupashe tena joto, uwe wenye huruma na wenye kutoa msamaha kwa wote, hata kwa wale walioniumiza sana. Naomba tu niwaze na kusema yale yanayokupendeza na kuwa mtu mwenye mapendo kwa wote ninao kutana nao. Amina


Copyright ©2013-2024 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

No comments:

Post a Comment