Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, JUNI 7, 2024



MASOMO YA MISA, JUNI 7, 2024
IJUMAA YA 9 YA MWAKA

SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU KRISTO


SOMO 1 
Hos. 11 : l, 3-4, 8-9

Israeli alipokuwa mtoto, nalikuwa nikimpenda, nikamwita mwanangu atoke Misri. Lakini nalimfundisha Efraimu kwenda kwa miguu; naliwachukua mikononi mwangu; hawakujua ya kuwa naliwaponya. Naliwavuta kwa kamba za kibinadamu, kwa mafungo ya upendo; nami nalikuwa kwao kama hao waondoao kongwa tayari mwao, nikaandika chakula mbele yao.

Moyo wangu umegeuka ndani yangu, huruma zangu zimewaka pamoja. Sitatumia ukali wa hasira yangu, sitarudi kumvvangamiza Efraimu; kwa maana mimi ni Mungu, si mwanadamu mimi; mimi ndiye aliye Mtakatifu katikati yenu; wala sitaingia ndani ya mji.

Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI 
Isa. 12:2-6 (K) 3

(K) Basi, kwa furaha mtateka maji katika visima vya wokovu.

Tazama, Mungu ndiye wokovu wangu;
Nitatumaini wala sitaogopa;
Maana Bwana Yehova ni nguvu zangu na wimbo wangu;
Basi, kwa furaha mtateka maji katika visima vya wokovu. (K)

Na katika siku hiyo mtasema,
Mshukuruni Bwana, liitieni jina lake;
Yatangazeni matendo yake kati ya mataifa,
Litajeni jina lake kuwa limetukuka. (K)

Mwimbieni Bwana, kwa kuwa ametenda makuu;
Na yajulikane haya katika dunia yote.
Paza sauti, piga kelele, mwenyeji wa Sayuni;
Maana Mtakatifu wa Israeli ni mkuu kati yako. (K)


SOMO 2 
Efe. 3: 8-12, 14-19

Mimi, niliye mdogo kuliko yeye aliye mdogo wa watakatifu wote, nalipewa neema hii ya kuwahubiri Mataifa utajiri wake Kristo usiopimika; na kuwaangaza watu wote wajue habari za madaraka ya siri hiyo, ambayo tangu zamani zote ilisitirika katika Mungu aliyeviumba vitu vyote; ili sasa, kwa njia ya kanisa, hekima ya Mungu iliyo ya namna nyingi ijulikane na falme na mamlaka katika ulimwengu wa roho; kwa kadiri ya kusudi la milele alilolikusudia katika Kristo Yesu Bwana wetu. Katika yeye tunao ujasiri na uwezo wa kukaribia katika tumaini kwa njia ya kumwamini.

Kwa hiyo nampigia Baba magoti, ambaye kwa jina lake ubaba wote wa mbinguni na wa duniani unaitwa, awajalieni, kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake, kufanywa imara kwa nguvu, kwa kazi ya Roho wake, katika utu wa ndani. Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani mkiwa na shina na msingi katika upendo; ili mpate kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, na urefu, na kimo, na kina; na kuujua upendo wake Kristo, upitao ufahamu kwa jinsi ulivyo mwingi, mpate kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu. Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya marnbo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu; naam, atukuzwe katika Kanisa na katika Kristo Yesu hata vizazi vyote vya milele na milele. Amina.

Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.


SHANGILIO 
1 Yoh. 4:10

Aleluya, aleluya, 
Hili ndilo pendo, si kwamba sisi tulimpenda Mungu, bali kwamba yeyc alitupenda sisi, akatuma Mwanawe kuwa kipatanisho kwa dhambi zetu. 
Aleluya.


INJILI
Yn. 19:31-37

Wayahudi, kwa sababu ni Maandalio, miili isikae juu ya misalaba siku ya sabato, (maana sabato ile ilikuwa siku kubwa) walimwomba Pilato miguu yao ivunjwe, wakaondolewe. Basi askari wakaenda wakamvunja miguu wa kwanza, na wapili, aliyesulibiwa pamoja naye. Lakini walipomjia Yesu na kuona ya kuwa amekwisha kufa, hawakumvunja miguu; lakini askari mmojawapo alimehoma ubavu kwa mkuki; na mara ikatoka damu na maji. Naye aliyeona ameshuhudia, na ushuhuda wake ni kweli; naye anajua ya kuwa anasema kweli ili ninyi nanyi mpate kusadiki. Kwa maana hayo yalitukia ili andiko litimie, Hapana mfupa wake utakaovunjwa. Na tena andiko lingine lanena, Watamtazama yeye waliyemchoma. 

Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.


Copyright © 2024, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment