MASOMO YA MISA, JUNI 22, 2024
JUMAMOSI, JUMA LA 11 LA MWAKA
SOMO 1
Nya. 24:17 – 25
Baada ya kufa kwake Yehoyada,
wakuu wa Yuda wakamwendea mfalme, wakamsujudia. Naye mfalme akawasikiliza
maneno yao. Wakaiacha nyumba ya Bwana, mungu wa baba zao; wakatumikia maashera
na sanamu; ghadhabu ikawajia Yuda na Yerusalemu kwa sababu ya hiyo hatia yao.
Hata hivyo akawapelekea manabii, ili kuwarudisha kwa Bwana; nao wakawashuhudia;
lakini hawakukubali kuwasikiliza.
Na roho ya Mungu ikamjia
Zekaria, mwana wa Yehoyada, kuhani; naye akasimama juu ya watu, akawaambia,
Mungu asema hivi, Kwani ninyi kuzihalifu amri za Bwana, hata msiweze
kufanikiwa? Kwa kuwa mmemwacha Bwana, yeye naye amewaacha ninyi. Basi,
wakafanya shauri juu yake, wakampiga kwa mawe kwa amri ya mfalme, katika ua wa
nyumba ya Bwana. Basi hivyo mfalme Yoashi hakuukumbuka wema, ambao Yehoyada,
baba yake, alimfanyia, bali alimwua mwanawe. Naye alipokufa, alisema, Bwana na
ayaangalie haya, akayatakie kisasi.
Ikawa mwisho wa mwaka, wakakwea
juu yake jeshi la Washami; wakafika Yuda na Yerusalemu, wakawaangamiza wakuu wa
watu wote miongoni mwa watu, wakamletea mfalme wa Dameski nyara zao zote. Maana
wakaja jeshi la Washami watu haba; Bwana akatia mikononi mwao jeshi kubwa mno,
kwa sababu wamemwacha Bwana, Mungu wa baba zao.
Hivyo wakamfanyia Yoashi
hukumu. Hata walipoondoka kwake, (nao walimwacha ameshikwa sana na maradhi)
watumishi wake mwenyewe wakamfanyia fitina kwa ajili ya damu ya mwana wa
Yehoyada kuhani, wakamwua kitandani pake, akafa; wakamzika mjini mwa Daudi,
lakini hawakumzika katika makaburi ya wafalme.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 89: 3- 4, 28 – 33 (K) 28
(K) Nitamwekea fadhili zangu
milele.
Nimefanya agano na mteule
wangu,
Nimemwapa Daudi, mtumishi
wangu.
Wazao wako nitawafanya imara
milele,
Nitakijenga kiti chako cha enzi
hata milele. (K)
Hata milele nitamwekea fadhili
zangu,
Na agano langu litafanyika
amini kwake.
Wazao wake nao nitawadumisha
milele,
Na kiti chake cha enzi kama
siku za mbingu. (K)
Wanawe wakiiacha sheria yangu,
Wasiende katika hukumu zangu,
Wakizihalifu amri zangu,
Wasiyashike maagizo yangu. (K)
Basi, nitawarudi makosa yao kwa
fimbo,
Na uovu wao kwa mapigo.
Lakini fadhili zangu
sitamwondolea yeye,
Wala sitafanya uaminifu wangu
kuwa uongo. (K)
SHANGILIO
Zab. 119: 135
Aleluya, aleluya,
Umwangazie mtumishi wako uso
wako, na kunifundisha amri zako.
Aleluya.
INJILI
Mt. 6: 24 – 34
Yesu aliwaambia wanafunzi wake:
Hkuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili, kwa maana atamchukia huyu, na
kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia
Mungu na mali.
Kwa sababu hiyo nawaambieni,
Msisumbukie maisha yenu, mle nini au mnywe nini; wala miili yenu, mvae nini.
Maisha je! Si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi? Waangalieni ndege wa
angani, ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na Baba
yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je! Si bora kupita hao? Ni yupi kwenu
ambaye akijisumbua aweza kujiongoeza kimo chake hata mkono mmoja? Na mavazi, ya
nini kuyasumbukia? Fikirini maua ya mashamba, jinsi yameavyo; hayafanyi kazi,
wala hayasonkoti; nami nawaambia, ya kwamba hata Sulemani katika fahari yake
yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo la hayo.
Basi, ikiwa Mungu huyavika hivi
majani ya kondeni, yaliyopo leo, na kesho hutupwa kalibuni, je! Hatazidi sana
kuwavika ninyi, enyi wa imani haba? Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au
Tunywe nini? Au Tuvae nini? Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu
Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote. Bali utafuteni kwanza
ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.
Basi msisumbukie ya kesho; kwa
kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 2024, "MASOMO
YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings
reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:
Post a Comment