Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA JUNI 5, 2024



MASOMO YA MISA JUNI 5, 2024
JUMATANO, JUMA LA  9  LA MWAKA

KUMBUKUMBU YA MTAKATIFU BONIFASI


SOMO 1
2Tim. 1:1-3, 6-12

Paulo, mtume wa Kristo Yesu, kwa mapenzi ya Mungu; kwa ajili ya ahadi ya uzima ulio katika Kristo Yesu; kwa Timotheo, mwanangu mpendwa. Neema na iwe kwako, na rehema, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Bwana wetu.

Namshukuru Mungu, nimwabuduye kwa dhamiri safi tangu zamani za wazee wangu, kama vile nikukumbukavyo wewe daima, katika kuomba kwangu usiku na mchana.

Kwa sababu hiyo nakukumbusha, uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu. Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi. Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, wala usinionee haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu; ambaye alituokoa akatuita kwa mwito mtakatifu, si kwa kadiri ya matendo yetu sisi, bali kwa kadiri ya makusudi yake yeye na neema yake. Neema hiyo tulipewa katika Kristo Yesu tangu milele, na sasa inadhihirishwa kwa kufunuliwa kwake Mwokozi wetu Kristo Yesu; aliyebatili mauti, na kuufunua uzima na kutokuharibika, kwa ile Injili; ambayo kwa ajili ya hiyo naliwekwa niwe mhubiri na mtume na mwalimu.

Kwa sababu hiyo nimepatikana na mateso haya, wala sitahari; kwa maana namjua yeye niliyemwamini, na kusadiki ya kwamba aweza kukilinda kile nilichokiweka amana kwake hata siku ile.

Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 123:1-2 (K) 1

(K) Nimekuinulia macho yangu, ee Bwana.

Nimekuinulia macho yangu, 
Wewe uketiye mbinguni.
Kama vile macho ya watumishi 
Kwa mkono wa bwana zao. (K)

Kama macho ya mjakazi
Kwa mkono wa bibi yake;
Hivyo macho yetu humwelekea Bwana, Mungu wetu.
Hata atakapoturehemu. (K)


SHANGILIO
Lk. 8:15

Aleluya, aleluya.
Wanabarikiwa wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao hulisikia neno la Mungu, na kulishika.
Aleluya.


INJILI 
Mk. 12:18-27

Masadukayo, watu wasemao ya kwamba hakuna kiyama, walimwendea Yesu, wakamwuliza na kusema, Mwalimu, Musa alituandikia ya kwamba ndugu ya mtu akifa, akamwacha mkewe wala hana mtoto, ndugu yake amtwae yule mkewe akampatie ndugu yake mzao. Basi kulikuwa na ndugu saba; wa kwanza akatwaa mke, akafa, asiache mzao. Wa pili naye akamtwaa akafa, wala yeye hakuacha mzao. Na wa tatu kadhalika; hata na wote saba, wasiache mzao. Mwisho wa wote yule mwanamke akafa naye. Basi, katika kiyama atakuwa mke wa yupi katika hao? Maana wote saba walikuwa naye.

Yesu akajibu, akawaambia, Je! hampotei kwa sababu hii, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu? Kwa maana watakapofufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi, bali huwa kama malaika walioko mbinguni. Na kwa habari ya wafu ya kwamba wafufuliwa, hamjasoma katika kitabu cha Musa, Sura ya Kijiti, jinsi Mungu alivyomwambia, akisema, Mimi ni Mungu wa Ibrahi- mu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo? Yeye si Mungu wa wafu, bali wa walio hai. Hivyo mwapotea sana.

Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo. 


Copyright © 2024, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment