Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, JUNI 8, 2024


MASOMO YA MISA, JUNI 8, 2024
JUMAMOSI, JUMA LA 9 LA MWAKA

KUMBUKUMBU YA MOYO SAFI WA BIKIRA MARIA

SOMO 1
Isa. 61:9-11

Kizazi chao kitajulikana katika mataifa, na uzao wao katika kabila za watu; wote wawaonao watakiri ya kuwa wao ni kazazi kilichobarikiwa na Bwana. Nitafurahi sana katika bwana, nafsi yangu itashangilia katika Mungu wangu; maana amenivika mavazi ya wokovu, amenifunika vazi la haki, kama bwana rusi ajipambavyo kwa kilemba cha maua, na kama bibi harusi ajipambavyo kwa vyombo vya dhahabu. Maana kama nchi itoavyo machipuko yake, na kama bustani ioteshavyo vitu vilivyopandwa ndani yake; ndivyo Bwana Mungu atakavyootesha haki na sifa mbele ya mataifa yote.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI
1 Sam. 2:1, 4-8 (K) 1

(K) Moyo wangu wamshangilia Bwana.

Moyo wangu wamshangilia Bwana, 
Pembe yangu imetukuka katika Bwana,
Kinywa change kimepanuka juu ya adui zangu;
Kwa kuwa naufurahia wokovu wako. (K)

Pinde zao mashujaa zimevunjika,
Na hao waliojikwaa wamefungiwa nguvu.
Walioshiba wamejikodisha ili kupata chakula,
Na hao waliokuwa na njaa wamepata raha.
Naam, huyo aliyekuwa tasa amezaa watoto saba,
Na yeye aliye na wana wengi amedhoofika. (K)

Bwana huua, naye hufanya kuwa hai;
Hushusha hata kuzimu, tena huleta juu.
Bwana hufukarisha mtu, naye hutajirisha;
Hushusha chini, tena huinua juu. (K)

Humwinua mnyonge kutoka mavumbini,
Humpandisha mhitaji kutoka jaani,
Ili awaketishe pamoja na wakuu,
Wakakirithi kiti cha enzi cha utukufu. (K)

INJILI
Lk. 2:41-51

Wazee wa Yesu huenda Yerusalemu kila mwaka, wakati wa sikukuu ya Pasaka. Na alipopata umri wake miaka kumi na miwili, walipanda kama ilivyokuwa desturi ya sikukuu; na walipokwisha kuzitimiza siku, wakati wa kurudi kwao, yule mtoto Yesu alibaki nyuma huko Yerusalemu, na wazee wake walikuwa hawana habari. Nao wakadhani ya kuwa yumo katika msafara; wakaenenda mwendo wa kutwa, wakawa wakimtafuta katika jamaa zao na wenzao; na walipomkosa, wakarejea Yerusalemu, huku wakimtafuta.

Ikawa baada ya siku tatu wakamwona hekaluni, ameketi katikati ya waalimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. Nao wote waliomsikia walistaajabia fahamu zake na majibu yake. Na walipomwona walishangaa, na mama yake akamwambia, Mwanangu, mbona umetutenda hivi? Tazama, baba yako na mimi tulikuwa tukikutafuta kwa huzuni. Akawaambia, Kwani kunitafuta? Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu? Nao hawakuelewa na neno hilo alilowaambia.

Akashuka pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii; na mamaye aliyaweka hayo yote moyoni mwake. Naye Yesu akazidi kuendelea katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu. 

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo. 

Copyright © 2024, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment